Waziri Mkuu aagiza ujenzi wa madarasa zaidi

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kila Halmashauri inajenga vyumba vya madarasa vya kutosha ili kuwawezesha wanafunzi waliofaulu kwenda kidato cha kwanza wanapata nafasi za kuendelea na masomo yao.

Agizo hilo amelitoa baada ya kusomewa taarifa ya miradi ya maendeleo ya mkoa wa Ruvuma na Mkuu wa mkoa huo Christina Mndeme.

Waziri Mkuu amesema watoto wote waliofaulu lazima wahakikishe wanasoma hivyo  waweke nguvu katika ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami barabara zote zinazounganisha mkoa kwa mkoa na wilaya kwa wilaya.

Rais Magufuli amjulia hali Dkt. Salim

0

Rais Dkt. John Magufuli leo tarehe 02 Januari, 2019 amemjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye anapatiwa matibabu Jijini Dar es Salaam baada ya kufanyiwa upasuaji.

Pamoja na kutoa pole kwa Dkt. Salim, Rais Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli ameongoza sala ya kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili apone haraka.

Dkt. Salim alilazwa hospitalini jana na hali yake inaendelea vizuri.

Waziri aagiza uchunguzi ujenzi wa barabara Tabora

0

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema wizara yake itafanya uchunguzi haraka iwezekanavyo kuhusu uwezo wa mhandisi mkazi na mhandisi ubora wa vifaa wanaosimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya kutoka Usesula hadi Komanga mkoani Tabora yenye urefu wa kilomita 108.

Waziri Kamwelwe ametoa kauli hiyo baada ya kukagua barabara hiyo wilayani Sikonge na kutoridhishwa na uwajibikaji wa wahandisi hao hali ambayo imesababisha mkandarasi anayejenga barabara hiyo kupeleka mapipa 3,770 ya lami  katika eneo la ujenzi ilhali ubora wake haujathibitishwa.

Amesema haridhishwi na uwezo wa makandarasi wazawa wanaosimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya kutoka Usesula hadi Komanga mkoani Tabora yenye urefu wa Kilomita 108.

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (Afdb) inatumia zaidi ya shilingi Bilioni 158.8 kujenga barabara hiyo.

Wakulima Zanzibar wasisitizwa kilimo cha mbogamboga

0

Waziri asiyekuwa na Wizara maalum Juma Ali Khatib amewataka wakulima wa visiwa vya Zanzibar kuhakikisha wanajikita katika sekta ya kilimo cha mboga mboga, matunda na viungo ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya visiwa hivyo.

Akizungumza mjini Unguja wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo la kutoa mafunzo ya kilimo biashara Waziri Khatib amesema umefika wakati kwa wakulima kujikita katika mapinduzi ya kilimo kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kufuata ushauri wa wataalum wa kilimo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Ahmad Kassim Haji amewataka vijana kuzitumia vizuri fursa za kilimo na kujiunga na jumuiya zinazoelimisha wakulima ili wajiajiri.

Wakulima Sumbawanga wahimiza kilimo cha kisasa

0

Baadhi ya wakulima mkoani Rukwa wameelezea umuhimu wa kuboresha miundombinu ya kilimo ili kuwawezesha kuendesha kilimo chenye tija kwa ajili ya ustawi wa jamii na shughuli za maendeleo.

Wakishiriki semina ya siku moja kuhusu matumizi ya teknolojia sahihi ya zana za kilimo iliyoandaliwa na Shirika la Taifa la Maendeleo – NDC wakulima hao wameshauri mtandao wa Benki ya Kilimo utumike kuwasaidia wakulima nchini.

Wamesema pamoja na ushauri wa wataalamu wa kilimo wanaopatikana katika maeneo mbalimbali nchini bado benki ya kilimo ina wajibu wa kuwawezesha wakulima katika jitihada zao za kuendesha kilimo cha kibiashara.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM wilaya ya Sumbawanga Said King’eng’ena aliyekuwa mgeni rasmi kwenye semina elekezi hiyo amesema matumizi ya zana za kisasa za kilimo ikiwa ni pamoja na matrekta ni miongoni mwa mbinu sahihi za kuboresha kilimo.

Imeelezwa kuwa katika mpango wa kuwezesha kilimo chenye tija matreka 105 yatapelekwa mkoani Rukwa katika awamu ya kwanza ya maboresho ya kilimo kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo –NDC.

