Ujio wa ndege mpya kuchochea thamani za bidhaa nchini

0

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela amesema ujio wa Ndege aina ya Airbus 220-300 ya Shirika la Ndege nchini -Atcl utaongeza mnyonyoro wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa katika sekta mbalimbali hapa nchini.


Mongela ameyasema hayo Jijini Mwamza wakati ndege hiyo ilipoanza safari zake rasmi hapa nchini kwa kusafiri kutoka Dar es salaam kwenda Mwanza na kusema kuwa ndege hiyo itachochea uchumi na ajira kwa watanzania.
 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amesema miundombinu ndio njia kuu katika kuutangaza utalii na kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano Atcl, Josephat Kangirwa amesema kuwa ndege hiyo pia itafanya safari za kwenda India, China na Thailand.

Ujumbe wa Afghanistan wawasili Pakistan kwa ajili ya mazungumzo

0

Ujumbe wa serikali ya Afghanistan umewasili nchini Pakistan ukijaribu kuishawishi serikali ya nchi hiyo kuwashawishi wapiganaji wa kikundi cha Taleban wa nchini Afghanistan kukubaliana na mpango wa amani wa nchi yao.

Kumekuwa na wapiganaji wa kikundi cha Taleban katika nchi za Pakistan na nchini Afghanistan, wote wakipigana dhidi ya serikali ya nchi zao.

Serikali ya Afghanistan kwa upande wake ilifanikiwa kufikia mkataba nawapiganaji wa Taleban nchini humo ili kurejesha amani.

Serikali ya Afghanistan imeiomba serikali ya Pakistan kuwashawishi wapiganaji wa Taleban wa Afghanistan kuitambua serikali ya nchi yao iliyoko madarakani na hatimaye pande hizo kuweza kukaa katika meza ya mazungumzo.

Rais wa Sudan kuhutubia raia wake

0

Rais Omar Al Bashir wa Sudan muda wowote kuanzia sasa anatarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara mjini Khartoum, akijaribu kuwatulinza waandamanaji ambao wamekuwa wakiandamana kupinga Serikali yake.

Watu hao wamekuwa wakimshinikiza kiongozi huyo kuachia madaraka kwa madai ya kuchoshwa na sera zake na kufanya maisha yao kuendelea kuwa magumu.

Bashir amekataa mpango wa kuachia madaraka na kusema kuwa mdororo wa uchumi nchini humo kwa kiasi kikubwa na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikiwekewa na jumuiya ya kimataifa.

Maandamano ya kupinga serikali yalianza nchini Sudan, mara baada ya bei ya mkate kuongezeka na bidhaa zingine zinazotokana na mafuta ya magari.

 Hata hivyo maandamano ya kudai punguzo la bei ya mkate walibadilika na kuanza kumshinikiza Bashir kuondoka madarakani.

Rais Magufuli ataka matumizi sahihi ya ofisi za umma

0

Rais John Magufuli amewataka watendaji serikalini kuacha kufanya ofisi za umma kama mali zao binafsi bali ziwe mali ya watanzania na kulitumikia taifa kwa ujumla.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar Es Salaam baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua Januari 8 ambapo amesema siku za karibuni umezuka mtindo kwa watendaji wa serikali kufanya ofisi za umma kama za kwao na kuwataka kuacha mara moja tabia hiyo.

Amewataka watendaji kutumikia wananchi kwa haki na kufuata sheria za nchi kwa kufanya maamuzi yenye tija na si kumuonea mtu.

“Naomba watendaji wote msichukue  ofisi za umma kama mali zenu, bali ziwe mali kwa watanzania na mkafanye majukumu kwa ajili ya nchi”alisema Rais Magufuli.

Rais amewataka kufanya kazi kwa weledi na wasiogope kufanya maamuzi pale inapotakiwa lakini isiwe kwa ubinfasi.

Janauri 8 Rais Magufuli alifanya teuzi za viongozi mbalimbali huku akifanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri, kuteua Makatibu wakuu, Naibu Katibu Wakuu, Balozi na Katibu Tawala.

Rais Magufuli ataka udhibiti mapato ya dhahabu

0

Rais Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Madini kuanzisha vituo vya ukaguzi wa madini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na rekodi ya idadi ya madini yaliyouzwa na kudhibiti mapato yatokanayo na madini.

Hayo ameyasema leo Ikulu jijini Dar Es Salaam baada ya kuwaapisha viongozi mbali mbali aliowateua Januari 8 ambao ni Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Balozi na Katibu Tawala.

