Mourinho atimuliwa Man U

0

Klabu ya Manchester United ya nchini England imetangaza kumfuta kazi meneja wake Jose Mourinho.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imemshukuru Mourinho kwa kazi aliyoifanya muda wote aliokua akifanya kazi na klabu hiyo na imemtakia kila la kheri kwa siku zijazo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa meneja wa muda atakayeiongoza klabu hiyo hadi mwishoni wa msimu, atatangazwa wakati wowote kuanzia sasa wakati uongozi wa klabu  hiyo ya Manchester United ukitafuta meneja wa kudumu.

Mourinho, Raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 55 amefukuzwa kazi baada ya kuingoza klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili na nusu, huku akiipatia timu hiyo taji la Europa na kombe la ligi.

Manchester United imekubali kipigo cha mabao matatu kwa moja kutoka kwa Liverpool mwishoni mwa juma, kipigo kinachoiweka timu hiyo nyuma kwa alama 19 dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu ya England.

Mourinho anaondoka klabuni hapo wakati ambapo droo ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ikiwa imetangazwa na Manchester United imepangwa kucheza na PSG ya Ufaransa.

 

REA na TANESCO watakiwa kufanya kazi kwa umakini

0

Naibu Waziri wa Nishati, – Subira  Mgalu  ameuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwa makini katika kupanga vijiji vinavyopaswa kupatiwa huduma ya umeme kwenye wilaya zenye majimbo mawili ya uchaguzi ili kuepusha malalamiko ya kupendelea upande mmoja.

Naibu Waziri Mgalu ametoa agizo hilo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma alipokuwa akikagua miradi ya usambazaji umeme vijijini katika wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini.

Amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kupata malalamiko kutoa kwa baadhi ya wakazi wa wilaya ya Tunduru waliodai kuwa vijiji vingi vya  jimbo la Tunduru Kaskazini ndivyo vimepatiwa huduma ya umeme huku  jimbo la Tunduru Kusini likiwa na vijiji vichache vilivyopatiwa huduma hiyo.

Naibu Waziri huyo wa Nishati, – Subira  Mgalu  ameelekeza kuwa kazi ya upangaji wa vijiji vilivyo katika mpango wa kupatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali ishirikishe viongozi wa ngazi tofauti ili kuondoa malalamiko.

Kuhusu kazi ya uunganishaji wilaya ya Tunduru  kwenye umeme wa Gridi ya Taifa,  amesema kuwa wilaya hiyo itaanza kupata  umeme huo kuanzia mwezi Machi mwaka 2019 baada ya kuvuta umeme kutoka wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akiwa wilayani Tunduru, Naibu Waziri Mgalu amewasha umeme katika vijiji vya Namiungo, Mchuluka, Kangomba na Daraja Mbili ambapo kaya zaidi ya mia moja zimeunganishwa na huduma hiyo vikiwemo vituo vya afya na shule.

Wakazi wa vijiji mbalimbali vilivyopatiwa huduma ya umeme wilayani Tunduru wameishukuru serikali kwa kuwafikishia  huduma hiyo ambayo imewawezesha kufanya shughuli za kiuchumi pamoja na kupata huduma za matibabu hata nyakati za usiku tofauti na ilivyokuwa awali.

Halmashauri Kuu ya CCM yakutana

0

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais John Magufuli amefungua kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Rais Magufuli amewataka wanachama wa CCM na Watanzania wote kujivunia kwa kuwa nchi inasonga mbele kimaendeleo.

Rais Magufuli ameongeza kuwa serikali imejidhatiti kulipa madeni yaliyokuwa yanadaiwa na wafanyakazi wakiwemo walimu.

Kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM kimehudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa Halmashauri Kuu ya CCM.

 

NEC yatangaza uchaguzi katika kata nne

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo  katika kata mbili utakaofanyika Januari 19  mwaka 2019, uchaguzi utakaofanyika pamoja na ule wa jimbo la Temeke mkoani Dar es salaam  na kata 46 za Tanzania Bara uliotangazwa hapo awali.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk amezitaja kata hizo kuwa ni Mwanahina iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga  na Kata ya Biturana katika halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Amesema kuwa fomu za uteuzi wa wagombea hao zitatolewa kati ya Disemba 21 na 27 mwaka huu na uteuzi wa wagombea utafanyika Disemba 27 mwaka huu,  huku kampeni za uchaguzi huo mdogo wa udiwani zikipangwa kuanza  Disemba 28 mwaka huu hadi Januari 18 mwaka 2019.

Jaji Mbarouk ametoa wito kwa  vyama vya siasa nchini  kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo wa udiwani.

Serengeti Boys yawasili nchini

0

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imerejea nchini ikitokea nchini Botswana baada ya kutwaa ubingwa wa soka kwa ukanda wa Tano wa Afrika.

Timu hiyo iliifunga Angola penati sita kwa tano katika  mchezo wa fainali.

