Rais Magufuli awataka polisi kuhudumia wananchi

0

Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt. John Magufuli amewataka polisi kutojihusisha na vitendo viovu kama rushwa na uonevu.

Katika hafla ya kuwatunuku vyeti askari waliofanya vizuri katika mafunzo ya uafisa na ukaguzi wa jeshi la polisi Rais Magufuli amewataka kutumia elimu vizuri kwa jamii ya watanzania katika kuboresha utendaji kazi, kuhudumia wananchi vizuri na kufuata taratibu za kazi.

“Mkaonyeshe utofauti  katika utendaji kazi zenu, mkafanye kazi kwa weledi”alisema Rais Magufuli.

Amesema atasikitika kuona askari hao waliomaliza kuwa wa kwanza katika kuwabambikia kesi wananchi zisizowahusu na kuwataka kuwa askari wema katika jamii.

Pia amesema ataendelea kushughulikia matatizo ya askari wote nchini ili kuhakikisha  wanafanya kazi kwa weledi.

Jeshi la Polisi haliyumbishwi – Masauni

0

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Yusuph Masauni amesema Jeshi la Polisi halitayumbishwa katika kuhakikisha wanalinda usalama na kutoa onyo kwa wote wenye kupanga njama za kuvuruga nchi kuacha mara moja.

Akizungumza kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti askari waliofanya vizuri katika mafunzo ya uafisa na ukaguzi wa jeshi la polisi Masauni amesema serikali imejipanga kuhakikisha usalama wa nchi uko vizuri kwa gharama yeyote.

Naibu Waziri Masauni amewasisitiza wahitimu kuendeleza uzalendo na nidhamu kama mafunzo aliyoyapata na kwamba atashangaa endapo watakiuka yote waliyofunzwa.

Amewataka askari hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kufuata taratibu zinazotakiwa.

Uhalifu wapungua nchini – Polisi

0

Jeshi la Polisi nchini limesema uhalifu nchini umepungua kwa kiasi kikubwa jambo ambalo limefanya hali ya usalama kuwa ya kiwango cha juu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Simon Sirro jijini Dar Es Salaam kwenye hafla ya kuwatunuku wahitimu waliofanya vizuri katika mafunzo ya uofisa na ukaguzi wa jeshi la polisi.

Amesema hali ya mwaka huu imekuwa tofauti katika usalama.

“Kiwango cha uhalifu kimepungua kwa kiasi kikubwa na hii imetokana na ushrikiano mkubwa wa wananchi, polisi na vyombo vya usalama hapa nchini jambo linaloashiria alama nzuri ya ushirikiano hapa nchini”alisema IGP Sirro.

Kamanda Sirro amesema uhalifu katika makosa ya unyang’anyi umepungua kwa asilimia 25, uhalifu wa makosa ya usalama barabarani ukiwa umepungua kwa asilimia 32.

Katika hatua nyingine Kamanda Sirro amesema kwa mwaka huu jeshi la polisi kupitia makosa ya barabarani limeingiza mapato ya shilingi Bilioni 63.8 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo mapato yalikuwa  shilingi Bilioni 62.2.

Tisa wakamatwa kwa kuwaoza wanafunzi

0

Jeshi la Polisi wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu limewakamata watu tisa wanaotuhumiwa kuhusika kuwaoza wanafunzi wa shule ya msingi Giyuki kata ya Nkololo.

Jeshi la Polisi limetekeleza agizo la Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka aliyemwagiza mkuu wa wilaya ya Bariadi kuwakamata wazazi na wanafunzi waliooana baada ya kumaliza darasa la saba.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga ametangaza msako kwa kata zote.

Wakala wa maji vijijini kuanzishwa

0

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo amesema serikali imedhamiria kuanzisha wakala wa maji vijijini kwa lengo la kuharakisha utekelezwaji wa miradi ya maji vijijini.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma Profesa Mkumbo amesema utaratibu wa kuanza kwa wakala huo umefikia hatua ya kupata maoni ambayo yatawezesha azma ya serikali kuanzisha wakala huo kutimia ili kukabiliana na changamoto ya maji vijijini.

Aidha Katibu Mkuu huyo wa wizara ya maji ametoa pongezi kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira kwa kuwa mamlaka bora ya utoaji huduma ya maji katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Hata hivyo Prof. Mkumbo amesema Wizara ya Maji inaendelea kusimamia miradi ya nchi nzima ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji katika maeneo yao.

Mtolea apita ubunge Temeke

0

Msimamizi wa uchaguzi wa ubunge jimbo la Temeke, Lusubilo Mwakabibi amemtangaza Abdallah Mtolea kuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya kupita bila kupingwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Lusubilo amemtangaza Mtolea kushinda kiti hicho cha ubunge baada ya wagombea wa  vyama vingine vya siasa kushindwa kutimiza vigezo  ambavyo vimewekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi -NEC.

Muda wa kurejesha fomu za uchaguzi huo ulikuwa leo Alhamis Desemba 12 saa kumi jioni.

Wananchi wahamasishwa kupokea ndege Jumapili

0

Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda amewaomba wakazi wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere katika mapokezi ya ndege mbili za Shirika la Ndege Nchini –ATCL.

Akizungumza na waandishi wa habari Makonda amesema ndege hizo zitapokelewa na Rais Dkt. John Magufuli siku ya Jumapili ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za serikali.

Tukio la kuwasili na kupokelewa kwa ndege hizo litatangazwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC kupitia vyombo vyake vya Radio na Televisheni.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete watakiwa kujiendeleza kielimu

0

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete -JKCI wametakiwa kujiendeleza kielimu ili waweze kutoa huduma bora zaidi na za kisasa  kwa wagonjwa.

Rai hiyo imetolewa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi wakati akizungumza katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.

Profesa Janabi amesema utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa na wananchi unaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia hivyo basi ni jukumu la wafanyakazi hao kuhakikisha wanajiendeleza kielimu   kwa njia ya mtandao, elimu ya masafa marefu au kwenda darasani.

Pia amewahimiza wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii, kuwahi kazini na kutumia muda wao wa kazi  kutoa huduma kwa wananchi na si vinginevyo huku wakifuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na maadili ya kazi zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi Robert Mallya amesema kurugenzi yake itaendelea kutoa mafunzo kwa maafisa uuguzi ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo ili wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo waendelee kupewa huduma bora zaidi ya kiwango cha kimataifa.