Viongozi wa upinzani nchini Sudan wahamasisha wananchi kuandamana

0

Viongozi wa upinzani nchini Sudan wameendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika maandamano ya kupinga serikali leo jumapili, baada ya maandamano hayo kuanza kusambaa nchi nzima na kusababisha serikali kutangaza hali ya tahadhari.

Waandamanaji wamekuwa wakishiriki katika maandamano ya kupinga ongezeko la bei za bidhaa za vyakula hasa mikate ambayo ndio chakula chao kikuu, pamoja na ongezeko la bei za mafuta.

Serikali ya Sudan imekuwa ikitumia nguvu kutawanya maandamano ya watu hao.

Serikali ya nchi hiyo wiki iliyopita ilitangaza hali ya tahadhari katika baadhi ya maeneo, ambako maandamano yalionekana kupambana moto na baadaye kuondoa amri hiyo katika baadhi ya maeneo, huku katika maeneo mengine ikiendelea kutekelezwa.

Hali ya tahadhari bado inaendelea kutekelezwa katika miji ya Atbara Geddaf, hadi sasa watu kumi wamekufa kutokana na maandamano ya kupinga serikali yanayoendelea nchini Sudan, yaliyoanza jumatano iliyopita.

Tetemeko la ardhi nchini Indonesia laleta maafa

0

Watu wapatao 168 wamekufa na wengine zaidi ya mia saba kujeruhiwa nchini Indonesia, baada ya tetemeko la ardhi chini ya bahari tsunami kuitikisa nchi hiyo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.

Zoezi la uokoaji linaendelea katika eneo hilo na wanasayansi wanasema Tsumani iliyotikisa eneo hilo imesababisha na mlipuko wa volkano chini ya bahari, ambao pia umeendelea kurusha matope ya moto katika eneo la Anak Krakatoa.

Maji hayo yalikuwa yakirushwa umbali wa mita ishirini kwenda juu. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na tetemeko hilo ni yale yaliyoko katika jimbo Sunda.

Watazamaji, wanamuziki na watu wote waliokuwa wakishuhudia tamasha la Muziki magharibi mwa kisiwa cha Java walijikuta wamesombwa na maji wakiwa ukumbini na kupoteza maisha baada ya mafuriko ya tetemeko hilo kuingia katika ukumbi wa tamashaa hilo la muziki.

Tetemeko hilo lilikuja kwa ghafla sana kiasi kwamba kulikuwa hakuna tahadhari wala onyo lolote lililokuwa limetolewa kabla ya tukio.

Kapteni Mapunda apewa milioni 10 na Rais Magufuli

0

Rais John Magufuli ametoa Shilingi Milioni 10 kwa Kapteni Mstaafu Narzis Mapunda kwa ajili ya kuthamini mchango wake wa kusaidia kuokoa ndege ya Shirika la Ndege nchini -ATCL mwaka 1977.

Mbali na kutoa fedha hizo Rais Magufuli pia amempatia mstaafu huyo zawadi ya kusafiri katika ndege za ATCL kwa wakati wake mpaka atakapofariki akiwa yeye na mkewe eneo lolote itakapotua.

Kapteni Narzis Mapunda alikataa kushusha abiria waliokuwemo kwenye ndege baada ya kuelezwa kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku ikiwa na abiria wengi waliokuwa wakielekea Jijini Dar es salaam.

Hivyo Kapteni Mapunda aliamua kuelekea Dar es salaam na kwa kufanya hivyo kuliweza kuikoa ndege hiyo na kukabidhiwa nchini.

Watendaji 100 kukatwa mishahara yao

0

Rais Magufuli ameagiza watendaji wote waliokata tiketi za Shirika la Ndege nchini -ATCL  na kushindwa kusafiri kwa kutumia tiketi zao kukatwa katika mishahara yao gharama ya tiketi hizo.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo mbele ya wananchi kwenye hafla ya kupokea ndege mpya Air Bus 220 Jijini Dar es salaam  na kusema kuwa serikali haiwezi kuingia hasara kutokana na watendaji hao ambao hawakufanya safari zao kama walivyokusudia.

Amesema kuwa watendaji hao wanaofikia Mia Moja watakuwa mfano wa watendaji wengine wasio na huruma kwa fedha za walipa kodi.

Ameendelea kuwasisitiza wananchi kuwa wazalendo kwa nchi yao jambo ambalo litasiaidia nchi kusonga mbele katika maendeleo.

