Polisi DRC wapambana na waandamanaji

0

Polisi wa kutuliza ghasia mjini Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wamepambana na waandamanaji waliokuwa wakipinga tangazo la serikali la kuzuia kampeni za uchaguzi mjini humo.

Wafuasi wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu wamepambana na polisi baada ya kukiuka amri ya serikali ya kuzuia mikusanyiko ya kisiasa mjini Kinshasa, kwa madai kuwa inaweza kuleta ghasia, huku waandamanaji hao wakisema kuwa wananyimwa haki yao ya msingi.

Fayulu ameelezea kusikitishwa na amri hiyo ya serikali na kusema kuwa atakutana na uongozi wa Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri hiyo ili kuhoji ni kwa nini imetolewa mara baada ya yeye kutangaza nia yake ya kuanza kampeni.

Uchaguzi mkuu wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo na Fayulu amewalalamikia askari wa Jamhuri hiyo kwa kuwarushia risasi za moto wafuasi wake katika miji ya Kalembu na Lubumbashi ambako nako amezuiwa kufanya kampeni.

Serikali ya DRC ilitangaza kuwa huenda zoezi la kupiga kura nchini humo likachelewa kuanza siku hiyo ya Jumapili kutokana na sababu za kiufundi.

Karibu vifaa vyote vya kupigia kura viliteketezwa kwa moto katika ghala la kuhifadhia vifaa hivyo mjini Kinshasa wiki iliyopita, lakini serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ikatangaza kuwa uchaguzi huo  utafanyika kama ulivyopangwa.

 

Sudan yatangaza hali ya tahadhari

0

Serikali ya Sudan imetangaza hali ya tahadhari katika mji wa Atbara ulioko katika bonde la mto Nile, baada ya mfululizo wa maandamano ya wananchi waliokuwa wakipinga hali ya upungufu wa chakula kwenye mji wao.

Waandamanaji hao walichoma moto makao makuu ya chama tawala nchini humo, huku maandamano ya kupinga serikali ya Sudan yakiendelea kushika kasi.

Habari zaidi kutoka nchini Sudan zinasema kuwa, asilimia 60 ya raia wa nchi hiyo maisha yao yanaendelea kuwa magumu na wameendelea kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na ukosefu wa mafuta kwa ajili ya kuendeshea magari yao.

Golden Warriors yala mweleka

0

Bingwa  mtetezi wa Ligi ya Kulipwa ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani (NBA), – Golden State Warriors wameshindwa kutamba mbele ya Utah Jazz baada ya kula mweleka wa alama 108 kwa 103.

Licha Stephen Curry kufunga alama 32 na Kevin Durant kuongeza nyingine 30,  bado hazikutosha kuwapa Warriors ushindi mbele ya Jazz waliokuwa wakiongozwa na Joe Ingles aliyefunga alama 20.

Nayo timu ya  Cleveland  Cavaliers imeendeleza msimu mbovu baada ya kukubali kipigo cha alama 110 kwa 99 kutoka kwa Charlote Hornets katika mchezo ambao mchezaji Kemba Walker ameifungia Hornets alama 30 na kutoa pasi za kufunga sita.

Na katika michezo mingine timu ya San antonio Spurs wameinyuka Orlando Magic alama 129 kwa 90, wakati Brooklyn Nets wakiilaza Chicago Bulls alama 96 kwa 93 huku Indiana Pecers wakishindwa kufurukuta mbele ya Toronto Raptors na kula mweleka wa alama 99 kwa 96.

Nayo New Orlean Pelican imepoteza mbele ya Milwaukee Bucks kwa kunyukwa alama 108 kwa 103.

 

 

Real Madrid yatinga fainali klabu bingwa ya dunia

0

Timu ya Real Madrid imetinga fainali ya michuano ya klabu bingwa ya dunia baada ya kuinyuka Al Ain ya Umoja wa Falme za Kiarabu mabao matatu kwa moja.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Wales, -Gareth  Bale amefunga mabao yote matatu yaani Hat Trick na kuipeleka Madrid katika fainali ya tatu mfululizo ya michuano hiyo ya ngazi ya juu kabisa kwa vilabu duniani huku bao la kufutia machozi kwa Al Ain likifungwa na Shoma Doi.

Mabao matatu aliyofunga Bale yanamfanya kufikisha idadi ya mabao sita katika mechi tano za michuano ya klabu bingwa ya dunia na kuwa mchezaji wa tatu kufunga hat trick katika michuano hiyo nyuma ya Luis Suarez na Cristiano Ronaldo.

