Waandamanaji wapambana na polisi nchini Sudan

0

Kwa mara nyingine tena waandamanaji nchini Sudan wamepambana na polisi wa kutuliza ghasia, katika maandamano yao ya kupinga serikali, wakiwa wameingia katika siku yao ya nane ya maandamano hayo.

Rais Omar Abashir wa Sudan amewaita waandamanaji hao kuwa wasaliti na kuwataka kuachana na maandamano hayo mara moja. Jana polisi walitumia risasi za moto kuwazuia waandamanaji waliokuwa wakielekea katika ikulu ya nchi hiyo.

Awali waandamanaji waliokuwa wakiandamana kupinga serikali ya Sudan, walikuwa wakiandamana kupinga ongezeko la bei ya mikate na bidhaa za mafuta ya magari, lakini maandamano ya safari hii yamekuwa na sura nyingine.

Waandamanaji wanasema wataendelea na maandamano yao hadi serikali ya rais Bashir itakapoachia madaraka, na kupatikana kwa uongozi mpya. Maandamano mengine yanatarajiwa kufanyika leo nchini Sudan.

Maandamano ya safari hii yamekuwa na sura nyingine, kwani licha ya waandamanaji kushuhudia wenzao wakipigwa risasi na kufa, wamekuwa wakisonga mbele ya kuendelea na maandamano yao.

Wanaume wa wilaya ya Kibondo wavunja ukimya juu ya manyanyaso

0

Baadhi ya wanaume katika kata ya Kibondo mjini wilayani Kibondo mkoani Kigoma wamelalamikia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanavyofanyiwa na wake zao ikiwemo kupigwa pamoja na kufanyishwa kazi za ndani.

Licha ya kutendewa vitendo hivyo,wanaume hao wamesema kuwa wanashindwa kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wanaotendewa na wake zao kutokana na changamoto zao kutotatuliwa.

Baadhi ya wanaume hao wamesema wameamua kuvunja ukimya kuhusu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao ili wapate msaada na kuondokana na vitendo hivyo.

Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya KIBONDO Mjini Phinias Samizi amesema wanawake na watoto ndio wahanga wakubwa wa unyanyasaji wa kijinsia katika kata hiyo hivyo taarifa hiyo kutoka kwa wanaume hao wanaipokea na wataifanyia kazi.

Hayo yamebainika katika Mdahalo uliolenga kuielimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia ambao umeendeshwa na shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana la kivulini.

Makundi kombe la klabu bingwa Afrika kujulikana Disemba 28

0

Droo ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika inatarajiwa kufanyika Ijumaa Disemba 28 makao makuu ya shirikisho la soka barani Afrika-Caf jijini Cairo nchini Misri.

Katika droo hiyo wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo ambao pia ni wawakilishi pekee kwa nchi za Afrika Mashariki, timu ya Simba itawakilishwa na mwenyekiti wa bodi ya klabu hiyo Swed Nkwabi.

Shirikisho hilo limepanga poti ama vyungu vinne ambapo kila chungu kina timu 4 huku kila poti itatoa timu moja kuunda kundi moja.

Poti hizo zimepangwa kulingana na matokeo chanya ya klabu kwa miaka mitano iliyopita katika ligi ya mabingwa barani Afrika na michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Chungu cha kwanza kina timu za Tp Mazembe Englebert kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye alama 66, Al Ahly ya Misri yenye alama 62, Wydad Casablanca ya morocco yenye alama 51 na Esperance Sportive De Tunis ya Tunisia yenye alama 45.

Chungu cha pili kina timu za Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini yenye alama 40, As Vita club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye alama 29, Horoya ya Guinea yenye alama 19 na club African ya Tunisia yenye alama 12.

Katika chungu cha tatu kina timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 8.5, Orlando Pirates ya Afrika Kusini yenye alama 8, fc Constantine ya algeria na fc platinum ya Zimbabwe zenye alama sifuri.

Na katika chungu cha nne kuna timu za Simba ya Tanzania, Lobi Stars ya Nigeria , Ismaily ya Misri na Js Saoura ya Algeria zote zikiwa na alama sifuri.

Kila chungu kitatoa timu moja kwa kila kundi huku timu zilizo katika poti moja haziwezi kupangwa kundi moja na kutakuwa na makundi manne yenye timu nne na kila timu itacheza mechi 6 ikiwa mechi 3 za nyumbani na mechi 3 za ugenini.

Mechi za makundi zitaanza Mwezi Januari hadi Machi ambapo mechi za kwanza kwenye kundi zitachezwa kati ya Januari 11 hadi 13, mechi za pili kwenye kundi zitachezwa kati ya Januari 18 hadi 20 ,mechi za tatu zikipangiwa kuchezwa kati ya Februari MOSI hadi TATU wakati mechi za nne zitachezwa kati ya Februari 12 hadi 13, mechi za tano kwenye kundi zitachezwa kati ya machi 8 hadi 11 na mechi za mwisho kwenye kundi zitachezwa kati ya machi 15 hadi18.

