Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula watoa tamko

0

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Nchini -NFRA, Vumilia Zikankuba amesema kamwe hatanunua mahindi ya wakulima yasiyo na ubora.

Zikankuba ametoa kauli hiyo mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mathew Mtigumwe ambaye amekutana na wakulima wa Mkoa wa Katavi ambao  wanalalamika kuwa mahindi yao hayajanunuliwa kutokana na kukosa ubora.

Jumla ya Tani 2500 za mahindi za wakulima zimeshindwa kununuliwa kutokana na madai ya mahindi yao kukosa ubora unaotakiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula nchini.

Wagonjwa 45 kufanyiwa upasuaji wa moyo

0

Jumla ya wagonjwa 45 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo wa bila kufungua  kifua katika kambi maalum ya matibabu ya moyo kuanzia Tarehe 7 hadi 18 mwezi huu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete       -JKCI.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano cha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imesema kuwa upasuaji huo unafanywa  kupitia madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na Madaktari Afrika na Shirika la Cardio Start wote kutoka nchini Marekani.

Matibabu yanayofanyika  katika kambi hiyo ni upasuaji wa kufungua kifua bila kufungua kifua ambao unafanyika kupitia tundu dogo kwenye paja kwa wagonjwa kuzibuliwa mishipa ya moyo iliyoziba yaani                  -Percutaneous Coronary Intervention na kuwekewa vifaa  vinavyosaidia kurekebisha mapigo ya moyo ambavyo ni Permanent Pacemaker na High Powered Devices.

Wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ambayo ni valve, mishipa ya moyo iliyoziba, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matibabu kwa watu wazima waliozaliwa na matatizo ya moyo na wale wenye matatizo ya moyo yaliyotokana  na ugonjwa wa Kisukari.

Kambi hii inaenda  sambamba na utoaji wa elimu kwa madaktari na wauguzi pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa wageni na wataalamu kutoka nchini Marekani.

Hii ni kambi ya kwanza ya matibabu ya moyo tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019 na ni mara ya kwanza kwa Shirika Cardio Start  kuja hapa nchini.

Watu watatu wanashikiliwa polisi kwa tuhuma za ujangili

0

Jeshi la Polisi Mkoani Iringa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika katika matukio ya ujangili wa tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Mkoani Iringa.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Juma Bwire amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia taarifa za wasamaria wema ambapo wamekutwa na bunduki mbili aina ya gobore zinazosadikiwa kutumika kwenye uwindaji huo haramu.

Kukamatwa kwa watuhumiwa watatu wa ujangili kumekuja siku chache baada ya kuripotiwa kurejea tena kwa kasi vitendo vya ujangili wa tembo katika Hifadhi ya Ruaha ambavyo vilikuwa vimepungua kwa kiasi kikubwa.

Katika kipindi cha mwaka jana inakadiriwa kuwa tembo sita walikutwa wameuawa kwenye eneo la nje ya Hifadhi ya Ruaha hali iliyoashiria kuwa wawindaji haramu wameanza tena ujangili wa tembo.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limewatia mabaroni watuhumiwa watano akiwemo dereva wa lori la kusafirisha mafuta kwa wizi wa Lita Elfu 38 za mafuta ya Dizeli yaliyokuwa yanasafirishwa kwenda nchini Zambia.

Kim Jong Un awasili nchini China

0

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim jong Un amewasili Nchini China kwa ziara ya siku nne .

Akiwasili mjini Beijing kwa kutumia usafiri wa treni Kim amepokelewa na vingozi mbalimbali wa serikali ya china na baadae anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake  Rais Xi Jinping katika ikulu ya nchi hiyo kwa mazungumzo.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini ameianza ziara hiyo leo huku ikiwa ni kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, ambapo anatimiza umri wa miaka 35.

Ziara hiyo inafanyika huku maandalizi ya mkutano wa kilele kati ya kim na rais Donald Trump wa marekani yakiendelea.

Habari zinaeleza kuwa  maafisa wa Marekani na Korea Kaskazini wamekutana Vietnam kujadiliana kuhusu eneo utakapofanyika mkutano huo kati ya viongozi hao wawili.

