Manchester City yatinga nusu fainal EFL

0

Timu ya Manchester City imetinga nusu fainali ya michuano ya EFL baada ya kuifunga Leicester City kwa changamoto ya mikwaju ya penati tatu kwa moja baada ya kutoshana nguvu kwa kufungana bao moja kwa moja ndani ya dakika 90.

Manchester City ndio walikuwa wa kwanza kupata bao ambapo kiungo wake aliyerudi kutoka kuuguza majeraha, – Kevi DE Bruyne aliiandikia bao timu yake kwenye dakika ya 14 huku Leicester City wakisawazisha katika dakika ya 73 kupitia kwa  Marc Albrighton.

Timu hizo zilipotinga kwenye mikwaju ya penati, -Leicester City waliokuwa nyumbani wakakosa mikwaju mitatu kati ya minne huku Manchester City wakikosa mmoja kati ya minne waliyopiga, ukikoswa na nyota wake Raheem Sterling.

Katika mchezo mwingine wa robo fainali uliopigwa Jumanne Disemba 18, Burton FC wamewaondosha Middlesbrough kwa kuwanyuka bao moja kwa nunge huku michezo mingine miwili ya robo fainali ikichezwa hii leo Disemba 19 ambapo Arsenal wanawaalika Tottenham Hotspur  na Chelsea wakiwa wenyeji wa AFC Bournemouth.

 

Man U yapata kocha wa muda

0

Klabu ya Manchester United ya nchini England  imemtangaza mchezaji wake wa zamani, –  Ole Gunnar Solskjaer kama kocha wake wa muda mpaka mwisho wa msimu huu,  kuchukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mreno Jose Mourinho aliyefukuzwa kazi.

Kocha huyo aliyeichezea Manchester United michezo 235 na kuifungia mabao 91, anachukua majukumu ya kukiongoza kikosi hicho kikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu ya England.

Akiongelea kupewa majukumu hayo, -Solskjaer amesema kuwa  amefurahishwa sana na kurudi tena klabuni hapo kwa sababu klabu hiyo bado ipo moyoni mwake huku Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa klabu hiyo, -Ed Woodward akisema kuwa Solskjaer ana vinasaba na Man United ndio maana wamempa jukumu hilo.

Kutangazwa kwa Solskjaer mwenye miaka 45 raia wa Norway kurithi mikoba ya Mourinho,  kunahitimisha uvumi ulioenea kufuatia tangazo lililotolewa kimakosa na Manchester United likimtambulisha kocha huyo anayekinoa kikosi cha Molde cha nchini Norway hivi sasa.

Tangazo hilo lililowekwa kwenye tovuti ya klabu hiyo likisindikizwa na bao la nyota huyo alilofunga kwenye fainali ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya mwaka 1999 akiichezea Manchester United, lilifutwa muda mchache baadaye,  hali iliyoibua mijadala.

Tangazo hilo lilisababisha Waziri Mkuu wa Norway, -Erna Solberg kutumia ukurasa wake wa  mtandao wa kijamii wa Twitter kumtakia kila la kheri kocha huyo katika safari ya kukinoa kikosi hicho huku akisema kuwa ni siku kubwa sana kwa soka la Norway kwa Solkjaer kupata nafasi ya kuwa kocha mkuu wa muda wa Manchester United.

Hata hivyo, muda mchache baada ya Manchester United kufuta taarifa ya kumtambulisha Solkjaer, Waziri Mkuu wa Norway naye akauondoa ujumbe wake wa kumtakia kila la kheri Sosha.

Ole Gunnar Solkjaer aliichezea Manchester United kuanzia mwaka 1996 mpaka mwaka 2007 huku akipata nafasi ya kufundisha timu ya akiba ya Manchester United kwa miaka mitatu tangu alipostaafu kucheza soka mwaka 2007 hadi mwaka 2010.

Solkjaer atasaidiwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo enzi za Sir Alex Ferguson huku Michael Carrick na Kieran McKenna waliokuwa wasaidizi wa Mourinho nao wakiendelea kuwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer.