Amesema kuwepo kwa vituo hivyo kutasaidia nchi kufahamu kiwango cha madini kinachouzwa nje na ndani ya nchi na kusaidia kutopoteza rekodi ya madini.

“Wizara ya Madini hakikisheni mnaanzisha vituo hivyo vya madini kwani kwa kutokuwepo kwake kunachangia taifa kupoteza fedha nyingi kwa kutojua kiasi gani cha madini kimepatikana na kuuzwa”alisema Rais Magufuli.

Wizara inapaswa kuhakikisha inafanya uchunguzi wa kina kuhusu soko kubwa la dhahabu kwani Tanzania inaonekana kutofaidika na biashara hiyo.

Amesema sheria ya madini iko wazi namna ya kuingia mikataba na watu wakubwa na wafanyabiashara hivyo ametoa wito kwa Wizara ya Madini kuhakikisha inaweka mambo sawa.

Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kupitia Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro kwa juhudi za kukamata dhahabu hivi karibuni mkoani Mwanza.

Amesema juhudi za  askari waaminifu ambao walifanikiwa kuwakamata wenzao nane waliokuwa katika nia ya kutorosha madini hayo zimeonyesha kuwa bado jeshi la polisi lina askari waaminifu na wenye uchungu na nchi yao.

Pia Rais amemtaka waziri mpya wa Madini Doto Biteko kuhakikisha anashughulikia masuala muhimu ili kuhakikisha nchi haipotezi mapato kupitia sekta hiyo ya madini.

Ameitaka Benki Kuu ya Tanzania -BOT kuanzisha utaratibu wa kununua dhahabu na kuhifadhi dhahabu hiyo ili isaidie nchi katika pato la taifa.

Kwa viongozi aliowaapisha, Rais Magufuli amewataka kwenda kufanya  kazi kwa bidii na kuacha ubinafsi utakaosababisha kuzorota kwa maendeleo ya taifa.

Kocha wa Chelsea awalalamikia waamuzi England

0

Kocha wa Chelsea Maurizio Sarri amesema, marefa wa England bado hawajui kuitumia technologia ya var katika kuamua mchezo baada ya kutoa penati kwa Tottenham Spurs katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la ligi,mchezo uliochezwa katika uwanja wa wembely na spurs kuibuka na ushindi wa bao moja kwa bila.

Sarri amesema picha za marudio ya video zinaonyesha Harry Kane alikuwa ameotea lakini cha kushangaza mwamuzi wa mchezo ametoa adhabu ya penati aliyofungwa na Kane.

Timu hizo zitakutana katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya pili ya kuwania kombe la ligi, utakaochezwa katika dimba la Stanford Bridge wiki mbili zijazo.

Simba yarejea Dar es salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Saoura ya Nigeria

0

Kikosi cha Simba kinarejea leo kutoka Zanzibar kilipokuwa kinashiriki kombe la Mapinduzi tayari kujiandaa na mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Saoura ya Algeria mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Januari 12.

Katika mchezo wa Januari 8,Simba ilifunga timu ya Mlandege kwa  bao moja kwa bila na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambapo kikosi cha pili cha Simba kitacheza mchezo huo.

Bao pekee la Simba lilifungwa na Haruna Niyonzima kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa pembeni wa Simba Asante Kwasi kuangushwa katika eneo la penati.

Matokeo ya michezo  mwingine uliochezwa  jana timu ya Kmkm imeibuka  na  ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi yaK,na kuifanya Kmkm kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Michezo hiyo ya kombe la Mapinduzi inaendeleo kwa kuzikutanisha mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam Fc dhidi ya Malindi.

Salah atangazwa kuwa mchezaji bora wa Afrika 2018

0

Mshambuliaji wa timu ya Liverpool na timu ya Taifa ya Misri Mohmed Salah ametangazwa na Shirikisho la soka Barani Afrika Caf kuwa mchezaji bora wa mwaka 2018 wa Afrika katika sherehe za utoaji wa tuzo zilizofanyika jijini dakar nchini senegal

Mohamed Salah amewashinda nyota wengine waliokuwa wanawania tuzo hiyo, Sadio Mane wa Liverpool pamoja na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal ambao wanacheza ligi kuu ya England.

Wakati huo huo shirikisho la soka Barani Afrika Caf limeiteua nchi ya  Misri kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Juni mwaka huu.

Taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika lina miezi isiyozidi sita ya kujiandaa kwa fainali hizo zitakazoshirikisha mataifa 24 mwaka huu.

Misri inaandaa fainali hizo baada ya shirikisho la soka Afrika (Caf) kuipoka Cameroon uenyeji wa fainali hizo kutokana na kusuasua kwa maandalizi ya fainali hizo.