Basata yakanusha kuwafungulia wasanii Diamond na Rayvan

0

Baraza la Sanaa la Taifa(Basata) limekanusha kuwafungulia wasanii wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platnamz na Raymond Mwakyusa maarufu kama Rayvan kufanya maonesho ndani na nje ya nchi .

Taarifa iliyosambazwa leo Decemba 22 iliyoandikwa na kaimu katibu wa Basata Onesmo Kayanda imesema kuwa baraza halijatoa ruhusa kwa msanii huyo na uamuzi wa awali unabakia kama ulivyo.

“Baraza liasisitza kwamba halijawafungulia wasanii hao kufanya onesho lolote ndani nan je ya nchi kama taarifa zinavyosambazwa”alisema Kayanda katika taarifa ya Basata.
Tarehe 18/12/2018 Basata iliwafungia wasanii hao kujishughulisha na sanaa ndani na nje ya nchi kwa kipindi kisichojulikana kutokana na kutumia kwa makusudi wimbo wao wa Mwanza ambao uemfungiwa na Baraza la Sanaa kwa sababu za kimaadili.

Aidha Basata imesisitiza kuwa linawataka wasanii hao kutii maagizo waliyopewa na kuacha mara moja kupotosha umma kwa kusambaza taarifa za uongo kabla ya hatua kali Zaidi kuchukuliwa Zaidi yao.

Usafiri wa reli baina ya Manyoni na Kanda ya Ziwa wakatika

0

Shughuli za usafirishaji kati ya Stesheni ya Manyoni, Itigi na mikoa ya Kanda ya ziwa zimesimama kwa muda baada ya eneo la ardhi kutitia na kutengeneza shimo kando ya reli nje kidogo ya mji wa Itigi mkoani Singida.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kitopeni wamesema walisikia kishindo kikubwa wakati mvua ikinyesha kilichosababisha nyufa na mashimo katika baadhi ya maeneo ambapo pia nyumba tatu zimebomoka.

 Hali hiyo imeathiri shughuli za usafirishaji reli ya kati baina ya stesheni ya Itigi na Manyoni na hivyo kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya Singida na mikoa ya Kanda ya ziwa inayotumia usafiri huo wa reli.

Tayari mafundi wa kampuni ya Reli Tanzania wamefika katika eneo hilo kuanza ukarabati wa eneo la reli lililoharibika ili kurejesha huduma za usafiri.

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Singida wametembelea maeneo yaliyoathirika na mvua hiyo ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Rehema Nchimbi amesihi wananchi kuwa watulivu  wakati serikali inatafuta mtaalamu wa miamba kufanya uchunguzi wa kina katika maeneo hayo yaliyotitia.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani aachia ngazi

0

Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis leo ametangaza kujiuzulu wadhifa wake.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Mattis amesema anaamini kwamba Marekani inahitaji kuendeleza ushirikiano imara na washirika wake, na inapaswa kuweka msimamo usio na utata dhidi ya mataifa ya China na Russia.

Mattis ambaye ni mwanajeshi aliyestaafu akiwa na cheo cha Jenerali, amekuwa akichukuliwa kama mhimili wa utulivu katika baraza la mawaziri la Rais Donald Trump wa Marekani.

Uamuzi huo wa Mattis umekuja baada ya tangazo la Rais Trump la kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria, hatua ambayo imewakasirisha washauri wake na washirika wa Marekani.

Hata hivyo Rais Trump wa Marekani amesema atatangaza mrithi wa Mattis hapo baadae.

Mtibwa wajipanga kuwadhibiti KCCA ya Uganda Disemba 22

0

Kocha mkuu wa Mtibwa  Sugar, Zuber  Katwila amesema anatambua kibarua walichonacho cha kupindua matokeo mbele ya Kcca ya Uganda kwenye mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho barani Afrika utakaochezwa kwenye dimba la Chamazi, lakini amekiandaa vyema kikosi chake  kwa ajili  ya kupambana na kuibuka na ushindi.

“Kikosi change kipo imara kupigania matokeo ya ushindi  kwenye mchezo huo na kwamba tutaingia na tahadhari kubwa kutokana na ubora wa wapinzani wetu na kwamba tutatumia kucheza  soka la kushambulia zaidi”alisema katwila

Mtibwa sugar wanahitaji ushindi wa mabao manne kwa bila mbele ya Kcca, ili waweze kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano hiyo kufuatia kula mweleka wa mabao matatu kwa bila katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Kampala nchini Uganda.

Mchezo huu utatangazwa mubashara na tbc taifa kuanzia saa kumi alasiri.