 

Uturuki yatoa picha za watuhumiwa wa mauaji

0

Serikali ya Uturuki imetoa picha za watu wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, -Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia uliopo mjini Istanbul.

Picha hizo zinawaonyesha watuhumiwa hao wakiingia kwenye ubalozi huo wa Saudi Arabia na nyingine wakipanda ndege na kutua katika uwanja wa ndege mjini Istanbul.

Serikali ya Saudi Arabia imekataa kuwakabidhi watuhumiwa wa mauaji ya Khashoggi nchini Uturuki ili washitakiwe.

Mwana wa mfalme wa Saudi Arabia, – Mohammed Bin Salman anatuhumiwa kuamuru mauaji ya Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekua mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudia.

 

Simba kumenyana na KMC

0

Mabingwa watetezi wa  Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, -Simba wanashuka dimbani  jioni ya leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuumana na timu ya KMC ya Kinondoni katika mchezo wa kiporo kwenye mfululizo wa ligi hiyo.

Simba yenye alama 27 baada ya kushuka dimbani mara 12,  ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo ambapo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya KMC iliyo katika nafasi ya tisa ikiwa imejikusanyia alama 21.

Mabingwa hao watetezi wako nyuma kwa alama 17 dhidi ya vinara wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, -Yanga wenye alama 44 baada ya kucheza michezo 16 huku wakifuatiwa na Azam walio kwenye nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 40 katika michezo 16.

Ligi hiyo itaendelea Alhamisi Disemba 20 mwaka huu, kwa mchezo mmoja kupigwa huko mkoani Arusha ambapo African Lyon waliohamishia michezo yao ya nyumbani kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid wanawaalika vinara wa ligi hiyo, timu ya Yanga.

 

Raia wa Madagascar wapiga kura

0

Raia wa Madagascar wanapiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi, kuchagua viongozi mbalimbali akiwemo Rais atakayeliongoza taifa hilo kwa kipindi kingine.

Waliowahi kuwa marais wa nchi hiyo Andry Rajoelina na Marc Ravalomanana ni miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais nchini Madagascar.

Hii ni mara ya pili kwa wanasiasa hao wawili kuchuana katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa rais nchini humo.

Mara ya kwanza walichuana mwaka 2009, ambapo Ravalomanana alishindwa katika kinyang’anyiro cha urais na kulazimika kuachia madaraka.

 

Watanzania watakiwa kutovamia hifadhi ya barabara

0
Rais John  Magufuli ameweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro iliyopo  jijini Dar es salaam katika eneo la  kuanzia Kimara mkoani Dar es salaam hadi Kibaha mkoani Pwani yenye urefu wa Kilometa 19.2.
Upanuzi huo utahusisha kuongeza njia za kupita magari kutoka mbili zilizopo sasa hadi nane, kujenga madaraja sita na makalavati 36 na kujenga barabara ya juu katika eneo la Kibamba CCM kwenye makutano ya barabara inayotokea Bunju na barabara ya kwenda hospitali ya Mloganzila.
Sherehe hizo za kuweka jiwe la msingi la upanuzi huo zimefanyika katika eneo la Kimara Stop Over na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, Mawaziri, Wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam wakiongozwa na Mkuu wa mkoa huo Paul Makonda.
Akizungumza wakati wa sherehe  hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa barabara ya Morogoro ni lango kuu la usafiri kati ya jiji la Dar es salaam lenye bandari kuu na mikoa mingi ya Tanzania Bara na nchi jirani na kwamba upanuzi wake utasaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari takribani elfu  50 yanayopita katika barabara hiyo kila siku.
Mhandisi Mfugale ameongeza kuwa, upanuzi wa barabara hiyo pia utaokoa muda kutoka saa tatu zinazotumika kupita eneo hilo kwa sasa hadi nusu saa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mfugale, upanuzi wa barabara hiyo ya Morogoro kuanzia eneo la Kimara hadi Kibaha,  utafanyika kwa muda wa miezi 30 kuanzia Julai 21 mwaka huu wa 2018 kwa gharama ya shilingi Bilioni 141.56, fedha zinazotolewa na serikali.
Akizungumza katika sherehe hizo,  Rais Magufuli amewapongeza wakazi wa mkoa wa Dar es salaam kwa kupatiwa mradi huo mkubwa na kubainisha kuwa pamoja na barabara hiyo, serikali  inaendelea kuboresha miundombinu ya Dar es salaam ambapo barabara zenye jumla ya kilometa 212 zinajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 660.
Kuhusu fidia kwa nyumba zilizovunjwa wakati wa upanuzi wa barabara hiyo, Rais Magufuli amewataka wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kuwa watalipwa fidia.
Amesisitiza kuwa serikali haitalipa fidia kwa mtu yeyote aliyejenga katika eneo la hifadhi ya barabara kwa mujibu wa sheria.
“Kuna wanasiasa wanataka waonekane wao ndio wanawatetea wananchi na wanasema serikali itoe fidia, nataka niwaambie ndugu ukivamia barabara unatafuta umasikini, fidia haipo, fidia haipo, narudia fidia haipo” amesisitiza Rais Magufuli.
 Amewataka  Watanzania kote nchini kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kujenga makazi.
Naye Spika wa Bunge Job Ndugai amempongeza Rais Magufuli kwa namna serikali inavyosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na kumhakikishia kuwa Bunge litaendelea kuunga mkono juhudi hizo zenye maslahi kwa Taifa.