Timu sita kumenyana ligi kuu

0

Timu ya Alliance fc ya Mwanza itateremka dimbani kuvaana na RUVU Shooting kwenye uwanja wa nyamagana mkoani Mwanza.

Biashara United ya Mara inawaalika wagonga nyundo wa jiji la Mbeya – Mbeya City fc kwenye uwanja wa kumbukumbu Karume mjini Musoma huku.

Nayo timu ya  Singida United wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa NamfuA mjini Singida wanawakaribisha Coastal Union ya Tanga huku Kagera sugar wakikipiga na Mbao fc.

Kwenye mchezo pekee uliochezwa hapo Januari Mosi ,timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (Kmc) imeibuka na ushindi wa mabao mawili kwa nunge dhidi ya kikosi cha African lyon katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam .

Kwa ushindi huo, Kmc inafikisha alama 25 baada ya kushuka dimbani mara 19 ambapo inapanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu kutoka nafasi ya tisa iliyokuwepo kabla ya mchezo wa January Mosi.

Nyota wa Liverpool wawania tuzo za wachezaji bora Afrika

0

Nyota wawili wa Liverpool Mohamed Salah raia wa Misri na Sadio Mane raia wa Senegal wameingia kwenye orodha ya wachezaji watatu wa mwisho wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa afrika zitakazotolewa wiki ijayo jijini dakar, Senegal.

Wachezaji wote wawili wamekuwa na kiwango kizuri mwaka uliopita wakiitumikia klabu yao ya Liverpool na timu zao za taifa ambapo Salah anatetea taji hilo kufuatia kuibuka kidedeaa mwaka jana.

Mwaka jana Salah alivunja rekodi ya upachikaji mabao kwenye ligi kuu ya Egland baada ya kupachika kimiani mabao 38 na kuifikisha klabu yake kwenye fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya.

Kwa upande wake Sadio Mane aliyeshika nafasi ya pili kwenye tuzo za mchezaji bora za mwaka jana, naye alikuwa na kiwango kizuri lakini akiwa nyuma ya salah kwenye takwimu za upachikaji mabao kwenye klabu yao huku wakiunda safu nzuri ya ushambuliaji wakiwa sambamba na mbrazil – roberto firmino.

Mchezaji anayekamilisha idadi ya wachezaji watatu kwenye kinyang’anyiro hicho ni mshambuliaji wa Arsenal na timu ya Taifa ya Gabon – Pierre Emerick-Aubameyang ambaye ni mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2015.

Nyota huyo aliifungia Arsenal mabao 10 msimu uliopita ukiwa ni msimu wake wa kwanza akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani ambapo kwa mwaka jana peke yake, ukiwa ni msimu wa mwaka 2018/2019 amefunga mabao 14.

Wizara ya afya yalaani vitendo vya ukatili kwa watoto nchini.

0

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani na kukemea vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kujitokeza nchini.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha wizara imesema kuwa vitendo hivyo vinafanywa na kuhusisha ndugu na walezi wa karibu wa watoto, hivyo kuzua hofu kubwa katika jamii kwani vitendo hivyo  vinaathiri malezi na makuzi ya awali ya watoto.

Taarifa hiyo imeelezea tukio liloripotiwa kuhusu mwalimu wa shule moja  ya msingi jijini Dodoma ambaye anatuhumiwa kumfungia mtoto mdogo ndani ya kabati kwa takribani miaezi mitano  na kusababisha afya ya mtoto huyo kudhohofika.

Pia Mwalimu huyo anatuhumiwa kumfanyia vitendo vya ukatili mama mzazi wa mtoto  huyo kwa kumpiga na kumsababishia maumivu mwilini yaliyosababisha  binti huyo na mtoto wake kulazwa.

Wizara inawapongeza wanajamii wote walioibua tukio hilo na kuwezesha Jeshi la Polisi kumkamata mtuhumiwa kwa ajili ya uchunguzi ili Sheria ichukue mkondo wake.

Matukio ya ukatili kwa watoto  yanarudisha nyuma jitihada za Serikali za kulinda na kuendeleza haki na ustawi wa watoto katika ngazi ya familia ambayo ndio kitovu cha jamii.

Hata hivyo wizara inatoa wito  kwa jamii  kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka makosa ya kisheria yanayoweza kutokea kwa kusambaza, kuchapisha na kupiga picha za watoto ambao ni wahanga wa ukatili na kuziweka wazi kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009.