Kamati ya bunge kumhoji CAG

0

Spika wa bunge Job Ndugai amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Assad kufika katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge tarehe 21 Januari ili kutoa ufafanuzi kuhusu kauli yake anayodaiwa kuitoa katika mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini Marekani.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inayodaiwa kulidhalilisha bunge.

Pia ametoa ushauri kwa wananchi na taasisi mbalimbali za serikali kuwa ni ustaarabu na kutoisema vibaya nchi, nje ya nchi.

Halikadhalika Spika Ndugai amemtaka mbunge wa Kawe Halima Mdee kufika katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya bunge tarehe 22 Januari ili kuthibitisha maneno anayodaiwa kusema katika mitandao ya kijamii kuhusu bunge.

Jaribio la mapinduzi Gabon ladhibitiwa

0

Serikali ya Gabon imesema imerejesha hali ya utulivu nchini humo, baada ya kikundi cha askari waasi kufanya jaribio la mapinduzi, katika kipindi hiki ambapo Rais wa nchi hiyo Ali Bongo yuko nchini Morocco kwa matibabu.

Msemaji wa serikali ya Gabon amesema watu wanne wanaotuhumiwa kufanya jaribio hilo wamekamatwa.

Mapema leo baadhi ya askari walidai kufanya jaribio la mapinduzi nchini Gabon kwa lengo la kurejesha demokrasia nchini humo ambapo magari yenye silaha yalionekana katika mitaa ya mji mkuu wa Gabon, Libreville.

Timu ya Los Angeles yafungwa katika ligi ya kikapu Marekani

0

Ligi ya kulipwa ya mpira wa kikapu nchini Marekani ya Nba imendelea na kuchezwa michezo saba.

Los Angeles Lakers wakiwa ugenini wamekiona cha moto baada ya kunyukwa alama 108 kwa 86 na Minasota Timberwolves ambao wamepata ushindi wa 19 msimu huu wakati Lakers wakipoteza mchezo wa 19.

Katika matokeo mengine Miami Heat wamenyukwa alama 106 kwa 82 na Atlanta Hawks wakati Washngton Wizards wakiinyuka Oklahoma City Thunder alama 116 kwa 98 na Charlote Hornets wameilaza Phonix Suns alama 119 kwa 113.

Los Angeles Clippers wameshinda  nyumbani kwa kuinyuka Orlando Magic alama 106 kwa 96 wakati Indiana Pecers wakishindwa kuhimili vishindo vya Toronto Raptors na kula mweleka wa alama 121 kwa 105 huku Brooklyn Nets wakiinyuka Chicago Bulls Al.

Hali ya utulivu kurejea nchini Brazil

0

Serikali ya Brazil imepeleka askari wake katika mji wa Fortaleza ulikoko kaskazini mwa nchi hiyo kurejesha hali ya utulivu baada ya vitendo vya uhalifu kuongezeka kwenye mji huo katika siku za hivi karibuni.

Matukio yapatayo themanini yameripotiwa katika jimbo la Sariya katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na vitendo vya ujambazi, unyang’anyi wa kutumia nguvu na mashambulio dhidi ya watu kwa kutumia kemikali zenye athari kwa maisha ya binadamu.

Magenge ya wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya yamekuwa yakihusika na matukio hayo ya uhalifu kuanzia kwenye magereza ya nchi hiyo hadi mitaani.

Serikali mpya iliyoingia madarakani, iliahidi kuwachukulia hatua kali watu wote wanaohusika na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Pande mbili zinagombana nchini Yemen kupataishwa

0

Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa nchini Yemen, amerejea nchini humo kujaribu kuzisihi pande zinazohusika na mapigano nchini Yemen kutekeleza mkataba wa kusimamisha mapigano zilizotiliana saini nchini Sweden.

Kila upande nchini Yemen unaohusika na mapigano ya nchi hiyo, umekuwa ukuishutumu upande mwingine kuwa chanzo cha kukiuka mkataba wa amani ya kusimamisha mapigano nchini humo.

