Mapigano yasitishwa Hodeida

0

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, – Mike Pompeo amesifu usitishwaji wa mapigano katika mji wa bandari wa Hodeida uliopo nchini Yemen.

Hatua hiyo ya usitishwaji mapigano imefikiwa baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya kutafuta amani nchini Yemen yaliyokuwa yakifanyika nchini Sweden kati  ya waasi wa Houthi na wawakilishi wa serikali.

Pompeo amesema kuwa licha ya kuwa bado yanahitajika majadiliano zaidi baina ya pande hizo mbili, lakini masuala yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya pande hizo ni  muhimu.

Amempongeza mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, – Martin Griffiths pamoja na mataifa Sweden na Saudi Arabia kwa kuwezesha kufanyika kwa mazungumzo hayo.

 

Ghasia zasababisha vifo Somalia

0

Watu 11 wamethibitika kufa katika jimbo la Baidoa nchini Somalia kufuatia ghasia zilizozuka baada ya kukamatwa kwa Kamanda wa zamani wa Wanamgambo wa Al-Shabab, –  Mukhtar Robow.

Miongozi mwa watu waliokufa katika ghasia hizo ni Mbunge wa jimbo hilo la Baidoa.

Mbali na vifo, ghasia hizo pia zimesababisha hasara ya mali ikiwa ni pamoja na magari kuchomwa moto na kuharibiwa kwa majengo mbalimbali.

Miezi miwili iliyopita, serikali ya Somalia ilimzuia Robow kushiriki katika kinyang’anyiro cha Ubunge katika jimbo la Baidoa lakini Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimpa ruhusu ya kushiriki katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa muda mrefu, serikali ya Somalia imekua ikimshutumu Robow na kusema kuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa  Taifa hilo.

Kamanda huyo wa zamani wa Wanamgambo wa Al-Shabab wa nchini Somalia, –  Mukhtar Robow ana umri wa miaka 46 na alipata mafunzo yake ya kigaidi nchini Afghanistan, mafunzo  yaliyomuwezesha kuwa miongoni mwa waanzilishi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Jamii yatakiwa kuwasaidia wenye uhitaji

0

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson ametoa wito kwa jamii nchini kuendelea kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Dkt Tulia ametoa wito katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam, alipofika kwa lengo la kukabidhi msaada wa viti mwendo viwili, pesa taslimu zaidi ya Shilingi Milioni Sita, kitanda na godoro  kwa mtoto Amos Gabriel mkazi wa jiji la Mbeya aliyeanguka kutoka juu ya mti na  kuvunjika uti wa mgongo.

Pia amewashukuru watu wote waliojitokeza na kumsaidia mtoto Amos na kuwataka Watanzania wote wenye mapenzi mema kujitokeza na kuwasaidia wenye uhitaji.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Ackson  ndiye aliyemsafirisha Mtoto Amos kutoka jijini Mbeya kwenda jijini  Dar es salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Tukio la kuanguka kwa mtoto Amos lilitangazwa na TBC kupitia kipindi chake cha  televisheni cha  Wape Nafasi na hivyo kusababisha wadau mbalimbali kujitokeza na kumpatia msaada.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania Dkt Ayub Rioba amewashukuru Watanzania kwa ukarimu waliouonyesha katika kumsaidia mtoto Amos na wengine wanaohitaji misaada ya aina mbalimbali.

Amos mwenyewe amewashukuru watu wote waliompatia msaada na kuwashauri watu wenye ulemavu kutokana tamaa, bali wafanye bidii ili kutimiza ndoto zao.

Mtoto Amos mwenye umri wa miaka Kumi na Minne  alivunjika uti wa mgongo baada ya kuanguka kutoka juu ya mti  alipotumwa kukata fimbo akiwa shuleni mwezi wa Aprili mwaka huu.

 

Njoya ahaidi kuendeleza soka la Cameroon

0

Rais mpya wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini Cameroon (FECAFOOT), – Seidou Njoya amesema kuwa lengo lake ni kurejesha uaminifu kwenye soka la nchi hiyo.

Njoya ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili tu tangu achaguliwe kuwa Rais wa FECAFOOT na kuongeza kuwa atafanikisha lengo hilo kwa kuupa kipaumbele uwazi katika uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu nchini Cameroon.

FECAFOOT imekuwa haina Rais tangu mwaka 2013 baada ya aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo Iya Mohammed kuhukumiwa kifungo jela, hali iliyosababisha shirikisho hilo kuendeshwa na kamati maalumu kwa kipindi cha miaka mitano.

