Kikokotoo cha zamani kuendelea kutumika kipindi cha mpito

0

Rais John Magufuli ameagiza wastaafu wote waliofikia umri wao wa kustaafu kulipwa kulingana na kikotoo kilichotumika katika mifuko yao ya hifadhi ya jamii kabla mifuko hiyo haijaunganishwa kwa kipindi cha mpito hadi mwaka 2023.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar Es Salaam kwenye mkutano na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini na watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na viongozi wa serikali ambapo amesema kustaafu ni heshima hivyo wafanyakazi lazima waheshimiwe kutokana na kufanya kazi kwao.

“Nimeamua kuanzia leo wastaafu wote walipwe kwa kikotoo kilichokuwepo cha zamani kwenye mifuko yao na si vinginenvyo na baadae ndio yaletwe mapendekezo mapya ya kikokotoo kilicho bora na si kwa sasa kwa kuwashtukiza wastaafu ambao wamefanya kazi kwa heshima”alisema Rais Magufuli.

Amesema katika kipindi cha mpito ana uhakika  msimamizi wa mifuko pamoja na serikali wataweza kukaa pamoja na kushirikiana kuwa na kikotoo ambacho kitakuwa bora na chenye kuridhisha pande zote.

Rais Magufuli amewataka wafanyakazi wote nchini kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha malengo yanatimia na kusaidia maendeleo hapa nchini.

Rais kukutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na watendaji wa mifuko nchini

0

Rais. Dkt. John Magufuli anakutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi –TUCTA, vyama shiriki, watendaji wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii –PSSSF na NSSF na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii –SSRA, kujadili masuala yahusuyo mafao ya wafanyakazi hususani Kikokotoo.

Mkutano huo utafanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara husika watashiriki.

Mazungumzo ya Rais Magufuli na viongozi hao yatarushwa moja kwa moja yaani Live   na vyombo vya habari vya Redio, Televisheni, www.ikulu.go.tz, youtube ya ikulumawasiliano na mitandao ya kijamii muda wowote kunzia sasa

TCAA yashughulikia maombi ya Fastjet

0

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini – TCAA imesema inashughulikia maombi ya kampuni ya ndege ya Fastjet kuingiza ndege nchini kwakuwa lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha huduma za usafiri wa anga zinakuwa salama kwa wateja wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema Mamlaka hiyo haijazuia Fastjet kuingiza ndege mpya kwa ajili ya kuendelea na biashara nchini.

Johari amesema mamlaka hiyo inapenda kuona huduma ya usafiri wa anga inakuwa na ushindani na kutoa huduma zenye uhakika na usalama kwa wateja wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi za sekta binafsi Godfrey Simbeye amezishauri taasisi binafsi kuzingatia sheria katika uendeshaji wa shughuli zao.

Ubadhirifu wa shilingi Bilioni 2.9 kujadiliwa Ulanga

0

Mkuu wa mkoa wa Morogoro  Dkt. Kebwe  Stephen  ameagiza kuitishwa kwa baraza la dharura la Halmashauri ya wilaya ya Ulanga kujadili taarifa ya Tume iliyoundwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI kuchunguza tuhuma za  ubadhirifu wa shilingi Bilioni 2.9 zinazodaiwa kutumika kinyume na utaratibu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Morogoro, Dkt. Kebwe pia ameagiza aliyekuwa  mhasibu  mkuu wa halmashauri hiyo Rajabu Siriwa ambaye amehamishiwa wilayani Gairo kurejea  mara moja wilayani Ulanga ili kujibu tuhuma hizo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro ametoa wito kwa watumishi wa umma kuhusu matumizi ya fedha za serikali huku akimuelekeza Katibu Tawala wa mkoa huo kufuatilia utekelezwaji wa maagizo ya Tume hiyo.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi anaeshughulikia serikali za mitaa Noel Kazimoto amesema hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika na makosa hayo.

Byakanwa ahoji utendaji wa TARURA Mtwara

0

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amesema haridhishwi na utendaji kazi wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini – TARURA – mkoani humo ambao amewatuhumu kufanya kazi kwa kukurupuka bila ofisi yake kupewa taarifa.