Rais wa Benki ya dunia aatangaza kujiuzuru

0

Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim ametangaza kuwa atajiuzuru mwezi ujao, ikiwa ni miaka mitatu kabla ya muhula wake kumalizika mwaka 2022.

 Kim ambaye anajiunga na kampuni binafsi inayoangazia uwekezaji katika mataifa yanayoendelea, amesema imekuwa ni heshima kubwa kwake kuiongoza taasisi hiyo muhimu.

Afisa mkuu wa benki ya dunia, Kristalina Georgieva, atachukua nafasi ya rais wa mpito baada ya kim kuondoka Februari mosi.

Kim alianza kipindi chake cha pili kama rais wa benki ya dunia, Julai, 2017.

Serikali ya Ufaransa yaonya waandamanaji

0

Serikali ya Ufaransa imetangaza sheria kali dhidi ya waandamanaji  ikiwemo kupiga marufuku maandamano yasiyo halali na kuweka vikwazo kwa waandamanaji .

Waziri Mkuu wa Ufaransa, Edouard Philippe amesema hatua hiyoni katika kukabiliana na maandamano yasiyo na vibali kutoka Serikalini.

Serikali ya Ufaransa pia ametangaza mpango wa kuwapiga marufuku wanaosababisha fujo kushiriki katika maandamano.

Hatua hiyo inakuja baada ya maandamano yajulikanayo ”vizibao vya njano” ambayo yamedumu kwa wiki nane sasa na kusababisha ghasia na majibizano kati ya polisi na waandamanaji kwenye mji mkuu wa Paris pamoja na miji mingine ya Ufaransa.

Philippe amesema askari 80,000 watatawanywa nchi nzima katika maandamano yaliyopangwa kufanyika jumamosi ijayo.

Wakazi wa Katavi walalamikia barabara zao kujengwa chini ya kiwango

0


Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Makanyagio Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi wameuomba uongozi wa Mkoa huo kuingilia kati ujenzi wa miundombinu ya barabara inayodaiwa kujengwa chini ya kiwango.

Akizungumza na Tbc, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Makanyagio, Simon Misonge amesema hali ya mtaa huo si nzuri kwa sasa kutokana na barabara kuzunguka mtaa huo kusombwa na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha kutokana na kukosekana kwa mitaro madhubuti ya kuhimili maji.

Kila kona ya Mtaa wa Makanyagio umezungukwa na miundombinu ya barabara  na mitaro ambayo ni kero kwa wananchi.

Kwa upande wake katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi, Jackson Lema ameelekeza lawama kwa wakala wa barabara vijijini na mjini -Tarura na kuitaka kujitathimini katika kipindi hiki cha mvua ambacho barabara nyingi Mkoani Katavi hazipitiki.

Rais Magufuli afanya mabadiliko madogo baraza la mawaziri

0

Rais Dkt. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri, kuteua makatibu wakuu, Naibu Katibu Mkuu, Balozi na Katibu Tawala wa mkoa.

Akitangaza mabadiliko hayo Ikulu jijini Dar Es Salaam Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. John Kijazi amesema walioteuliwa ni pamoja na Angela Kairuki ambaye amekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Doto Biteko amekuwa Waziri wa Madini ambapo Stanslous Nyongo anaendelea kuwa Naibu Waziri wa Madini.

Katika uteuzi huo Rais Magufuli amemteua Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu –TAMISEMI kuchukua nafasi ya Musa Iyombe aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Zainab Chaula anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuchukua nafasi ya Dkt. Mpoki Ulisubisya aliyeteuliwa kuwa Balozi. Dkt. Ulisubisya atapangia baadae kituo cha kazi.Dorothy Mwaluko ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uwekezaji,Elius  Mwakalinga anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi.

Kwa upande wa Naibu Katibu wakuu walioteuliwa ni pamoja na Dorothy Gwajima anayekwenda TAMISEMI, Dkt. Francis Michael anayekuwa Naibu Katibu Mkuu Utumishi na nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Ulinzi ikiwa imefutwa rasmi.

Aidha Profesa Faustine Kamuzora ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera.