Kesi ya mfanyabiashara ya dawa za kulevya yaanza kusikilizwa Marekani

0

Kesi ya kuhusika na biashara haramu ya dawa za kulevya na mauaji inayomkabili mfanyabiashara maarufu wa dawa hizo, pamoja na kiongozi wa genge la uhalifu El chapo au Gus Man, imeanza kusikilizwa nchini Marekani.

El chapo ambaye ni raia wa Mexico alipelekwa nchini Marekani ili kukabiliana na kesi yake, baada ya kuonekana kuwa ni mahabusu hatari, kwani mara kadhaa ametoroka gerezani alikokuwa akishikiliwa nchini Mexico.

Gus Man, mara kadhaa kwa msaada wa wafuasi wake amewatoroka polisi waliokuwa wakimtafuta au kutoroka gerezani hata katika magereza yenye ulinzi mkali.

Mara ya mwisho El chapo alitoroka kupitia handaki lililokuwa kwenye mahabusu hadi umbali mrefu nje ya gereza na kisha kuchukuliwa na helikopta.

Marekani na Uturuki zaanza mazungumzo kuhusu usalama

0

Ujumbe wa Idara ya Ulinzi nchini Marekani umewasili mjini Ankara nchini Uturuki kwa ajili ya mazungumzo ya usalama baina ya mataifa hayo mawili.

Wachunguzi wa siasa za Magharibi wamesema miongoni mwa mambo ambayo pande hizo mbili zinatarajia kujadiliana ni pamoja na kurejeshwa nchini Uturuki, mhubiri maarufu wa dini ya Kiislam Fatullah Gullan, anayeishi nchini Marekani.

Serikali ya Uturuki imekuwa ikimtuhumu mhubiri huyo wa dini, mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu, kuhusika na jaribio lililoshindwa la mapinduzi ya serikali ya Uturuki hata hivyo Gullan amekuwa akikanusha tuhuma hizo na kusema zimesababishwa kisiasa.

Nchi hizo mbili zinaangalia kama kuna uwezekano wa Marekani kumrejesha Gullan nchini Uturuki ili akabiliane na kesi ya uhaini inayomkabili.

Bilioni Tano zatengwa kwa ajili ya utafiti wa madini

0

Serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 8.5 kwa ajili ya utafiti wa kina wa Jiosayansi kuhusu rasilimali za madini ya dhahabu nchini ili wachimbaji wadogo waondokane na dhana ya kuchimba kwa kubahatisha.

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema hayo katika ufunguzi wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa eneo la Katente wilayani Bukombe mkoani Geita ambapo amesema pindi tafiti hizo zitakapokamilika watapewa wachimbaji wadogo sehemu mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa wachimbaji hao watakuwa na uhakika na shughuli zao za uchimbaji na namna watakavyoendelea kunufaika na rasilimali hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini nchini Mhandisi Sylvester Ghuliku amesema serikali iliwapa jukumu la kufanya utafiti pamoja na wakala wa jiolojia nchini katika vituo mbalimbali nchini ambapo Katente ni moja ya vituo hivyo.

Matokeo ya uchaguzi DRC kuchelewa

0

Tume ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo –DRC imesema matokeo ya uchaguzi mkuu uliomalizika nchini humo, huenda yakachelewa kutangazwa kwa vile, imeshindwa kupata matokeo ya uchaguzi kwa wakati.

Tume hiyo ya uchaguzi ya DRC imesema changamoto mbalimbali zimesababisha Tume hiyo kushindwa kupata kwa wakati matokeo ya uchaguzi huo wa Rais na wabunge kutoka katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Zoezi la kupiga kura huko DRC Jumapili iliyopita pia halikufanyika katika baadhi ya maeneo kwa sababu za kiusalama na maeneo hayo kukabiliwa na ugonjwa wa Ebola.

Ligi ya soka ya wanawake yaendelea nchini

0

Kivumbi cha ligi kuu ya wanawake Tanzania bara kinaendelea leo kwa michezo sita ya mzunguko wa pili kuunguruma kwenye viwanja tofauti kuanzia majira ya saa kumi jioni.

Kwenye dimba la Isamuhyo jijini Dar Es Salaam bingwa mtetezi JKT Queens wanashuka dimbani kuwaalika Tanzanite ya Arusha wakati Evergreen Queens wakiwa wenyeji wa Simba Queens mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Karume jijini Dar Es Salaam huku Yanga Princes wakisafiri hadi kwenye dimba la Nyamagana jijini Mwanza kumenyana na Marsh Queens.