Wananchi ya Yemen wanataka uwanja wa ndege wa Sanaa ambao kwa sasa umefungwa kutokana na mapigano ufunguliwe.

Baadhi ya wananchi wa Yemen ambao ni wagonjwa na wanahitaji matibabu ya haraka nje ya nchi wanasema, wanashindwa kusafiri, kwenda kupata matibabu nje ya nchi kwa vile uwanja huo wa ndege bado umefungwa.

Matokeo ya uchaguzi Drc Congo bado kutangazwa

0

Upande wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo -Drc-umekuwa ukihoji ni kwa nini matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo yanaendelea kuchelewa kutangazwa.

Matokeo ya uchaguzi katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo yalikuwa yatangazwa Decemba 6, lakini tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imesema huenda matokeo hayo yakatangazwa wiki ijayo.

Hadi sasa nusu ya kura zote zilizopigwa wakati wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo tayari zimehesabiwa.

Upande wa upinzani huko Drc- una wasiwasi kuwa serikali ya nchi hiyo inapanga udanganyifu wa matokeo ya uchaguzi ndio maana matokeo hayo yamekuwa yakichelewa kutangazwa.

serikali ya Drc imekanusha tuhuma hizo za upinzani na kusema kuwa nchi hiyo ni kubwa na baadhi ya maeneo yako pembezoni, hiyo zoezi la kukusanya matokeo halikuwa rahisi.

hata hivyo katika baadhi ya maeneo wapinzani wameshindwa kuonyesha uvumilivu na kushiriki katika maandamano ya kupinga kuchelewa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais, hali iliyosababisha vyombo vya usalama kutumia nguvu kutawanya maandamano hayo.

Askari mmoja afariki baada ya kulipukiwa na bomu

0

Askari polisi mmoja amekufa mjini Cairo nchini Misri alipokuwa akijaribu kutegua bomu lililokuwa limetegwa karibu na kanisa moja kwenye mji huo.

Askari wengine wawili waliokuwa wakisaidia na askari polisi huyo kutegua bomu hilo wamejeruhiwa, baada ya kushindwa kuliwahi bomu hilo na kisha kulipuka.

Bomu hilo lilikuwa limetegwa siku mbili kabla ya wakristo wa madhehebu ya Coptic nchini humo kusherehekea sikukuu ya Krismas.

Mara kadhaa yametokea mashambulio katika makanisa ya kikristo nchini Misri na kusababisha maafa na hivi sasa Serikali ya nchi hiyo inaendelea kuimarisha ulinzi ili kudhibiti milipuko kama hiyo inayolenga mikusanyiko ya watu.

Mkoa wa Dar es salaam watakiwa kuongeza kasi kukusanya kodi

0

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amewataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa  manispaa na wakuu wa mamlaka ya mapato nchini kuangalia  uwezekano wa kuongeza makusanyo kutoka asilimia kumi na saba  hadi asilimia thelathini katika kipindi hiki cha mwaka 2019.

Akizungumza na viongozi hao katika kikao maalum cha utendaji ambacho kilikuwa kinapanga mkakati wa kuongeza  makusanyo ya mapato katika mkoa wa Dar es salaam ,Makonda  amesema lazima viongozi hao watambue fursa  nyingine za ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha yanaleta tija katika ustawi wa maendeleo ya mkoa wa Dar es salaam.

Pia amewataka viongozi hao kuwawezesha vijana kutambua fursa za ajira ambazo zitawawezesha vijana hao  kuondokana na umasikini.

Kikao hicho tendaji cha kupanga mkakati wa utafutaji wa fursa mbalimbali za makusanyajo wa mapato kimewashirikisha  wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wakuu wa halmashauri,vikosi vya ulinzi na usalama ,maafisa kutoka idara mbalimbali na maafisa kutoka mamlaka ya mapato nchini –Tra.