Kansela Angela Merkel afanya ziara nchini Ugiriki

0

Kansela Angela Merkel  wa Ujerumani amefanya ziara nchini  Ugiriki  kuonyesha mshikamano na nchi hiyo baada ya kipindi kigumu cha kubana matumizi na kuipa msaada wa kidiplomsia kuhusu ubadilishaji wa jina wa taifa jirani la Macedonia.

Merkel pia amefanya  mazungumzo na waziri Mkuu Alexis Tsipras kujadili hatua inayosubiriwa ya kubadili jina la taifa hilo la Macedonia iliyokuwa sehemu ya Jamhuri ya zamani ya Yugoslavia .

Merkel alizuru mji mkuu wa Macedonia, Skopje kabla ya kura ya maoni juu ya kubadili jina kuonyesha uungaji wake mkono ambapo bado  suala hilo linasababisha mgawanyiko nchini Ugiriki ambako mojawapo ya vyama vinavyounda muungano wa Tsipras kinapinga na kutishia wingi wake wa bungeni.

Wakati huo huo polisi  nchini Ugiriki imewatawanya  kwa kutumia mabomu ya machozi mamia ya waandamanaji waliokuwa wakipinga ziara hiyo ya Merkel 

Rais wa Nigeria ajihakikishia kushinda awamu ya pili ya uchaguzi

0

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema ana uhakika wa kushinda muhula wa pili, katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 mwezi Februari mwaka huu.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76 amesema hayo katika  kampeni zake za  kuelekea uchaguzi mkuu nchini  humo ambapo ujumbe wake mkubwa katika kampeni hizo ni kuendeleza vita dhidi ya ufisadi.

Hivi karibuni Rais huyo aliwaambia wafuasi wake jijini Abuja, kuwa kwa muda wa miaka minne ambayo amekuwa madarakani, ametekeleza ahadi ya kuimarisha usalama lakini pia kupambana na rushwa.

Wagombea 78 kutoka vyama 91, wanawania nafasi ya urais nchini Nigeria ambapo ushindani mkubwa katika uchaguzi huo  unatajwa kuwa ni  kati ya Buhari na mgombea wa chama kikuu cha upinzani Pdp na aliyekuwa Makamu wa rais Atiku Abubakar.

Umoja wa Afrika yajiandaa kusuluhisho mgogoro nchini Congo

0


Umoja wa Afrika Au umetoa wito wa kusuluhisha kwa amani mzozo wowote utakaotokana na matokeo ya uchaguzi nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo yaliyompatia ushindi mgombea wa upinzani Felix tshisekedi .

Taarifa kutoka ofisi ya mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat imesema ni muhimu kwamba tofauti zozote kuhusu matokeo hayo yaliotangazwa na Tume ya uchaguzi  yatafutiwe muafaka wa kitaifa kwa kuheshimu kanuni za demokrasia pamoja na kulinda na kuimarisha amani.

Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesisitiza kuwa  matokeo ya awali hayawiani na takwimu zilizokusanywa na wasimamizi wake.

Mapema hapo jana Kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi alitangazwa kuwa mshindi wa uraisi  nchini humo lakini mgombea mwenzake wa upinzani Martin  Fayulu ameyapinga matokeo hayo kwa kusema  ni ya udanganyifu.

Msemaji wa Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic amesema kwa sasa wanasubiri ufafanuzi kutoka kwa waangalizi wa Kimataifa huku ikizitaka pande zote kujiepusha na vurugu na kuonya kuwa matokeo ya mwisho yanapaswa kuendana na matakwa ya raia wa Congo.

Rais afurahishwa na Airtel kuongeza hisa za Serikali

0

Rais John Magufuli amesema amefurahishwa na hatua na iliyofikiwa Kampuni ya Bharti Airtel ya kuongeza hisa zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania katika Kampuni ya Airtel Tanzania kutoka Asilimia 40 hadi Asilimia 49 na hivyo kupunguza hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Bharti Airtel.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bharti Airtel, Sunil Mittal, Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo wamezungumzia maendeleo ya mazungumzo ya umiliki wa hisa za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Bharti Airtel, Sunil Mittal ameongeza kuwa mazungumzo kati ya kampuni yake na Serikali ya Tanzania yanakwenda vizuri na kwamba kampuni ya Bharti Airtel imeridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa katika masuala yaliyokuwa yakijadiliwa yenye lengo la kuiimarisha kampuni ya Airtel, kuleta manufaa kwa pande zote mbili na kuboresha huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.

Kilele cha Sherehe za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanyika Januari 12

0


Kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar kinatarajia kifikiwa hapo Kesho ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapanduzi Dokta Ali Mohamed shein ndiye atakayekuwa mgeni rasmi.

Akizungumza na Tbc Kisiwani Pemba  Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed amesema shughuli hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi  mbalimbali wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Aboud ametoa wito kwa wananchi kiziwani humo kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Gombani ili kusherekea sherehe  hizo.

Kauli mbiu ya maadhimisha ya Miaka 55 ya Mapindizi ni “’Mapinduzi yetu ndio Umoja wetu, Tuyalinde kwa maendeleo yetu”.

Mamlaka ya viwanja vya ndege waendelea na ukarabati wa vyumba vya abiria

0

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Richard Mayongela amesema mamlaka yake imeanza kufanya marekebisho ya vyumba vya abiria katika viwanja vikubwa hapa nchini ili kuendana na mahitaji ya ongezeko la abiria kutokana na ujio wa ndege mpya za shirika la ndege Tanzania.

Mayongela amesema hayo katika Kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Tbc, na kubainisha kuwa marekebisho katika viwanja vya ndege yanaenda sambamba na upanuaji wa viwanja kikiwemo kile cha Iringa.

Kuhusu mapato yatokanayo na viwanja vya ndege, Mayongela amesema katika kipindi cha miaka mitatu wameongeza zaidi ya Asilimia ishirinI ya mapato kutokana na kuboresha hudma na kupungza matumizi yasiyo na lazima kwa Asilimi kumi.

Pia amesema Jengo la Tatu la abiria na miundombinu yake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere litakabidhiwa rasmi Mei mwaka huu ambapo litakuwa na uwezo wa kupokea abiria Milioni sita kwa mwaka.

Vifaa vya ujenzi Mkoani Dodoma kufanyiwa ukaguzi wa ubora

0

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameliomba Shirika la Viwango Mkoani Dodoma, Wakala wa Barabara za Mjini na Vijini Tarura na Wakala wa Barabara nchini -Tanroads kufanya ukaguzi wa ubora wa vifaa vya ujenzi yakiwemo matofali ili kuhakikisha majengo yote yanayojengwa jijini Dodoma yanakuwa salama.

Dakta Mahenge ametoa ombi hilo wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea katika wilaya ya Dodoma Mjini ambapo ametilia shaka ubora wa matofali yanayotumika katika ujenzi wa baadhi ya shule.

Kwa upande wake wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi anaahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo ya mkuu wa mkoa nakukakisha ubora wa matofali unaotumika ni wa kiwango cha juu.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu , ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde ameahidi  kuendelea kushirikiana na serikali ya mkoa kuhakikisha kuna kuwa na madarasa ya kutosha na wanafunzi wanaendelea na masomo yao.

Mpaka sasa Wilaya ya Dodoma Mjini inakabiliwa na upungufu wa madarasa 52 kwa shule za sekondari.

Wahandisi wazembe kutopewa kazi za miradi ya maji nchini

0


Serikali imesema haitawajumuisha baadhi ya wahandisi wanaozembea kukamilisha miradi mbalimbali ya maji katika Wakala wa Maji Vijijini na Mijini mara wakala huo utakapoanza.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Kagera ambapo amekagua mradi wa maji wa Manispaa ya Bukoba ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia kwa zaidi ya Shilingi bilioni thelathini na nane.

Japokuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni thelathini na nane kwa ufadhili wa Benki ya Dunia bado haujaweza kukidhi mahitaji ya maeneo yote.

Meya  manispaa Bukoba , Chifu Kalumuna akaipongeza serikali kwa hatua kubwa ya kupunguza adha ya upatikanaji wa maji katika mji huo.

Kisha Naibu Waziri wa Maji Jumaa aweso pamoja na kupongeza ufanisi katika mradi huo bado anaonekana kutoridhika katika ujenzi wa miradi mingine ya maji Mkoani Kagera akitolea mfano mradi wa Katoke Wilayani Muleba.