Katika michezo mingine ya kombe la shirikisho vita kubwa itakuwa kati ya Elgeco Plus  alfa ya madagascar wataalika kaizer chiefs ya afrika kusini katika mchezo ambao wanahitaji ushindi wa mabao manne kwa bila ili kusonga mbele.

Daring club Motema Pembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo watakuwa wageni wa fc san Pedro ya Ivory Coast baada ya sare ya bao moja kwa moja katika mchezo wa kwanza huku salimata et tasere fc ya burkina faso wakiwa na faida ya ushindi wa mabao mawili kwa bila walioupata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa juma moja lililopita nchini misri watawaalika wabaya wa simba, Al Masry ya Misri huku asante kotoko ya ghana baada ya matokeo ya suluhu ugenini juma lililopita, watakuwa wenyeji wa kariobangi sharks ya kenya.

Serengeti Boys yaendelea kujifua fainali za vijana

0

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti boys – Oscar Mirambo amesema katika kipindi kifupi kilichobaki kuelekea fainali za afrika kwa vijana wa umri huo watapambana kupata michezo ya kimataifa ya kirafiki na timu kutoka magharibi mwa bara la Afrika.

Mirambo anasema anaamini michezo ya kimataifa ya kirafiki na mataifa hayo itawajenga zaidi vijana wake kutokana na utimamu wa mwili waliokuwa nao vijana wa mataifa hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakisumbua kwenye soka la Afrika.

Kwa upande wao nahodha wa kikosi hicho Morice Abraham na mshambuliaji machachari Kelvin John wamesema wapo tayari kwa fainali hizo na watapambana kuhakikisha kombe linabaki hapa nchini.

Serengeti boys wamepangwa kundi Aa kwenye fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 pamoja na mataifa ya Nigeria, Angola na Uganda wanaoshiriki kwa mara ya kwanza fainali hizi, huku kundi Be likiwa na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Vijana wa Serengeti Boys wataanza kampeni ya kusaka taji kwa kuumana na Nigeria, Aprili 14 katika dimba la TaifA jijini dsm kwenye mchezo wa ufunguzi.

Michuano hiyo itadumu kwa wiki Mbili kuanzia aprili 14 hadi 28 katika viwanja vitatu vya jijini dsm, ambavyo ni uhuru, taifa na azam complex.

Wagombea upinzani DRC wailaumu Tume ya Uchaguzi

0

Wagombea wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC wameilalamikia Tume ya uchaguzi nchini humo Ceni kwa kuahirisha uchaguzi uliopangwa kufanyika Jumapili ya tarehe 23 mwezi huu.

Wagombea hao wamesema hawataki uchaguzi uahirishwe kwa kuwa wako tayari kwa uchaguzi huo huku wakitishia kuandamana na wafuasi wao dhidi ya maamuzi hayo ya Tume ya uchaguzi nchini humo.

Uamuzi wa kuahirisha uchaguzi huo ulitangazwa jana Desemba 20 mjini Kinshasa, na Mkuu wa Tume hiyo Norneille Nangaa ambaye ametaja  tarehe 30 Desemba ndio itakuwa siku ya uchaguzi .

Miongoni mwa sababau zilizosababisha kuahirishwa uchaguzi huo ni pamoja na  kuungua kwa ghala lenye vifaa vya uchaguzi huo mjini Kinshasa, ghasia zilizofanyika wakati wa kampeni na hofu ya kuenea kwa maradhi hatari ya Ebola Mashariki mwa nchi hiyo.

Wanane wauawa katika maandamano Sudan

0

Watu wanane wameuawa katika maandamano yaliyofanyika nchini Sudan wakipinga kupanda kwa gharama ya maisha.

Hasira zimekuwa zikiongezeka nchini Sudan kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa, ugumu wa maisha na kuwekewa ukomo wa kiasi cha fedha wanachoweza kuchukua katika akaunti zao za benki.

Waandamanaji hao pia wamemtaka Rais Omar Al Bashir wa nchi hiyo kujiuzulu.

Polisi waliwatawanya waandamanaji hao kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi  huku baadhi yao wakikamatwa na kuwekwa kizuizini.

Jimbo Katoliki la Mbeya lapandishwa hadhi

0

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Fransisko amelipandisha hadhi jimbo Katoliki la Mbeya kuwa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania imesema Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya lina majimbo ya Iringa na Sumbawanga.

Halikadhalika Papa Fransisko amemteua Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga kuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Jimbo Kuu la Mbeya.

Mpaka wakati wa uteuzi wake, Mhashamu Askofu Nyaisonga alikuwa Askofu wa Jimbo la Mpanda.