Njoya amesema kuwa baada ya miaka mitano ya mvutano kwenye soka la nchi hiyo, umefika wakati wa kufanya mabadiliko kwa kufuata weledi na utawala bora kwenye soka.

Kwenye uchaguzi uliomuingiza madarakani Njoya siku ya Jumatano, kigogo huyo mwenye umri wa miaka 57 alipata kura 46 kati ya 66 huku mpinzani wake wa karibu akiwa mlinda mlango wa zamani wa timu ya Taifa ya Cameroon, -Joseph Bell akipata kura 17.

Giresse kocha mpya Tunisia

0

Shirikisho la soka nchini Tunisia limemteua nyota wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa, – Alain Giresse kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa kuchukua nafasi ya Faouzi Benzarti.
Benzarti alitimuliwa kazi mwezi Oktoba mwaka huu, siku nne tu tangu alipokipeleka kikosi cha Taifa hilo katika fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2019 ambazo mpaka sasa bado haijajulikana zitafanyikia wapi.

Giresse anayechukua nafasi ya Benzarti ataanza rasmi kukinoa kikosi cha Tunisia Januari Mosi mwaka 2019 huku mkataba wake ukitarajiwa kufikia kikomo Juni 2020.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 66, ana uzoefu wa kutosha kwenye soka la Afrika ambapo amevinoa vikosi vya mataifa ya Gabon, Senegal na Mali ambayo ameifundisha mara mbili.

Mapema mwaka huu, kocha huyo pia alikuwa akihusishwa kwenda kukinoa kikosi cha timu ya Taifa ya Cameroon lakini nafasi hiyo ilichukuliwa na Clarence Seedorf akisaidiana na Patrick Cluivert.

Eritrea na Somalia kuimarisha uhusiano

0

Rais Isaias Afwerki wa Eritrea yuko mjini Mogadishu nchini Somalia kwa ziara ya kikazi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Nchi za Somalia na Eritrea zimeamua kufufua uhusiano wa kidiplomasia kwa maslahi ya raia wa mataifa hayo mawili.

Kwa miaka kumi na mitano, mataifa hayo mawili yamekuwa hayana uhusiano wa kidiplomasia.

Somalia imekuwa ikiishutumu Eritrea kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa Al Shabaab wa nchini Somalia.

Nchi hizo mbili zilitiliana saini kuanza rasmi uhusiano wa kidiplomasia mwezi Julai mwaka huu.

Chaneli mpya ya Utalii kuzinduliwa Disemba 15

0

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini wanatarajia kuzindua chaneli mpya ya utalii itakayojulikana kama Tanzania Safari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt Ayub Rioba amesema kuwa chaneli hiyo itakayozinduliwa Disemba 15 mwaka huu ni fursa kwa Watanzania kuvifahamu vivutio  vya utalii vinavyopatikana Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, –  Dkt Abdulla Mohammed Juma amesema kuwa chaneli hiyo ya Utalii ni muhimu katika kuleta mabadiliko katika sekta ya utalii nchini.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro (NCAA) Dkt Freddy Manongi amesema kuwa kuanzishwa kwa chaneli hiyo ya utalii itakayojulikana kama Tanzania Safari kunatoa fursa kwa Watanzania kujua mambo mengi yanayohusu utalii.

Profesa Dos Santos Silayo ni Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) ambaye amesema kuwa suala la Utalii linaenda pamoja na uhifadhi wa mazingira, hivyo kuanzishwa kwa chaneli ya Utalii kutasaidia kutoa elimu kuhusu mazingira.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa Chaneli mpya ya Utalii anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Moto wazua taharuki DRC

0

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) imesema kuwa uharibifu uliotokea baada ya kuteketea kwa moto kwa  majengo yanayotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi  katika  Jamhuri hiyo ni mkubwa.

Waziri wa wizara hiyo Henri Sakanyi amesema kuwa majengo hayo yaliyopo katika mji wa Kinshasa  yameteketea kwa moto majira ya usiku na kuzua taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa mji huo.

Sakanyi amesema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na kwamba majengo yaliyoathirika zaidi ni yale ambayo yamekua yakitumiwa kuhifadhi vifaa vya uchaguzi.

Habari zaidi kutoka katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinasema kuwa takribani mashine Elfu Saba zilizotarajiwa kutumika wakati wa zoezi la upigaji kura zimeharibiwa na moto huo.

Tukio hilo la kwa kuteketea kwa moto kwa  majengo yanayotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi  katika  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limetokea zikiwa zimesalia siku Kumi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika Jamhuri hiyo, uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi  ya DRC kupitia kwa Msemaji wake  Jean Pierre Kalamba imeelezea matumaini yake kuwa tukio hilo halitavuruga mchakato wa uchaguzi.