Miaka 55 ya Mapinduzi yaadhimishwa Pemba

0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Ali Mohamed Shein amewataka watumishi wa umma kuongeza kasi ya kutekelaza wajibu wao kwa ufanisi ili kutatua na changamoto zinazowakabili wananchi.

Dokta Shein amesema hayo Kisiwani Pemba katika Kilele cha Maaadhimisho ya Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo amesema watumishi wanatakiwa kufanya kazi kwa vitendo na kuongeza kiwango cha uzalendo katika kutekeleza majukumu yao.

Pia akaelezea mafanikio ya sekta mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwemo sekta ya uchumi.

Kilele cha Maadhimisho ya Miaka hamsini na tano ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yamepambwa na vikundi mbalimbali vya ngoma pamoja na maonesho maalum ya Jeshi la Wananchi na Jeshi la Polisi.

Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yalifanyika mwaka 1964 yaliyokuwa na lengo la kumkomboa mwananchi kutoka kwenye utawala wa kikoloni.

Mahakama kuu kutoa uamuzi dhidi ya shauri la muswaada wa sheria

0

Mahakama Kuu ya Tanzania Januari 14 inatarajia kutoa maamuzi dhidi ya shauri lililofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na wenzie ya kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa kujadiliwa bungeni

Mahakama hiyo imesikiliza pingamizi la Serikali dhidi ya shauri  la muswada wa Sheria ya marekebisho ya vyama vya Siasa wa mwaka 2018 chini ya Jaji Benhajji Masoud.

Pingamizi la serikali liliwasilishwa na Jopo la  mawakili wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Mark Mulwambo ambaye amedai kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania haina mamlaka ya kusikiliza shauri la kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Siasa.


Kwa upande  wa walalamikaji wamedai kuwa Katiba inaipa mamlaka mahakama ya kusikiliza shauri hilo kwa sababu inatoa nafasi kwa mtu yeyote kupekea kesi pindi anapoona haki yake au katiba inavunjwa .

Simba kuwavaa JS Soura ya Algeria katika hatua ya makundi

0

Timu ya Simba ya Tanzania leo inashuka katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuivaa Js Soura ya Algeria kwenye mchezo wa  Ligi ya  mabingwa wa Afrika huku ikiwa na matumaini ya kupata ushindi mnono.

Kocha wa Simba  Patrick Aussems akizungumza  Januari 11  amesema kuwa amefanya maandalizi mazuri ya timu na kwamba ana imani na timu yake kufanya vizuri katika mchezo huo .

Amesema wanawaheshimu wapinzani wao hao kwani wana imani kuwa nao wamejiandaa vyema kukabiliana nao hivyo amewajenga wachezaji wake vizuri katika kupambana.

Simba ambayo ipo  kundi  D pamoja na  timu za Al Ahly ya Misri,As Vita ya Congo ya Drc na Js Saoura ya Algeria itakuwa inashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuitoa timu ya  ya Nkana Rangers ya Zambia  kwa mabao matatu kwa moja na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi.

Simba na Azam kuvaana fainali ya michuano ya Mapinduzi

0

Timu za Simba na Azam Fc zitakutana fainali hapo Januari  13 kuwania ubingwa wa michuano ya kombe la mapinduzi baada timu hizo kutinga fainali mchezo utakaofanyika katika dimba la Gombani kisiwani Pemba .

Simba wametinga fainali baada ya kuifunga timu ya Malindi kwa mikwaju ya penati mitatu kwa  moja katika mchezo uliochezwa Januri 11.

Mabeki Yussuf  Mlipili, Mghana Asante Kwasi na kiungo Mohammed ‘mo’ Ibrahim waalifungia  Simba penalti zao huku beki mpya, Zana Coulibaly kutoka Burkina Faso alikosa penati kutokana na kupiga mpira  juu.

Kwa upande wa Malindi, Abdulswamad Kassim pekee alifunga penalti yake, huku Ali Kani, Muharami Issa na Cholo Ali walikosa penati wote.

