Wahandisi wa Maji Ruvuma na Mbeya wasimamishwa kazi

0

Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kumsimamisha kazi mara Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini, Vivian Mdolwa kwa tuhuma za ubadhilifu wa miradi ya maji aliyoifanya akiwa Mhandisi wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri Aweso pia amemsimamisha kazi Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Ruvuma, Genes kimaro kwa kushindwa kusimamia miradi hiyo ya maji na kusababisha wananchi kuendelea kupata shida ya huduma ya maji.

Wananchi wa Kata ya Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga  wamekosa  maji kwa muda mrefu  licha ya miradi ya maji mitatu katika kata hiyo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 840 kukamilika.

Mchezaji wa Azam ajiunga na timu ya Ismailia

0

Mshambuliaji wa timu ya Azam Fc, Yahya Zayed amejiunga na klabu ya Ismailia ya Misri kwa mkataba wa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Azam Fc, Jaffar Idd, amesema kuwa Zayed amejiunga na Ismailia bila ya kufanya majaribio zaidi ya kufanyiwa tu vipimo vya afya .

Zayed ambaye ni mchezaji  wa kimataifa wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 20 amesaini mkataba huo kuitumikia Ismaili ambayo ni moja kati ya Klabu kongwe nchini Misri, na kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kucheza ligi kuu ya Misri, baada ya kiungo Himid Mao anayechezea Petrojet.

Nyota huyo pia anaungana na wachezaji wengine kutoka Namibia na Nigeria waliosajiliwa hivi karibuni kuboresha kikosi cha Ismailia  katika michuano mbalimbali ikiwemo hatua ya makundi ya ligi ya Mabingwa Barani Afrika ambapo wamepangwa katika kundi che.

Yanga yaondolewa kombe la Mapinduzi

0

Timu ya Yanga imetupwa nje ya michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja na timu ya Malindi, katika mchezo wa Kundi Be uliochezwa Januari 7 katika uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Bao la Yanga lilifungwa na mshambuliaji wake Matheo Anthony, huku yale ya Malindi yakipachikwa wavuni na Abdulsamad Kassim na Juma Hamad.

Kwa matokeo hayo, Malindi inafikisha alama saba baada ya kucheza michezo mitatu, ikishinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja ,huku Yanga ikibaki na alama zake tatu baada ya kucheza michezo mitatu, ikishinda mchezo mmoja na kupoteza michezo miwili.

Malindi inaungana na Azam fc iliyoshinda mabao mawili kwa moja mchezo wake dhidi ya Kvz na kufuzu hatua ya nusu fainali kutoka kundi Be, wakiungana na Simba kutoka kundi Aa, huku ikisubiriwa timu moja kutoka kundi Aa, kukamilisha idadi ya timu nne katika hatua hiyo ya nusu fainali.

Michuano hiyo ya 13 ya Kombe la Mapinduzi inaendelea kwa kuchezwa michezo mingine miwili ambapo Kmkm watacheza na chipukizi saa kumi na robo alasiri huku simba wakishuka dimbani saa mbili na robo usiku dhidi ya Mlandege.

Liverpool yatolewa kombe la Fa

0

Baada ya timu ya Liverool kutolewa katika mzunguko huo wa tatu wa michuano ya FA,  droo ya mzunguko wa nne imeshapangwa ambapo Arsenal wataanzia nyumbani katika dimba lao la Emirates kuwakabili Manchester United.

Vijana hao wa The Gunners wametwaa mara 13 ubingwa wa kombe la FA, huku Manchester United wakitwaa taji hilo mara 12.

Michezo mingine ambayo inatolewa macho na wapenzi wa soka ni Tottenham hotspur, watakaokuwa ugenini kuikabili Crystal Palace, Manchester City   wao watakuwa nyumbani dhidi ya  Burnley  wakati Chelsea  watakuwa katika dimba lao la Stamford Bridge jijini London, kuwakabili Sheffield Wednesday baada ya timu hizo kupambana na kupatika mshindi siku ya jumatano.

TRA watakiwa kuwajengea wafanyabiashara tabia ya ulipaji kodi kwa hiari

0

Mkuu wa Mkoa wa  Mbeya, Albert Chalamila amewataka wafanyabiashara mkoani humo kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari na kuwatahadharisha baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato nchini  -TRA wanaotumia mianya ya kujinufaisha kwa kuchukua fedha nje ya utaratibu  wa serikali kuacha mara moja.

Chalamila ametoa rai hiyo Mkoani Mbeya baada ya  kuzungumza na baadhi ya wawekezaji na wafanyabiashara kuhusiana na changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.

Amesema moja ya mikakati ya uongozi wa Mkoa wa Mbeya ni  kuhakikisha  wawekezaji wanajengewa uwezo na mazingira mazuri ili  waweze kulipa kodi.

Ameongeza kuwa lazima kuwepo na mahusiano ya moja kwa moja   kati ya mfanyabiashara na serikali yatakayowezesha kwa pamoja kufikia malengo ya kuinua uchumi nchini.

Serikali yaendelea kutathmini mishahara bora

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea na kazi ya kukamilisha tathmini katika Wizara na Taasisi ili kupanga vizuri mishahara na motisha kwa watumishi wa umma baada ya kumalizika kwa zoezi la kuwaondoa watumishi hewa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jijini Dodoma baada ya kupokea maandamano ya wafanyakazi yaliyofanyika kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kurudisha kikokotoo cha zamani katika mafao ya wastaafu.

“Serikali imeweka azma ya kuongeza motisha kwa wafanyakazi wote nchini ikiwemo na ulipaji wa madeni ya wafanyakazi”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Shule kuunda madawati ya ulinzi wa mtoto

0

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu amewataka wazee wanaoendeleza mila ya ukeketaji kutafuta njia mbadala ya kuwafundisha vijana bila kuwaumiza au kuathiri miili yao.

Akizungumza mkoani Mara wakati wa ufungaji kambi okozi mabinti zaidi ya 400 waliokimbia tohara mwaka 2018 na vijana 29 waliofanyiwa tohara salama katika kijiji cha Masanga wilayani Tarime, Dkt. Jingu amesema zipo njia za kuendeleza mila kwa kumfundisha binti mambo ya msingi ikiwemo elimu dunia.

Ameelezea mikakati ya serikali kulinda haki ya mama na mtoto ifikapo mwaka 2020 huku akitumia fursa hiyo kuwakumbusha walimu katika shule zote nchini kuunda madawati ya ulinzi wa mtoto.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la TGNP Lilian Liundi amesema ni muhimu jamii ikawa na usawa ili kufikia uchumi wa viwanda.

Maafisa uhamiaji mipakani waaswa kutowanyanyasa wananchi

0

Serikali imewataka Maafisa Uhamiaji katika mikoa ya pembezoni  mwa nchi kuacha kuwanyanyasa wananchi kwa kutumia muonekano wao wa maumbile na kuwalazimisha kuimba wimbo wa Taifa kama vigezo katika kubaini uraia wao.

Akizungumza na wananchi wilayani Ngara mkoani Kagera, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amewataka maafisa uhamiaji hao kutumia utaalam wao kuondoa kero na malalamiko dhidi yao.

Waziri Lugola ametoa mwezi mmoja kwa Halmashauri ya wilaya ya Ngara kuhakikisha inanunua vifaa vya kujikinga na moto katika taasisi zilizo chini yake ikiwemo shule na vituo vya afya.