Wamiliki wa maabara kufuata taratibu za usajili

0

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wamiliki wa maabara binafsi za afya kufuata utaratibu wa kusajiliwa na kutambuliwa kisheria.

Akizungumza jijini Dar Es Salaam na waandishi wa habari Dkt. Gwajima amesema wamiliki wa maabara ambao hawatimiza matakwa ya kisheria watafungiwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema wizara hiyo inashirikiana na viongozi wa serikali kuu na serikali za mitaa ili kubaini maabara zinazokiuka taratibu na sheria.

Mpaka sasa ni asilimia 58 za maabara binafsi zilizopo nchini ndizo zinatekeleza matakwa ya kisheria.

Tume ya ushindani nchini kufungua ofisi kila kanda

0

Tume ya Ushindani Nchini – FCC – imeweka mikakati ya kufungua ofisi zake kila kanda ili kusimamia kwa ukaribu ushindani wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa hapa nchini ili kumlinda mlaji.

Mkurugenzi wa FCC Dkt. John Mduma amesema hayo mkoani Mtwara katika semina kuhusu sheria ya ushindani kwa wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa.

 Amesema ili kuhakikisha Tume inafanya vizuri imeweka mikakati ya kufungua ofisi kila kanda ili kusimamia kwa ukaribu ushindani wa bidhaa zinazozalishwa na zinazoingizwa hapa nchini ili kumlinda mlaji.

Tume ya ushindani kwa sasa inafanya uchunguzi kwa wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni zinazozalisha bidhaa zinazofanana ambao wana mpango wa kutopeleka bidhaa sokoni kwa lengo la kuharibu ushindani.

Wananchi wa Bariadi waaswa kuchemsha maji ya kunywa

0

Wananchi wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wameaswa kuwa na utamaduni wa kuchemsha maji ya kunywa ili kuepuka magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu, homa ya tumbo na minyoo.

Hayo yamesemwa na Afisa Afya wa Wilaya ya Bariadi Jumanne Kisanka wakati wa mkutano na watendaji wa vijiji na madiwani wa Tarafa ya Dutwa.

Kisanka amesema visima vingi vya maji havifunikwi na wengine wanachota maji kwenye mito bila kujali usalama wa maji hayo ambapo amewaomba wananchi kuchukua tahadhari ya kuchemsha maji kabla ya kuyanywa.

Katika hatua nyingine Kisaka amewataka viongozi hao kuhakikisha shule zote za msingi katika eneo hilo zina matundu ya vyoo na kwamba shule ambazo hazitakuwa na vyoo vya kutosha zitafungwa.

Kocha wa Manchester City ajitapa kunyakua ubingwa wa England

0

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kikosi chake lazima kikubali kuwa wapinzani wao kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England, Liverpool huenda ndiyo timu bora kwa sasa duniani.

Mabingwa hao watetezi ambao jana wameibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Southampton alhamisi wiki hii wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kumenyana na vinara Liverpool kwenye Dimba la Etihad huku tofauti ya alama baina yao ikiwa ni alama saba.

Kuelekea mchezo huo Guardiola anasema tatizo ni kwamba wapinzani wao wapo kwenye ubora wa hali ya juu na wanaweza kuwa ni timu bora kwa sasa Barani Ulaya na hata duniani.

Wakati Manchestr City wakipokea vipigo kutoka kwa Chelsea, Crystal Palace na Leicester City Liverpool wao wameshinda mechi zao zote saba walizocheza na wamemaliza mwaka 2018 kwa kugawa dozi nzito baada ya kuitandika Arsenal mabao matano kwa moja.

Kocha wa Manchester United asema wataongeza bidii kupata ushindi zaidi

0

Kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema hatajikita zaidi kwenye soka la kushambulia baada ya kikosi chake kufunga goli la 12 kwenye mchezo wa tatu akiwa kama kocha wa Manchester United wakiilaza FC Bournemouth mabao manne kwa moja.

Solskjaer anasema kila mmoja anadhani kuwa anapendelea soka la kushambulia zaidi muda wote lakini msingi wa yote hayo ni namna unavyojilinda na kutoruhusu kufungwa huku ukitengeza nafasi ya kushinda.

Decemba 30 Manchester United imeibuka na ushindi wa mabao manne kwa moja dhidi ya FC Bournamouth mabao mawili kati ya hayo yakifungwa na Paul Pogba ambaye amehusika kwenye mabao sita kati ya 12 kwenye mechi tatu zilizopita akifunga manne na kutoa pasi za mabao mbili huku mabao mengine yakifungwa na Marcus Rashford na Romelu Lukaku.