BASATA yawafungia Diamond na Rayvan

0

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA ) limewafungia kwa muda usiojulikana wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Nassib Abdul maarufu kama Diamond na Raymond Mwakyusa maarufu kama Rayvan kufanya onesho lolote ndani na nje ya nchi.

Taarifa iliyotolewa na BASATA imesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na wasanii hao kukiuka maagizo ya Baraza hilo kwa kuimba wimbo wa Mwanza uliofungiwa kutokana na kukiuka maadili.

BASATA pia imesitisha kibali cha tamasha la Wasafi Festival kwa mwaka 2018, tamasha lililokua likifanywa na wasanii hao kutokana ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wake.

Novemba 12 mwaka huu, BASATA ilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia wimbo unaojulikana kwa jina la Mwanza ulioimbwa na Diamond pamoja na Rayvan na kupiga marufuku kutumbuizwa sehemu yoyote.

Hata hivyo wasanii hao wameshindwa kutii agizo hilo na kuendelea kuuimba wimbo huo katika matamasha yao mbalimbali.

 

 

Majaji wafukuzwa kazi kwa tuhuma za rushwa

0

Rais Nana Akufo-Addo  wa Ghana amewafukuza kazi Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo, ikiwa ni miaka mitatu baada ya tume iliyoundwa kuchunguza vitendo vya rushwa kutoa ripoti yake na kuwatuhumu kuwa walihusika na vitendo hivyo.

Mbali na kuwafukuza kazi majaji hao, Rais Akufo-Addo pia amekabidhi majina ya majaji hao kwa jeshi la polisi la Ghana ili liendelee na upelelezi zaidi na baadae kuwafungulia mashitaka.

Hata hivyo  haijafahamika ni kwa nini Rais  Akufo-Addo ameamua kuchukua uamuzi hivi sasa, baada ya kupita miaka mitatu tangu kutolewa kwa ripoti hiyo.

Majaji hao watatu wa Mahakama Kuu ya Ghana ni miongoni mwa zaidi ya watumishi mia moja wa idara ya mahakama ya nchi hiyo walioorodheshwa katika ripoti ya watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ripoti iliyoitikisa nchi hiyo mwaka 2015.

Tayari majaji hao wamefungua shauri katika mahakama ya Jumuiya ya uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ili kupinga hatua hiyo ya kufukuzwa kazi na pia wameelezea kusikitishwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Rais  Nana Akufo-Addo.

Mwandishi wa habari za uchunguzi wa Ghana, – Anas Aremeyaw Anas ndiye aliyefichua taarifa za watumishi wa idara mbalimbali nchini humo ikiwemo ile ya mahakama kuhusika na vitendo vya rushwa ambapo aliwarekodi watumishi hao wakichukua rushwa hizo kwa njia mbalimbali.