Michezo mingine itawakutanisha Sisters ya Kigoma wakiwa kwenye dimba la Lake Tanganyika kuwakaribisha Baobab ya Dodoma wakati kwenye dimba la Mabatini pale Mlandizi – Kibaha mkoani Pwani wenyeji Mlandizi Queens watachuana na Alliance Girls huku Panama wakiwa nyumbani kwenye dimba la Samora mjini Iringa kumenyana na Mapinduzi Queens.

Mpaka sasa bingwa mtetezi wa ligi hiyo JKT Queens wanaongoza kwenye msimamo wakiwa na alama 3 na faida ya magoli 9 ya kufunga waliyopata kwenye mchezo wa kwanza wakifuatiwa na Alliance Girls, Mlandizi Queens, Marsh Queens, Simba Queens na Sisters ya Kigoma wenye alama tatu kila mmoja huku Evergreen ya Dar Es Salaam ikiburuza mkia.

Timu zaendelea kuchuana vikali ligi ya NBA

0

Katika ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani ya NBA hali imezidi kuwa mbaya kwa  timu ya Cleveland Cavaliers baada ya kutandikwa alama 117 kwa 92 na Miami Heat wakiwa nyumbani Quicken Loans Arena mjini Cleveland – Ohio.

Huu unakuwa mchezo wa 30 kwa Cavaliers kupoteza kwa msimu huu na kuweka rekodi ya matokeo mabaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni huku  Miami Heat wakipata ushindi wa 18 kwa msimu katika mchezo huo ambao mchezaji Josh Richardson amefunga alama 24.

Katika matokeo mengine timu ya Dalas Mavericks wameibuka na ushindi wa alama 112 kwa 84 dhidi ya Charlote Hornets huku Atlanta Hawaks wakishindwa kutamba mbele ya Washington Wizards na kula mweleka wa alama 114 kwa 98, New Orlean Pelicans wameambulia kipigo cha alama 126 kwa 121 kutoka kwa Brooklyn Nets na Orlando Magic wakiinyuka Chicago Bulls alama 112 kwa 84.

Timu ya Memphis Grizzilies ikiwa nyumbani wameshindwa kufurukuta mbele ya Detroit Piston na kula kichapo cha alama 101 kwa 94

Newcastle yafungwa katika uwanja wake wa nyumbani

0

Timu ya Newcastle imepoteza mchezo wa nane kati ya kumi na moja waliyocheza ya ligi ya Uingereza kwenye uwanja wake wa nyumbani kwa msimu baada ya kukubali kipigo cha mabao mawili kwa bila kutoka kwa Manchester United.

Mabao ya Romelu Lukaku aliyetokea benchi katika dakika ya 64 na Marcus Rashford katika dakika ya 80 yanaifanya Manchester United kushinda mchezo wa nne mfululizo kwa mara ya kwanza tangu mwezi April mwaka 2018.

Manchester United sasa imeshinda michezo 68 kati ya 100 waliyocheza mwezi Januari na kuwa timu pekee iliyoshinda michezo mingi kwenye ligi kuu ya England kwa mwezi huo.

Katika matokeo ya michezo mingine Bournamouth wamelazimishwa sare ya mabao matatu kwa matatu na Watford wakati Westham United wakibanwa na kutoka sare ya mabao mawili kwa mawili na Brighton huku Crystal Palace wakiinyuka Wolves mabao mawili kwa bila na Chelsea wakishindwa kufurukuta nyumbani na kutoka suluhu dhidi ya Southampton.

Baade unachezwa mchezo mmoja wa ligi ya kandanda ya England ambapo vinara wa ligi hiyo Liverpool wenye alama 54 wanasafiri kuwafuata Manchester City wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa na alama 47 mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Etihad kuanzia majira ya saa tano kamili za usiku.

Wafugaji mkoani Katavi wamaliza mgogoro na wakulima

0

Baadhi ya wafugaji mkoani Katavi wameanza kutekeleza mpango wa kumaliza migogoro baina yao na wakulima kwa kupanda nyasi kama malisho ya mifugo yao.

Afisa Mifugo wa mkoa wa Katavi, Zediheri Mhando amesema tayari serikali mkoani humo, kupitia sheria ya matumizi bora ya ardhi wametenga hekta zaidi ya laki moja ambayo wafugaji wamepatiwa bure maeneo ili kuendelea na upandaji wa malisho ya wafugaji hao.

Ameongeza kuwa zoezi la upandaji wa malisho katika kijiji cha Kapanga litaondoa migogoro baina yao na kwamba sheria ya matumizi bora ya ardhi imezingatiwa.