Bingwa mtetezi wa Michuano ya Kombe la Mapinduzi, Azam Fc wametinga kwa kishindo fainali ya michuano hiyo kwa kuishushia timu ya KMKM kipigo cha mabao matatu kwa bila kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye dimba la Aman Mjini Unguja.

Mabao ya nahodha Aggrey Morris kwenye dakika ya 9, Salu Aboubakar dakika ya 62 na Obreyt chirwa aliyefunga bao la tatu kwenye dakika ya 82 yametosha kuipeleka Azam Fc kwenye fainali ya tatu mfululizo ya michuano hiyo.

Bingwa wa michuano hiyo atajinyakulia kikombe pamoja na kitita cha shilingi Milioni 15 huku makamu bingwa akijizolea kitita cha shilingi milioni 10.

Matangazo yote katika michuano hiyo yatakujia moja kwa moja kupitia Tbc Taifa.

Watanzania watakiwa kuthamini Lugha ya Kiswahili

0

Rais Dkt John Magufuli amewataka Watanzania kuthamini lugha ya Kiswahili kwani ndio lugha inayomtambulisha duniani.

Akizungumza katika hafla ya  uzinduzi wa ndege mpya aina ya Air Bus 220-300 iliyowasili leo katika  uwanja wa ndege wa zamani Terminal One jijini Dar es salaam Rais Dakta Magufuli  amesema anashangazwa na tabia ya baadhi ya watanzania wanaoona aibu kuzungumza lugha ya Kiswahili huku wakithamini lugha nyingine za nje.

Rais Dakta Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akimsifia  balozi wa Canada nchini  Pamela O”DonnellTanzania ambaye amesoma risala yake kwa lugha ya Kiswahili.

“Ninawashangaa sana watanzania ambao wanaona aibu kuzungumza Kiswahili na ambao wanazungumza na watoto wao kiingereza badala ya kuzungumza nao lugha ya Kiswahili au lugha za asili? Alisema Rais Mgaufuli.

Rais Dakta Magufuli amesema Kiswahili kwa sasa ni lugha ya kumi katika lugha zinazozungumzwa zaidi duniani na raia kutoka nchi mbali mbali wanaendelea kujifunza.

Watanzania watakiwa Kujitegemea wenyewe kiuchumi

0

Rais John Magufuli amesema watanzania wanatakiwa kuitekeleza dhana ya kujitegemea kwa ajili ya maendeleo ya taifa lao.

Rais Magufuli ameyaema hayo Jijini Dar es salaam wakati akiongoza watanzania katika kupokea ndege mpya aina ya Airbus iliyonunuliwa na serikali kutoka nchini Canada ambapo amesema pasipo kujitegemea taifa halitaweza kupata maendeleo ya kujivunia.

Ndege mpya aina ya Airbus ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kutokea nchini Canada.

Ndege hii Airbus 220-300 inafanya idadi ya ndege mpya zilizonunuliwa na serikali ya awamu ya tano mpaka sasa kufikia ndege sita.

Akihutubia wageni waliofika kushuhudia mapokezi ya ndege hiyo, Rais John Magufuli amewasisitiza watanzania kundelea kulipa kodi na kuishi katika dhana ya kujitegemea.

Rais Magufuli akatoa agizo kwa Shirika la Ndege nchini -Atcl kuanza kutumia ndege mbili zilizokuwa zikitumia na Rais kwa ajili ya kusafirisha abiria.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia watanzania kuwa serikali itatekeleza ahadi zote walizoahidi wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza taifa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Atcl Mhandisi  Ladislaus Matindi amesema lengo la shirika hilo ni kuendelea kutoa huduma bora ya usafiri wa anga.

Ujio wa ndege mpya ya Airbus 220-300 iliyopewa jina la Ngorongoro inafungua wigo kwa Tanzania kuanza safari za ndege kwa nchi za nje ikiwemo Afrika Kusini, Zambia, India na China.