Manchester United imeshinda michezo yote mitatu ikiwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer na sasa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiwa alama tatu nyuma ya Arsenal wanaoshika nafasi ya tano.

Manaibu Waziri Biteko na Mavunde wawacharukia wazalisha kokoto mkoani Dodoma

0

Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde Decemba 30 wametembelea kwa kushtukiza katika migodi ya machimbo ya kokoto katika eneo la Chigongwe Jiji la Dodoma ili kujionea shughuli za uchimbaji na usagaji mawe.

Ziara hiyo ni kutokana na agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kutaka wazalishaji wa kokoto waliopata tenda ya kusambaza kokoto katika ujenzi wa mji wa serikali kuongeza kasi ya uzalishaji ili iendane sambamba na kasi ya ujenzi ambapo mahitaji ya kokoto yamekuwa makubwa sana.

Naibu Waziri Biteko amezitaka Kampuni za Adili S.Y Dhiyeb na Loray Aggregates Company Ltd kuanza uzalishaji mara moja ifikapo tarehe 3.01.2019 ili kukidhi mahitaji ya kokoto katika ujenzi wa Mji wa Serikali na na kuwapa tahadhari ya kuwa ya kwamba ikidhihirika hawana uwezo huo wa kuendana na kasi ya ujenzi wa mji wa serikali,Wizara itapanua fursa hii ya usambazaji wa kokoto kwa wazalishaji nje ya mkoa wa Dodoma ili shughuli za ujenzi zisikwame.

Kwa upande wake naibu Waziri Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini amewataka wazalishaji wa kokoto Dodoma kuitendea haki fursa hii waliyoipata ya uhakika wa soko la kokoto kupitia sekta ya ujenzi ambapo shughuli za ujenzi zimechukua kasi kubwa kwa kuhakikisha kwamba wanazalisha kwa wingi na kwa wakati muafaka.

Afisa misitu asimamishwa kazi kwa tuhuma za kupiga wanawake.

0

Naibu waziri wa maliasili na utalii Constantine Kanyasu ameagiza kusimamishwa kazi pamoja na kuchukuliwa hatua afisa nyuki wa hifadhi ya msitu wa kisiwa cha kome wilayani sengerema mkoani mwanza Gerald Athanas anayetuhumiwa kuwapiga wanawake wanaokwenda kuokota  kuni kwenye hifadhi hiyo.

Kanyasu ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya afisa huyo ambapo pia ametangaza kuondoa zuio linalokataza makambi ya uvuvi yaliyoko ndani ya  hifadhi hiyo kuezekwa kwa mabati.

Wavuvi walioko ndani ya hifadhi ya kisiwa cha kome kilichoko kwenye ziwa victoria wilayani sengerema mkoani mwanza wanatarajia kuondokana na tatizo la makambi yao kuteketea kwa moto mara kwa mara baada ya serikali kuruhusu wavuvi kuezeka makambi yao kwa kutumia mabati.

Kero nyingine iliyowasilishwa kwa naibu waziri Kanyasu ni wanawake kutoruhusiwa kunyonyesha watoto pamoja na kukatazwa kusenya kuni kwenye hifadhi msitu wa kisiwa cha kome.

Naye kaimu meneja wa wakala wa huduma za misitu-Tfs kanda ziwa Thomas Moshi amesema kitendo cha baadhi ya watumishi kujichukulia sheria mkononi hakikubaliki na kuwaasa watumishi wengine kuacha mara moja.

Upanuzi wa bandari ya Kagunga mkoani Kigoma umefikia hatua nzuri

0

Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania   TPA imesema ipo katika hatua za mwisho  za kuanza awamu ya pili ya ujenzi na upanuzi wa bandari ya Kagunga iliyopo kaskazini mwa ziwa Tanganyika  mkoani  Kigoma.

Mkurugenzi mkuu wa Tpa mhandisi Deusdedit Kakoko upanuzi huo wa bandari ya Kagunga utasaidia kurahisisha  biashara kwa nchi za mwambao wa ziwa Tanganyika na kudhibiti mianya ya utoroshaji wa bidhaa.

Amesema kuwa kazi hiyo  ambayo  pia itahusisha na  uendelezaji wa ujenzi wa  soko la  ujirani mwema Kagunga  itaanza mwanzoni  mwa mwezi janury mwaka 2019.

Tayari gati na majengo ya kisasa vimekamilika, ishara ya kuelekea hatua za mwisho za ujenzi wa bandari hii inayoelezwa kuwa ya kipekee kutokana na kuwa na eneo kubwa lenye kina cha maji cha kutosha kwa ajili ya kuhudumia meli.