Necta yawafutia matokeo wanafunzi 47 wa kidato cha pili

0

Baraza la Mitihani nchini -Necta limewafutia matokeo jumla ya wanafunzi 47 wa Kidato cha Pili na 151 wa darasa la nne kwa kufanya udanganyifu na kuandika lugha ya matusi katika mitahani yao.

Akitangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa Kidato cha pili na Darasa la nne kwa 2018 Katibu mtendaji wa necta Dokta Charles Msonde Jijini Dodoma amesema kiwango cha ufaulu kimeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2017.

Dokta Msonde kwanza akaweka wazi kiwango cha ufaulu katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha Pili kwa mwaka 2018.

Pia akaitaja mikoa mikoa iliyofanya vizuri na mikoa iliyofanya vibaya katika Mitihani ya kidato cha pili kitaifa.

Katika matokeo ya Kidato cha pili wasichana wameongoza kwa ufaulu ambapo katika kumi bora wasichana wako saba kati ya kumi huku nafasi ya kwanza hadi ya sita kitaifa ikishikiliwa na wasichana.

Serikali yakerwa na watu wanaofanya vitendo vya utoroshaji madini

0

Naibu  Waziri wa Madini  Stanslaus  Nyongo amesema vitendo vya utoroshaji wa madini nje ya nchi vinavyofanywa na baadhi  ya wachimbaji wadogo vimesababisha serikali kukosa mapato.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi endelevu wa rasilimali madini kwa wachimbaji wadogo wa Bati Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera Naibu  Waziri  Nyongo amesema hali hiyo imesababisha wingi wa wachimbaji kutolingana na mchango wao katika pato la taifa.

Katika mafunzo hayo inaelezwa kuwa idadi ya wachimbaji wadogo wa madini ni Asilimia tisini na sita ya wachimba madini wote nchini lakini huchangia Asilimia nne tu katika pato la taifa kutokana na sababu kadhaa ikiwemo baadhi yao kutorosha madini.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya bati wanaelezea matarajio yao baada ya mafunzo hayo kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Madini  kwa kushirikiana na Shirika la Madini nchini -Stamico pamoja na Wakala wa Jiolojia.

Waziri Mkuu Majaliwa aridhishwa na kazi ya ujenzi wa barabara ya Mbinga

0

Waziri mkuu kassim majaliwa  ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa barabara ya lami kutoka Mbinga kwenda Mbamba Bay yenye urefu wa kilomita 69 itakayogharimu sh. bilioni 129.3 na kuagiza uongozi wa wakala wa barabara tanzania (tanroads) kusimamia vizuri mradi huo.

Waziri mkuu  majaliwa amesema hayo mkoani Ruvuma wakati akikagua utekelezaji wa mradi huo wa barabara inayojengwa na kampuni ya Chico ya nchini China na kusema kuwa hatua waliyoifikia inaonyesha barabara hiyo inayotarajiwa kukamilika januari 2021 itakamilika mapema zaidi.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi na mkoa kwa ujumla na kukuza  sekta ya utalii na uvuvi katika mkoa huo.

Rais magufuli ashuhudia utiaji saini mkataba wa uuzaji wa chakula

0

Rais dkt. John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula (Nfra) na shirika la chakula duniani (Wfp) uliofanyika ikulu jijini Dar es salaam.

Mkataba huo umetiwa saini na kaimu mtendaji mkuu wa Nfra Vumilia Zikankuba na mwakilishi na mkurugenzi mkazi wa Wfp hapa nchini Michael Danford, ambapo Wfp itanunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 21 kutoka Nfra.

Danford amesema mahindi hayo ni sehemu ya tani laki 1 na 60 elfu  za chakula zenye thamani ya shilingi bilioni 132.2 zilizonunuliwa na Wfp nchini tanzania katika mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la kutoka shilingi bilioni 63.6 zilizotumika kununua chakula mwaka 2017.

Danford amebainisha Wfp limeamua kuwa mnunuzi mkubwa wa mazao ya chakula nchini tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na nchi jirani zenye matatizo ya chakula.

Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Jeshi la Polisi, Wakala wa barabara Tanzania (Tanroads), shirika la viwango Tanzania (tbs), Mamlaka ya mapato Tanzania (tra), Shirika la Reli Tanzania (trc) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (tpa) kuhakikishia wanaondoa urasimu na kuharakisha ununuzi wa mazao yanayonunuliwa na Wfp (ili wakulima wa wanufaike na fursa hiyo.

