Rubani wa Atcl awataka vijana nchini kuwa wazalendo

0

Rubani mzawa wa Shirika la Ndege Nchini Tanzania-Atcl raymond Musingi aliyerusha ndege aina ya Airbus 220 Dash 300 kutoka Canada hadi Tanzania amewataka vijana wa Kitanzania wenye nia ya kusomea fani hiyo kujituma katika masomo ya sayansi huku wakitanguliza uzalendo kwa taifa lao.

Musingi amesema hayo mapema asubuhi ya leo katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Tbc One wakati akielezea ubora wa ndege mpya zilizonunuliwa na serikali ya Tanzania.

Aidha Capten Musingi amewaomba marubani wenzake kutumia fursa ya ndege za Atcl kuwaonesha abiria vivutio vya utalii wawapo angani ikiwemo mlima Kilimanjaro ili kuvutia watalii wengi kuja nchini.

Musingi amesema ndege aina ya Airbus 220 Dash 300 zimetengenezwa kwa teknolojia  mpya inayeoendana na mahitaji ya sasa katika usafiri wa anga.

Rais wa Ufaransa aandika barua ya wazi kwa raia wake

0

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameandika barua ya wazi kwa raia wa nchi hiyo ya kutaka kufanya mazungumzo  ya kitaifa  kutokana na maandamano yanayoendelea nchini humo.

Macron amewaandikia raia wake akisema anataka kuzigeuza hasira zao ziwe suluhisho.

Amesema mapendekezo yatakayotolewa katika mjadala huo yatasaidia kupanga vizuri kazi za serikali na bunge pamoja na nafasi ya Ufaransa barani na kimataifa.

Mada zitakazojadiliwa katika mazungumzo hayo ni kuhusiana na  kodi, demokrasia, ulinzi wa mazingira na uhamiaji.

Maandamano yajulikanayo  vizibao vya njano yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa sasa wakipinga sera za serikali ya  Macron.

Wamiliki wa mitandao ya kijamii watakiwa kuwa weledi

0

 Mamlaka  ya  mawasiliano  Tanzania  Tcra  nyanda  za  juu  kusini  imewataka  wamiliki wa mitandao  ya kijamii nchini  kufanya kazi  hizo  kwa  kuzingatia  sheria na weledi  katika kutoa habari kwa  jamii.

Wito  huo  umetolewa Mjini Mbeya   na mkuu wa Tcra  kanda  ya nyanda  za  juu kusini, mhandisi  Asajile John mara  baada ya kukutana  na wamiliki wa  mitandao  hiyo mkoani Mbeya.

Ameeleza kuwa mafunzo haya ni sehemu ya  kuwakumbusha wadau hao juu ya   sheria  na taratibu za Tcra katika kutimiza majukumu yao.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni  ya Kukaja ambao  ndio wasimamizi wa mitandao  hiyo anawataka vijana kutumia mawasiliano ya mitandao  kwa njia iliyo sahihi.

Takukuru yaagizwa kumkamata mhandisi wa maji Mkoani Kagera

0

Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso ameliagiza Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya kupambana na kuzuia  Rushwa nchini  Takukuru wilayani Muleba mkoani Kagera, kumkamata na kumhoji Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba Boniphace Lukoo pamoja na mkandarasi kampuni ya Sajac Investment aliyehusika katika ujenzi wa mradi wa Maji wa Katoke.

Naibu Waziri Aweso amechukua hatua hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wa Katoke ambao wamedai hawajawahi  kupata huduma ya maji  tangu  mradi huo ulipokabidhiwa mwaka 2016 huku mkandarasi akiwa kalipwa shilingi milioni mia nne na nne kati ya milioni mia nne sabini na sita ambazo ni gharama ya mradi wote.

Changamoto ya uhaba  wa Maji imekuwa ikiwakabili  wakazi zaidi ya elfu tatu na mia mbili na arobaini na watano wa kata ya Katoke yenye vijiji viwili vya Katoke na Kahumulo .

Pia  Naibu Waziri Aweso amepiga marufuku mkandarasi huyo kampuni ya Sajac Investment kupewa kazi yoyote ya ujenzi wa miradi ya maji iliyo chini ya wizara hiyo.

Kesi kupinga muswada wa vyama vya siasa bungeni yafutwa

0

Mahakama Kuu ya Tanzania imeifuta kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wabunge wa upinzani wakiongozwa na Zitto Kabwe ya kutaka kuzuia muswada wa kurekebisha vyama vya siasa usijadiliwe bungeni.

Hukumu hiyo imetolewa jijini Dar Es Salaam na Jaji Benhajo Masoud wa Mahakama Kuu nchini na kusema kesi hiyo imeonekana kuwa na dosari kutokana na kukiukwa kwa vifungu vya sheria.

Kesi hiyo ilikuwa ikipinga mjadala wa muswada wa kurekebisha vyama vya siasa katika bunge lijalo waliodai kuwa muswada huo unakiuka katiba na kukandamiza demokrasia nchini.

Pamoja na kuifuta kesi hiyo mahakama hiyo imewataka washtakiwa kuilipa serikali gharama za kuendesha kesi hiyo.

Hivyo kwa sasa baada ya kufutwa kwa kesi hiyo inamaanisha kuwa muswada huo sasa utajadiliwa bungeni kama ilivyopangwa.

Everton yaibuka na ushindi dhidi ya Bournemouth

0

Timu ya Everton wakiwa nyumbani wameitandika timu ya Bournemouth mabao mawili kwa bila na kusogea hadi nafasi ya kumi katika msimamo wa ligi hiyo.

Mabao ya ushindi ya Everton yamepatikana kipindi cha pili cha mchezo baada ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila majibu.

Mabao hayo yamefungwa na wachezaji Kurt Zouma na Dominic Calvert-Lewin akifunga dakika ya tisini ya mchezo.

Ndege za Rais kuanza kusafirisha abiria hivi karibuni

0

Mkurugenzi Mkuu Shirika la Ndege Tanzania –Atcl, Ladislaus Matindi amesema wataanza kuzitumia ndege mbili aina ya Foca waliozopewa na rais Dkt. John Magufuli kwa matumizi ya kubebea abiria kutokana na ndege hizo kuwa na mfumo unaoruhusu kubadilishwa matumizi yake.

Matindi amesema hayo katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Tbc one, wakati akielezea mikakati ya shirika hilo kufuatia ujio wa ndege ya pili aina ya Air bus 220-300 na kubainisha kuwa ndege mbili walizopewa na rais aina ya Foca, zitafanyiwa marekebisho ya mfumo na watalaam wa ndege hapa nchini ili zianze kutoa huduma mapema.

Kuhusu matengenezo ya ndege mbli za bombadier q400, Matindi amesema ndege hizo zinafanyiwa marekebisho ikiwa ni utaratibu wa kawaida baada ya kufikisha idadi ya kilometa ili kuboresha ufanisi wake.

Aidha Matindi amebainisha kuwa shirika hilo limefanya utafiti wa kina ili safari zote zinazofanywa na ndege zake zilete tija na faida kwa shirika hilo katika safari za ndani na nje ya nchi.