Mashindano ya Taifa ya kikapu kufanyika tena Simiyu

0

Baada ya mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu kufanyika kwa mafanikio mkoani Simiyu, uongozi wa shirikisho la mpira wa kikapu nchini TBF umeamua kuyapeleka tena mashindano hayo mkoani humo msimu ujao.

Rais wa TBF Phares Magesa amesema maandalizi yaliyofanywa na mkoa huo yameshawishi kuyarudisha mkoani Simiyu mashindano hayo mwakani.

Pia amesema mashindano hayo yamesaidia kuunda kikosi imara cha timu ya taifa ya mpira wa kikapu.

Mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu yaliyomalizika Jumapili Desemba 23 kwa timu ya mkoa wa Dar Es Salaam ya mchezo huo (The Dream Team) kutwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kuinyuka timu ya mkoa wa Mwanza alama 78 kwa 75 kwenye mchezo wa fainali.

Tsunami yasababisha hofu Indonesia

0

Hali ya wasiwasi imeongezeka nchini Indonesia baada ya nchi hiyo kukumbwa na tetemeko la chini ya bahari Tsunami, kwa kuwa kuna uwezekano wa kutokea Tsunami nyingine.

Wanasayansi nchini Indonesia wamesema mlima Anak Krakatau wenye volkano hai ulioko chini ya bahari umelipuka na kusababisha Tsunami hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia jana na kusababisha vifo vya watu 373.

Wanasayansi wamesema volkano ya mlima Anak Krakatau, jina linalomaanisha mtoto wa Krakatau inaonyesha dalili ya kuanza kulipuka tena na haifahamiki, safari hii italeta athari gani, kwani mlipuko wa kwanza ulitokea bila taarifa.

Habari zinasema katika pwani ya nchi hiyo matope ya moto kutoka baharini yanaweza kuonekana yakirushwa juu na hivyo watu hawajui watajisalimisha vipi.

Maelfu ya watu bado wako katika makazi ya muda baada ya maelfu ya nyumba kusombwa na maji yaliyokumbwa na Tsunami hiyo kutoka baharini na kwenda katika nyumba za watu na kusomba na hoteli pia.

Zoezi la kuwatambua watu waliokufa kwa Tsunami linaendelea na waokoaji wanaendelea kwa kazi ya kuwatafuta watu walionusurika na tukio hilo, kabla haujatokea mlipuko mwingine.

Watafiti waaswa kufanya tafiti bora

0

Wataalamu na watafiti wa Taasisi ya Utafiti Nchini -TARI wametakiwa kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija katika msimu ujao wa kilimo.

Akizungumza na wataalam wa taasisi hiyo wilayani Kibaha mkoani Pwani Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geofrey Mkamilo amesema endapo watafiti hao watafanya kazi zao vizuri na kuzifikisha kwa wakulima ipasavyo uhaba wa chakula nchini unaweza kuwa historia.

Kwa upande wake mtaalamu wa kituo hicho akiwemo Afisa Utafiti Kilimo Mkuu Dkt. Stephen Ngairo amesema kwa sasa wanaendelea kujipanga kuhakikisha wanasaidia katika sekta ya kilimo na namna ya kuongeza uzalishaji kwa mkulima  mdogo.

Waumini wa dini ya Kikristo watakiwa kudumisha amani

0

Waumini wa dini ya Kikristo nchini wametakiwa kutenda mema pamoja na kuwa wajasiri, waadilifu na wenye uthubutu kutenda mambo mema ili kudumisha amani na umoja ambavyo ni tunu ya taifa.

Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland – AICT nchini Mussa Magwesela katika ibada maalum ya kumuweka wakfu na kusimikwa kazini Askofu Philip Mafuja kuwa Askofu wa AICT Dayosisi ya Mwanza.

Amesema waumini na wananchi wote kwa ujumla wanawajibika katika nafasi zao ili kulinda amani, umoja na mshikamano nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela amesema Kanisa lina mchango mkubwa kulinda amani na kutoa rai kwa waumini kuliombea taifa na Rais Magufuli.

Uchaguzi wa kumchagua Askofu wa Dayosisi ya AICT hufanywa na sinodi kuu ambayo huundwa na wachungaji wa Kanisa hilo ambapo mshindi anayeteuliwa kuwa Askofu baada ya kupata theluthi mbili ya kura zote.

Simba yatinga hatua ya makundi michuano ya Afrika

0

Mabingwa wa soka la Tanzania Bara, klabu ya Simba imetinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya miaka 15 kupita baada ya kuinyuka timu ya Nkana FC ya Zambia mabao matatu kwa moja.

Timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi, Kariakoo imetinga hatua ya makundi baada ya kupindua matokeo ya kichapo cha mabao mawili kwa moja kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa wiki moja iliyopita nchini Zambia.

Bao la dakika ya 89 la kiungo Clatous Chama limeivusha timu hiyo baada ya mchezo huo kusomeka mabao mawili kwa moja hadi dakika ya 88 na hivyo bao hilo likaufanya mchezo huo usifike kwenye changamoto ya mikwaju ya penati.

Mara ya mwisho klabu ya Simba kutinga hatua ya makundi ilikuwa mwaka 2003 ambao ulikuwa ni miongoni mwa msimu wa mafanikio kwenye anga za kimataifa kwa klabu hiyo.

Simba inaungana na baadhi ya vilabu vingine kama Wydad Casablanca ya Morocco, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Orlando Pirates ya Afrika Kusini zilizotinga hatua hiyo pia.

Timu nyingine zilizotinga hatua hiyo ni Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini, Ismailia na Al Ahly za Misri, Lobi Stars ya Nigeria pamoja na bingwa mtetezi Esperance ya Tunisia

Droo ya hatua ya makundi itapangwa ijumaa, desemba 28 mwaka huu ambapo timu 16 zitakazotinga hatua ya makundi zitapangwa kwenye makundi manne yenye timu nne nne.

Michuano Kombe la Shirikisho nchini kuendelea leo

0

Michuano ya Kombe la Shirikisho nchini inaendelea leo kwa mchezo mmoja kwenye dimba la Taifa jijini Dar Es Salaam kwa wenyeji Yanga kuvaana na  Banyampala – Tukuyu Stars kutoka jijini Mbeya.

Yanga wanaingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa hasa baada ya timu kadhaa za ligi kuu kutupwa nje ya michuano hiyo na timu za ligi daraja la kwanza lakini pia historia ya Tukuyu Stars ikiwafanya kuwa makini zaidi.

Mpaka sasa timu tano za ligi kuu ambazo ni Ruvu Shooting Stars ya mkoani Pwani, Mwadui FC ya Shinyanga, Tanzania Prisons ya Mbeya, Ndanda FC kutoka Mtwara na Mbao FC ya jijini Mwanza zimeshafungasha virago kwenye michuano hiyo.

Bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa msimu ujao wa mashindano.

Golden Warriors yaendelea kupata ushindi NBA

0

Ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani ya NBA imeendelea ambapo bingwa mtetezi Golden State Warriors wameendeleza wimbi la ushindi kwa kuinyuka Los Angeles Clippers alama 129 kwa 127 kwenye mchezo uliochezwa kwenye dimba la Oracle mjini Oakland – California.

Nyota wa mchezo huo alikuwa Stephen Curry aliyefunga alama 42 huku Kevin Durant akifunga nyingine 35 na kucheza mipira iliyorudi uwanjani yaani rebounds 12 na kulizamisha jahazi la Clippers lililokuwa likiongozwa na Tobias Harris aliyefunga alama 32 na kucheza rebounds 9.

Wakati Warriors wakitakata makamu bingwa Cleveland Cavaliers wameendelea kupokea kipigo baada ya kunyukwa alama 112 kwa 92 na Chicago bulls.

Huu unakuwa mchezo wa 26 kwa Cavaliers kupoteza katika msimu huu, huku wakiwa wameshinda michezo 8 pekee na kuna wasiwasi kuwa huenda wakashindwa kufuzu kwa hatua ya mtoano yaani play off kama mambo yataendelea kuwaendea kombo.

Huko TD Garden mjini Boston – Massachusetts wenyeji Boston Celtics wameitandika Charlote Hornets alama 119 kwa 103 wakati Washington Wizards wakishindwa kutamba mbele ya Indiana Pecers na kula mweleka wa alama105 kwa 89 huku Orlando Magic wakikiona cha moto mbele ya Miami Heat kwa kutandikwa alama 115 kwa 91.

Waandamanaji wajitokeza tena jijini Paris kuipinga serikali

0

Waandamanaji wa wanaopinga serikali ya Ufaransa, maarufu kama manjano wamejitokeza tena katika mitaa ya mji wa Paris nchini humo kuendelea na maandamano ya kupinga sera za rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.

Maandamano ya safari hii yamekuwa ya amani ikilinganishwa na maandamano yaliyopita. Watu wapatao elfu arobaini wameshiriki katika maandamano ya safari hii ikilinganishwa na maelfu ya watu walioshiriki katika maandamano yaliyopita.

Serikali ya Ufaransa, ililazimika kutumia askari wa ziada kutawanya maandamanao ya Manjano yaliyopita ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta na ugumu wa maisha yaliyosambaa, karibu nchi nzima ya Ufaransa.