Mkandarasi wa wa majengo ya wizara ya Mifugo atakiwa kukamilisha ujenzi huo

0

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, amemtaka mkandarasi Suma Jkt anayejenga jengo la wizara hiyo katika mji wa serikali jijini Dodoma, kuhakikisha anaendelea kuwalipa wafanyakazi wanaojenga jengo hilo kwa wakati pamoja na kuhakikisha ubora wa jengo hilo unaendana na thamani hali pesa.

Ulega amesema hayo leo mara baada ya kufika katika mji huo uliopo kata ya Mtumba, kwa ajili ya kufanya tathmini ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la awali la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuonesha kuridhishwa na kasi ya ujenzi inavyoendelea na kumtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

“Unamlipa mtu kabla jasho lake halijakauka palepale unakuwa tayari umeshampa ndiyo dini inavyosema, ni jambo jema sana maana hawa mafundi wanasema wanalipwa kwa wakati”alisema Waziri  Ulega.

Waziri amefafanua kuwa siyo jambo jema endapo kutatokea taarifa mara baada ya kumalizika kwa mradi wa ujenzi wa jengo la wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuwa wafanyakazi waliokuwa wakijenga jengo hilo wanamdai mkandarasi ilhali wizara imemlipa pesa zote mkandarasi huyo suma Jkt ili aweze kufanya kazi kwa wakati.

Kwa upande wake mkandarasi msimamizi wa Suma Jkt Injinia David Pallangyo amesema ujenzi wa jengo hilo unaenda kwa kufuata mpangilio wa ratiba wa shughuli kwa kila tarehe na kwamba hadi kufikia mwisho wa mwezi januari mwaka huu jengo litakuwa katika hatua za mwisho.

ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ililenga  kufanya tathmini ya ujenzi wa jengo lao ambapo  ni mwendelezo wa ziara za viongozi wa juu wa wizara.

Watu 12 washikiliwa kwa tuhuma za mauaji Morogoro

0

Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu 12 wanaotuhumiwa kuwa majambazi sugu wakiwemo waliohusika na mauaji ya Afisa Tarafa ya Lupilo wilayani Ulanga.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Kamanda wa Jeshi hilo Wilbroad Mutafungwa amesema watuhumiwa hao walikamatwa  katika msako maalumu wa kukabiliana na uhalifu katika wilaya zote za mkoa wa Morogoro.

Aidha Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi baada ya hivi karibuni kuibuka mauaji yanayosababishwa na wivu wa mapenzi.

Lindi yatakiwa kuhakiki wanufaika wa TASAF

0

Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi ameagiza Halmashauri za mkoa wa Lindi kuhakiki wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF ili kuona endapo wanufaika wa mpango huo ndio wale wenye sifa zinazotakiwa.

Zambi ameyasema hayo mjini Nachingwea alipokuwa akizungumza na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini, baada ya kubaini miongoni mwao wengine hawana vigezo vya kunufaika na mpango huo.

Amesema wapo wazee ambao wana watoto wenye uwezo lakini watoto wao wanawakimbia wakikwepa wajibu wao na kuiachia serikali.

Mkuu wa mkoa wa Lindi amewataka wananchi kujua kuwa umaskini si sifa nzuri na kumtaka mratibu wa TASAF kumpatie taarifa ya fedha za Mfuko huo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kituo cha Afya Kifula chaombewa kupandishwa hadhi kuwa Hospitali

0

Naibu Spika wa bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuna umuhimu wa serikali kukipandisha hadhi ya kuwa hospitali kamili kituo cha afya Kifula cha wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akikabidhi gari ya kubeba wagonjwa pamoja na kuzindua wodi za wagonjwa zilizojengwa na mfuko wa maendeleo ya watu wa Ugweno kwa kushirikiana na taasisi ya Tulia Trust.

Majengo hayo yamefanyiwa ukarabati, ujenzi wa wodi mbili, vifaa vya kisasa na gari la kubebea wagonjwa kwa kituo cha afya Kifula kilichopo wilayani Mwanga.

“Kituo hiki ni faraja kwa wakazi wanaoishi katika tarafa ya Ugweno na maeneo ya jirani kwani wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya” alisema Naibu Spika Dkt. Tulia.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema kwa sasa watapata huduma ya afya karibu na hivyo kupunguza adha ya kwenda Hospitali ya Usangi kufuata huduma.