Madrid ambao wanawania kunyakua taji la tatu mfululizo la michuano hiyo,  sasa watamenyana na Al Ain ambao wamepata nafasi ya kucheza michuano hiyo kwa nafasi ya upendeleo inayotolewa kwa nchi mwenyeji wa michuano hiyo kwenye dimba la Zayed  Sports City Jumamosi Disemba 22 mwaka huu.

Changamoto za mawasiliano Pemba kushughulikiwa

0

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameahidi kuzifanyia kazi changamoto za kutokuwepo kwa mawasiliano ya simu za mkononi katika baadhi ya maeneo Kisiwani Pemba.

Mhandisi Nditiye ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi kwa wakazi wanaoishi kwenye mkoa wa Kaskazini uliopo kisiwani Pemba.

Wakati wa ziara hiyo Mhandisi Nditiye amebaini kuwa yapo baadhi ya maeneo katika mkoa huo yana usikivu mdogo wa mawasiliano na mengine hayana kabisa.

Katika hatua nyingine Mhandisi Nditiye amekagua vituo viwili kati ya kumi vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano vilivyojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote -UCSAF katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Watanzania wasisitizwa kujituma kufanyakazi

0

Rais John Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kujiletea maendeleo na kuacha kusubiri serikali ili iwapelekee maendeleo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja  jipya la Selander litakalounganisha eneo la hospitali ya Aga Khan na Coco Beach kupitia baharini.

Amesema kuwa daraja hilo linajengwa kwa fedha za serikali pamoja na mkopo nafuu kutoka Korea Kusini, nchi ambayo raia wake wamekua wakifanya kazi kwa bidii kubwa na kujituma.

Rais Magufuli pia ametumia hafla hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi kwa kwa kuwa bila nchi kuwa na amani miradi yote ya maendeleo haitaweza kutekelezwa.

 

Amemtaka mkandarasi anayejenga daraja hilo ambaye ni kampuni ya  GSE kutoka Korea Kusini kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi 30 iliyopangwa ama ikiwezekana hata kufupisha muda wa kufanya kazi hiyo.

Ameelezea matumaini yake kuwa kampuni hiyo itafanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kutoka na Korea ya Kusini kuwa na Wakandarasi waliobobea kwenye ujenzi wa miundomninu hasa madaraja na barabara.

Kwa upande wake Balozi wa Korea Kusini nchini, –  Cho Tae-Ick amesema kuwa licha ya kuwa ujenzi huo utarahisisha usafiri jijini Dar es salaam pia utaimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi hiyo.

 

Daraja hilo jipya la Selander ambalo ni kubwa kwa urefu nchini, litakapokamilika litakua na uwezo wa kupitisha zaidi ya magari elfu 50 kwa siku na hivyo kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam.

Tiketi za mabasi ya abiria kuwa za kielektroniki

0

Serikali imesema kuwa hadi kufikia  mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2019 itahakikisha tiketi za mabasi yote ya abiria zinakuwa za mfumo wa kielektroniki, lengo likiwa ni kuongeza mapato ya  nchi kupitia usafari wa mabasi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe wakati wa uwekeji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja  jipya la Selander lenye urefu wa kilometa 1.03 litakalopita baharini kuanzia hospitali ya Aga Khan mpaka Coco Beach jijini Dar es salaam.

“Mapato mengi yamekuwa yakipotea kutokana na tiketi za mabasi hayo kuwa za kawaida,  hivyo baada ya kuanza kutumika kwa tiketi  hizo mpya, mapato  yataongezeka”, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kamwelwe,  kwa sasa mabasi elfu 49 ya kusafirisha abiria yanatoa huduma hiyo,   na kutokana na idadi yake yataweza kuingizia kiasi kikubwa cha mapato serikali.

 

Ujenzi daraja jipya la Selander kuzinduliwa

0

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini – TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa daraja jipya la Selander wilayani Kinondoni jijini Dar Es Salaam hautaathiri nyumba wala majengo yaliyo katika eneo hilo.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa daraja hilo jipya Mfugale amewatoa hofu mabalozi na wakazi wengine wa eneo hilo kwa kuwa mradi huo hautakuwa na madhara kwa mali zao.

Rais Dkt. John Magufuli anatarajiwa kuzindua mradi huu.