Klabu ya Tottenham kuanza kutumia uwanja wao hivi karibuni

0

Klabu ya Tottenham hotspur imesema uwanja wao mpya wa Whitehart Lane utakuwa tayari na kuanza kutumika kwa michezo mbalimbali  kuanzia mwezi wa tatu mwaka huu.

Spur walipanga kuanza kuutumia uwanja wao mpya kuanzia mwezi wa Tisa kufuatia makubaliano ya awali na mkandarasi, lakini ujenzi umeshindwa kukamilika katika muda waliopanga.

Mwenyekiti wa klabu hiyo  Daniel Levy ameomba radhi kwa mashabiki wa timu hiyo kwa kushindwa kuutumia uwanja wao mpya katika muda waliopanga, na sasa wataendelea kuutumia uwanja wa Wembley kama uwanja wao wa nyumbani.

Manchester city yairarua Burton Albion mabao 9 kwa bila

0

Timu ya Manchester City imetanguliza mguu mmoja katika fainali ya michuano ya kombe la ligi pale England lijulikanalo kama  Carabao baada ya kuifunga timu ya Burton Albion mabao Tisa kwa bila.

Mabao Manne ya Gabriel Jesus, na mengine yaliyofungwa na Kevin De bruyne, Oleksandr Zinchenko, Phil Foden, Kyle Walker na Riyad Mahrez yametosha kuandikisha rekodi mpya kwa Manchester City kupata ushindi mnono wa mabao zaidi ya nane baada ya miaka 31, kwani mara ya mwisho walipata ushindi mnono kwa kuinyuka Huddersfield Town mabao kumi kwa bila, novemba 1987.

Manchester City sasa wanaandika pia rekodi ya kufunga mabao 16 ndani ya siku nne baada ya jumapili iliyopita kuibuka na ushindi wa mabao saba kwa bila dhidi ya Rotherham United katika mchezo wa mzunguko wa tatu wa kombe la Fa.

Manchester city sasa watakuwa na kazi rahisi kuelekea mchezo wa marejeano dhidi ya Burton Albion utakaochezwa januari 23katika dimba la Pirelli,  ambapo mshindi wa jumla ataungana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Chelsea na Tottenham Hotspur kufuzu kwa hatua ya fainali.

Tottenham wanafaida ya bao moja walilolipata katika ushindi mwembamba wa bao moja kwa bila walioupata katika mchezo dhidi ya Chelsea.

Fainali ya michuano hii itafanyika februari 24 katika dimba la wembley mjini London.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi DRC (Ceni) yamtangaza Tshisekedi kuwa mshindi wa urais.

0

Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo imesema kuwa Mgombea urais wa Upinzani Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi wa Rais nchini humo.

Matokeo ya uchaguzi ya awali kutoka katika majimbo mbalimbali yanaonyesha mgombea huyo wa upinzani amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea kutoka chama tawala Emmanuel Shadary.

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, amesema mapema Alhamisi kwamba Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na anatangazwa mshindi wa urais mteule.

Tshisekedi alipata zaidi ya kura Milioni 7 huku Fayulu akipata kura takriban Milioni  6.4  na mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary akipata takriban kura Milioni 4.4.

Tayari mgombea Fayulu ameyapinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi. Kwa mujibu wa taarifa ya Idhaa ya kifaransa ya BBC  amesema kwamba matokeo hayo ni kashfa na haya uhalisia wa kweli.

Hatua zaanza kuchukuliwa dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini

0

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imeanza kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika mikoa iliyo mpakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo    -Drc.

Akizungumza na wananchi Mkoani Katavi, Afisa Programu wa Mawasiliano ya Afya kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Tumaini Haonga amesema mpaka sasa hajaripotiwa mgonjwa yeyote wa Ebola hapa nchini na kwamba tayari wameweka mikakati ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo wakati wowote.

Katika mkutano wa dharura na uhusishaji jamii dhidi ya tishio la mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, Idara ya Afya Mkoa wa Katavi kupitia kwa Mganga Mkuu wa mkoa huo Dakta Omary sukali anasema wamejipanga kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo wa Ebola wakati wowote.

Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imeanzisha vituo vya kuhudumia wagonjwa wa Ebola Mkoani Katavi kituo pekee ni Kituo cha Karema ufukweni mwa Ziwa Tanganyika.

Serikali pia imefanya maandalizi ya kutosha ya kuwa na wataalam wanaoweza kutoa huduma za dharura kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola.

Tayari watalaam kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto wamesambaa katika mikoa ya Katavi, Kigoma, Mwanza, Kagera, Rukwa, Songwe, Mbeya, na Dar es salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo wananchi na tishio la ugonjwa wa Ebola hapa nchini.

Serikali yataka ujenzi wa Rada kukamilika kwa wakati

0

Serikali imeitaka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini -Tcaa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa rada mpya ya kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Agizo hilo limetolewa Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye baada ya kufanya ziara katika uwanja huo na kusema Rada hiyo inatakiwa ianze kutumika mapema kwa manufaa ya Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tcaa, Hamza johari ameahidi kutekeleza maagizo hayo.

Mkataba wa ujenzi wa Rada hiyo ulisainiwa March mwaka 2018 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.3.

Tanesco Dodoma yapewa siku 10 umeme kurejea katika hali yake

0

Waziri wa Nishati Dokta Merdan Kalemani ametoa Siku kumi na nne kwa Meneja wa Shirika la Umeme Mkoani Dodoma kuhakikisha umeme katika Jiji la Dodoma haukatiki mara kwa mara.

Dokta Kalemani amesema hayo katika ziara yake ya kukagua vituo vya kufulia umeme ambapo ameshuhudia umeme unaozalishwa ni mwingi na kuwepo na ziada na kutokuwepo kwa sababu ya umeme kukatikatika katika katika Jiji la Dodoma.

Pia amemtaka mkandarasi anayefanya upanuzi wa kituo cha kufulia umeme zuzu kukamilisha mradi  huo kwa wakati  ili kuhakikisha haujitokezi upungufu wa umeme kutokana na ongezeko la watumiaji wa umeme Mkoani Dodoma.

Katika hatua nyingine Waziri Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Mkoani Dodoma kuimarisha ulinzi katika vituo vya kufulia umeme.

Wakala wa barabara watakiwa kujenga haraka barabara mkoani Pwani

0

Bodi ya Barabara Mkoa wa  Pwani imewaagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini -Tarura kujenga haraka barabara ambazo zinafungua maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.


Agizo hilo limetolewa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo wakati akifungua kikao cha bodi  hiyo cha kujadili na kupitisha bajeti ya fedha zitakazitumika kujenga miradi ya barabara  katika kipindi cha mwaka 2019/2020..

Pia amewataka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini -Tarura kufungua barabara  zote zinazoenda katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na kutoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini -Tanroads pamoja na Tarura kuhakikisha barabara  wanazojenga zinaendana na kiasi cha fedha kilichotengwa.


Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara  Mkoa wa Pwani, Yudas Msangi amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 zaidi ya Shilingi Bilioni arobaini ma sita zimetengwa kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara  ikiwemo upanuzi wa Daraja la Mto Wami.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka ameishukuru serikali kwa kuanza kujenga barabara za lami katika kitovu cha mji huo.

Watoto waliofaulu Mkoani Dodoma marufuku kusafiri bila kibali

0

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amepiga marufuku wazazi kuwasafirisha watoto waliomaliza elimu ya msingi na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kutoka nje ya mkoa pasipo kibali cha uongozi wa kijiji ili kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanajiunga na Kidato cha kwanza.

Dokta Mahenge ametoa onyo hilo katika ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa Wilayani Chamwino ili kuwawezesha wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Dokta Mahenge pia amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma  kuweka mikakati ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi watakaochaguliwa mwaka ujao wa 2020, badala ya kusubiri matokeo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga amesema wanakabiliwa na changamoto ya kuwaandikisha wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia za wavuvi na wafugaji kutokana na kuhamahama.