Serengeti Boys wamelakiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Dkt Harrison Mwakyembe  ambaye amewapongeza wachezaji hao kwa ushindi walioupata.

Timu ya Serengeti Boys kwa sasa inaanza kujiandaa  na michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika mwaka 2019 nchini.

Wajasiriamali wadogo Tanga wapatiwa vitambulisho

0

Mkuu wa mkoa wa Tanga, -Martine Shigela amewaagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kuwasimamia wafanyabiashara wadogo katika maeneo yao ili wasibughudhiwe na suala la ulipaji kodi usiozingatia utaratibu.

Shigela ametoa kauli hiyo wakati wa ugawaji wa vitambulisho maalum vya wajasiriamali wadogo, vitambulisho vilivyotolewa na Rais John Magufuli Disemba 10 mwaka huu.

Lengo la vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ni kuwatambua wajasiriamali wadogo katika maeneo yote nchini.

Wajasiriamali wanaopatiwa vitambulisho hivyo, ni wale wenye biashara zenye mtaji usiozidi Shilingi Milioni Nne.

Sekretarieti ya Ajira yaendelea kupokea maombi

0

Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imepokea jumla ya maombi 594,300 kutoka kwa waombaji wa nafasi za kazi katika Utumishi wa Umma zilizotangazwa kwenye Wizara, Idara, Wakala, Sekretarieti za mikoa, manispaa, halmashauri na Taasisi za umma kuanzia mwezi Novemba  mwaka 2015 hadi hivi sasa.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka mitatu ya Sekretarieti hiyo kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka huu jijini Dar es salaam, Katibu wa Sektretarieti ya Ajira, – Xavier Daudi amesema kuwa tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya Tano, serikali imetangaza nafasi zilizo wazi 6,554 ambapo jumla ya waombaji Laki Moja na Elfu Arobaini waliitiwa katika usaili.

Xavier ameongeza kuwa hadi kufikia Disemba 15 mwaka huu,  jumla ya nafasi za wazi za kazi 6,099 zilikwishajazwa, huku nafasi 455 zilizotangazwa kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu mchakato wake ukiendelea na utakamilika hivi karibuni.

Ameongeza kuwa mbali na mchakato huo, pia wapo watumishi walioajiriwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kada za Afya na Ualimu, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya watumishi wa kada za afya 24,728 wameajiriwa wakati kwa upande wa kada ya ualimu jumla ya walimu 40,086 waliajiriwa serikalini.

“Idadi hii inaweza kuongezeka katika mwaka huu wa fedha wa  2018/2019 kwa watumishi watakaoajiriwa katika kada za walimu, afya pamoja na watumishi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama ambao utaratibu wake wa ajira unataratibiwa na mamlaka husika” amesema Katibu huyo wa Sektretarieti ya Ajira nchini.

Akizungumzia udhibiti wa waombaji wasio na sifa ikiwemo wenye vyeti vya kughushi, Xavier amesema kuwa Serikali  hiyo ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeendelea kukagua  nyaraka za waombaji mbalimbali vikiwemo vyeti vyao ili kuhakikisha kuwa wanaoajiriwa ni wale wenye sifa na vyeti vinavyostahili kwa mujibu wa sheria.

Akifafanua zaidi,  Xavier amesema kuwa kati ya mwaka 2015 na 2018,  jumla ya nyaraka za vyeti vya waombaji kazi 18,817 viliwasilishwa kwenye mamlaka zinazohusika na utoaji wa vyeti hivyo kwa ajili ya uhakiki, ambapo vyeti halali vilikuwa 18,112 na vyeti 706 vilibainika kuwa ni vyeti vya kughushi.

 

Al Bashir aitembelea Syria

0

Rais Omar Al Bashir wa Sudan amekuwa kiongozi wa kwanza kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu kuitembelea Syria, tangu nchi hiyo iingie kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe takribani miaka nane iliyopita.

Katika uwanja wa ndege wa Damascus , -Al-Bashir amepokelewa na mwenyeji wake Rais Bashar Al Assad wa Syria kabla ya viongozi hao kuelekea Ikulu ambapo wamefanya mazungumzo juu ya uhusiano wa nchi hizo mbili na maendeleo ya Syria pamoja na ya Mashariki ya Kati.

Syria ilifukuzwa uanachama wa mataifa 22 ya Umoja wa nchi za Kiarabu baada ya kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011.

Nchi za Kiarabu zimeiwekea Syria vikwazo na mara kwa mara zimekuwa zikimlaumu Rais Al Assad kwa kutumia nguvu kubwa ya kijeshi na pia kushindwa kwake kujadiliana na wapinzani.

Lengo la ziara ya Rais huyo wa Sudan, -Omar Al Bashir nchini Syria halijawekwa wazi, lakini kutokana na kuwa vita inaendelea kupungua nchini humo na vikosi vya serikali vikiendelea kuikomboa miji kadhaa muhimu, baadhi ya viongozi wa mataifa ya Kiarabu wameonyesha nia ya kutaka kurejesha uhusiano na serikali ya Syria.