Timu mbili zitakazomaliza kwenye nafasi ya juu kwenye kila kundi zitafuzu kucheza robo fainali ya michuano hii ya ligi ya mabingwa barani Afrika na droo ya Robo fainali na nusu fainali itafanyika Cairo Misri March 23.

Mechi za Robo fainali zitachezwa kati ya April 5 hadi 7, nusu fainali kati ya Aprili 26 hadi 28 na fainali itachezwa kati ya Mei 24 na 25.

Watoto waaswa kuwa wazalendo na wenye heshima kwa wazazi wao

0

Mkurugenzi mkuu wa shirika la utangazaji Tanzania Tbc Dakta  Ayub Rioba amewaasa watoto kuwatii na kuwaheshimu walezi na wazazi wao ili Taifa liwe na kizazi chenye uzalendo kwa taifa lao.

Dakta Rrioba ameyasema hayo kwa njia ya simu alipokuwa akitoa salamu za kristmass kwa watoto waliokuwa katika kipindi cha watoto na kristmass kilichorushwa na Tbc taifa na kusema kuwa iwapo watoto wakizingatia mafundisho wanayopewa na walezi na wazazi wao taifa litakuwa na viongozi wazuri wa baadae.

Dakta Rioba pia amewakumbusha wazazi na walezi kutimiza wajibu wao katika malezi ili kuwezesha Taifa kuwa na viongozi watakao fuata nyayo za Rais dakta John Magufuli ya kuonyesha dira ya maisha ya kesho.

Amesema Rais Dakta John Magufuli amedhibiti vitendo visivyofaa na kutokomeza rushwa, vitendo vya wizi na kufanya taifa liwe na watu waadilifu pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kuboresha miundombinu mbalimbali.

Mamlaka ya bima kuchukua hatua kwa wanaogushi bima

0

Mamlaka ya Usimamizi wa shughuli za bima nchini – TIRA imesema itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria watakaobainika kughushi bima kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kufanya vitendo hivyo.

Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Kati Stela Rutaguza ametoa onyo hilo jijini Dodoma kwenye semina ya kuwapatia elimu ya bima madiwani wa jiji hilo na kubainisha kuwa hivi sasa inawashikilia watu wanne kwa kosa la kughushi bima.

Baadhi ya madiwani walioshiriki semina hiyo wameomba elimu zaidi kuhusu bima kuendelea kutolewa kwa wananchi wa vijijini ili wajiunge na bima.

Marekani kupambana na IS

0

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeridhia majeshi ya nchi hiyo yaliyokuwa nchini Syria kupambana na wapiganaji wa kikundi cha IS waliokuwa wakitishia usalama nchini humo kurejea nyumbani, baada ya kazi ya kuwatokomeza wapiganaji hao kumalizika.

Wakati majeshi ya Marekani yakianza kurejea nyumbani, majeshi ya serikali ya Uturuki yameanza kuelekea nchini Syria kupambana na waasi.

Maandalizi ya sikukuu za Krismas yaendelea

0

Maandalizi ya sherehe za Krismas yanaendelea mjini Bethlehem, eneo ambako inasadikiwa alizaliwa Yesu Kristo.

Habari kutoka mjini Bethlehem zinasema ibada ya Krismas mwaka huu itafanyika nje ya Kanisa na Netevity ambamo Yesu alizaliwa ili kutoa fursa kwa wakristo kutoka Mamlaka ya Palestina, kushiriki kwa wazi misa hiyo.

Maelfu ya watu kutoka katika maeneo mbalimbali duniani wameanza kuwasili mjini Bethlehem kwa ajili ya sherehe za Krismas.

Desemba 25 kila mwaka waumini wa dini ya Kikristo huadhimisha kuzaliwa kwa mwokozi wao takriban miaka elfu mbili iliyopita.

Unywaji wa pombe uliokithiri chanzo familia kutelekezwa

0

Unywaji wa pombe uliokithiri mkoani Kigoma umechangia kuongezeka kwa idadi ya wanaume wanaotelekeza familia zao na hivyo kusababisha ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Baadhi ya wanawake waliotelekezwa na wenzi wao katika kijiji cha Mabamba wilayani Kibondo wameiomba serikali kuwasaidia ili wapate haki ya matunzo ya watoto wao.

Wakizungumza katika mdahalo wa kuielimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia,baadhi ya wanawake waliotelekezwa na wenzi wao katika wilaya ya Kibondo wameiomba serikali kuwasaidia kupata haki ya matunzo ya watoto wao.

Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma inakabiliwa na ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kutokana na baadhi ya wazazi wa kiume kutelekeza familia zao.

Hali hiyo imechangia baadhi ya watoto kukimbilia mitaani kwa  kukosa mahitaji muhimu.