Byakanwa ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza kwenye kikao cha Bodi ya Barabara na kusema amelazimika kuunda Tume kuchunguza barabara zote za wilaya ya Mtwara ambazo hazipitiki na kuleta adha kwa wananchi.

Ubovu wa baadhi ya barabara katika manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashauri ya mji wa Nanyamba wilaya ya Mtwara umekuwa ukilalamikiwa na wakazi wa maeneo hayo mara kwa mara.

Baadhi ya wadau wa kikao hicho wameomba TARURA kushirikisha ofisi za Halmashauri kazi wanazofanya ili kuondoa mkanganyiko.

Wakazi wa Rorya waomba wadau kuwachangia ujenzi wa zahanati

0

Wakazi wa Kijiji cha Dett Kata ya Nyaburogo Wilayani Rorya Mkoani Mara wameiomba serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuunga mkono jitihada zao ili kufanikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.

Wakazi hao wametoa ombi hilo kufuatia kukwama kwa ujenzi wa zahanati yao kwenye hatua ya kuezeka  ambapo Mbunge wa Rorya Lameck Airo amewataka wasikate tamaa na badala yake waendelee kuchangia ujenzi huo ili kusogeza huduma za afya karibu.

Hadi kufikia sasa ujenzi huo shilingi milioni 15 ambayo ni michango ya wananchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Rorya ameendesha harambee ya ujenzi huo na kufikisha kiasi cha shilingi milioni 12.

Liverpool yapaa kieleleni Ligi ya England

0

Liverpool imezidi kujikita kileleni mwa Ligi Kuu ya England na kuiacha Manchester City kwa alama 11 baada ushindi wa magoli manne kwa bila dhidi ya Newcastale United katika mchezo uliopigwa kwenye Dimba la Anfield.

Katika mchezo huo magoli ya Liverpool yamefungwa na wachezaji Dejan Lovren dakika ya 11 huku mchezaji Mohamed Salah akifunga kwa mkwaju wa penati dakika ya 48 na magoli mengine mawili yamefungwa na wachezaji Shaqiri na Fabinho.

Kutokana na ushindi huo Liverpool imefikisha alama 51 huku Manchester City ambao walikuwa wanaongoza ligi kwa muda mrefu wakiporomoka hadi nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 44 baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Leicester City  kwa kutandikiwa magoli mawili kwa moja ugenini.

Huu ni mchezo wa pili mfululizo kwa Manchester City kupoteza baada ya hivi karibuni kufungwa na Cystal Palace magoli matatu kwa mawili.

Katika mchezo huo mchezaji Ricardo Pereira ndiye alipeleka kilio Manchester City kwa kufunga goli dakika za lala salama za mchezo.

Manchester City walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 14 kupitia kwa mchezaji Benardo Silva.

Leicester City wakasawazisha dakika 19 ya mchezo kupitia kwa mchezaji wake Marc Albrighton.

Nayo Tottenham Hotspur wamepanda hadi nafasi ya pili kwa kufikisha alama 45 baada ya kuichapa Bournemouth magoli matano kwa bila.

Magoli ya Tottenham yamefungwa na wachezaji Eriksen akifunga dakika ya 16, Son Heung Min akifunga magoli mawili dakika ya 23 na 70 na magoli mengine yakipachikwa na wachezaji Lucas Moura na Harry Kane.

Bondia Cheka atandikwa na Dulla Mbabe

0

Bondia Abdallah Pazi maarufu Dulla Mbabe ndiye mfalume mpya wa masubwi Tanzania baada ya kumatandika Francis Cheka kwa Knock Out na kunyakua taji la mabara.

Mabondia wote walirushiana  makonde mazito lakini Dulla ndiye aliyemchapa makonde mazito zaidi mpizani wake Cheka katika mzunguko wa tatu na bondia Cheka kuokolewa na kengele.

Mabondia hao walicheza vyema katika mzunguko wa nne, tano na sita na hatimaye Dulla Mbambe akamtandika konde zito lilompeleka chini Francis Cheka na kuhitimishi rasmi ubabe wake katika masubwi hapa nchini.