Bilioni 28 zapatikana kutokana na mapato ya ndege mpya

0

Jumla ya Shilingi Bilini 28 zimepatikana kutokana mapato ya ndege mpya zilizoaingizwa nchini  kuanzia mwaka 2016.

Hayo yamesemwa na Rais John Magufuli  katika hafla ya kupokea ndege mpya Air Bus 220 inayotokea nchini Canada ambapo ameeleza kuwa mapato hayo yaliyopatikana ni chachu kubwa ya kufanyika kwa maendeleo zaidi katika sekta ya uchukuzi hapa nchini.

Rais Magufuli amesema anafurahi kuwa mpaka sasa Shirika la Ndege nchini limewepa kupata mapato makubwa tangu ndege hizo zimeanza kufanya kazi nchini na kulitaka kuhakikisha wanaongeza juhudi za kufanya biashara ili kuongeza mapato zaidi.

Amesema kuwa sekta ya uchukuzi  inachochea sana katika suala la utalii hapa nchini na kuongeza mapato kutokana na watalii wanaokuja nchini .

Hata hivyo amewataka wafanyakazi wa ATCL kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kuweka uzalendo mbele na kutoa huduma zilizo bora.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli,Tanzania ndio nchi ya kwanza kununua ndege ya aina hii katika Bara la Africa.

Mkoa wa Dar es salaam wajipanga ulipaji wa kodi nchini

0

Mkuu wa Mmkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amesema yeye na uongozi wa mkoa wake wanatarajia kutengeneza mkakati mahsusi wa namna ya kulifanya Jiji la Dar es salaam kuwa kinara katika ulipaji wa kodi nchini.

Makonda amesema hayo wakati hafla ya kupokea ndege mpya Air Bus 220 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa mkakati  huo utawezesha  kupatikana mapato kwa wingi na kusaidia kuongeza pato la Taifa.

“Tutahakikisha tunakuja na mkakati wenye tija wa kuhakikisha mkoa unakuwa kinara katika ulipaji kodi kimkoa”alisema Makonda

Ametoa wito kwa wanancchi wa Mkoa wa Dar es salaam kulipa kodi kwa lengo la kuleta maendeleo mbali mbali nchini .

Walimu nchini watakiwa kufanya kazi kwa umakini

0

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha amewataka waalimu wa somo la hisabati nchini kutokuwa chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya katika somo hilo na badala yake wawe msaada kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu wa somo hilo na sayansi kwa ujumla.

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Wilayani Korogwe Mkoani Tanga wakati akifunga mafunzo kwa waalimu wa Somo la Hisabati kutoka katika halmashauri 12 nchini zilizofanya vibaya katika somo la hisabati katika mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne ambapo amesema baadhi ya waalimu wamekuwa wakichangia wanafunzi kulichukia somo la hisabati kwakuwa mbinu wanazotumia kufundishia sio shirikishi.

Jumla ya waalimu 48 wa somo la hisabati wa shule za msingi na sekondari kutoka Halmashauri 12 za Meatu, Mkalama, Simanjiro, Ukerewe, Gairo, Momba, Rufiji, Nyasa, Korogwe, Madaba, Ruangwa na Nanyamba ambazo zimefanya vibaya kwa miaka mitatu mfululizo katika matokeo ya darasa la saba na kidato cha nne wamepatiwa mafunzo ya kuwawezesha kupata ufaulu katika shule zao.

Makubaliano yawekwa katika kusimamia sekta ya uvuvi nchini

0

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rashid Ali Juma, Mjini Unguja na kumweleza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahakikisha miradi inayohusu wavuvi inamnufaisha mvuvi moja kwa moja.

Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Makame Ali Ussi, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Islam Seif Salum pamoja na watendaji wengine Naibu Waziri Ulega amesema lengo kuu la ziara yake ya siku moja Visiwani Zanzibar ni kutazama shughuli za Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu Zanzibar kupitia mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi -SWIOFISH.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Rashid Ali Juma amesema uchafuzi wa bahari, uwepo wa maharamia na uvuvi haramu ni mambo ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kukabiliana nayo ili kuhifadhi bahari na kufanya sekta ya uvuvi kuwa yenye tija kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvyvi Abdalla Ulega ametoa wito kwa watendaji hao kutumia Shilingi Bilioni Tano zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi wa SWIOFISH ili kuleta mapinduzi ya kweli katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha wanafanyakazi kwa kasi kulingana na matarajio ya serikali zote mbili kwa wananchi wake.