Rais Magufuli akabidhiwa mfumo wa TTMS

0

Rais Dkt. John Magufuli amekabidhiwa mfumo mpya wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu – TTMS na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania –TCRA huku akiwataka watanzania kutumia vema sekta ya mawasiliano.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini DSM Rais Magufuli amesema mfumo huo una manufaa kwa taifa na kuwataka TCRA kuulinda kwa nguvu zote kwa kuwa ni nyeti.

Rais Magufuli ametoa agizo kwa watanzania kuhakikisha wanatumia vema mitandao kwani imesababisha madhara makubwa duniani ikiwemo uhalifu wa kimtandao na uvunjwaji na mmomonyoko wa maadili.

“Naomba TCRA mhakikishe mnatoa adhabu kali kwa wananchi wanaotumia vibaya mawasiliano kwani hawa wanachangia kuleta maafa hapa nchini”alisema Rais Magufuli.

Mfumo huo ulianza kutumika mwaka 2013 ambapo mpaka sasa umeongeza faida nchini ikiwemo kuongeza mapato kutokana na kodi inayopatikana kwenye kampuni za simu ambapo shilingi Bilioni 93 zimepatikana.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe amesema mfumo huo mpya umewezesha kutambua masuala mbalimbali ikiwemo mawasiliano ya simu yanayofanyika kwa udanganyifu na mifumo ya  simu za udanganyifu iliyokuwa imeunganishwa.

Mfumo wa usimamizi wa matumizi ya simu kuzinduliwa Januari 18

0

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini -TCRA Mhandisi James Kilaba amesema mfumo mahiri ya usimamizi wa matumizi ya simu uitaleta maendeleo nchini kupitia shughuli zinazohusiana na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam  Mhandisi Kilaba amesema mfumo huo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi na kijamii nchini.

Makabidhiano ya mfumo huo rasmi yatafanyika Januari 18 ambapo mgeni rasmi wa hafla hiyo anatarajiwa kuwa  Rais John Magufuli

Wawekezaji viwanda vya maziwa waomba kutatuliwa changamoto zao

0


Wawekezaji wa viwanda vya kusindika maziwa mkoa wa Iringa wameiomba serikali kupitia idara ya Mufugo kushirikiana na sekta binafsi ili kutatua changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo nchini.


Wakizungumza  na mkuu wa a mkoa wa Iringa alipofanya ziara  ya kutembelea viwanda vilivyopo mkoani humo na kujua changamoto zake ambapo  wawekezaji hao  wanasema  kuwa wafugaji wengi wanahitaji elimu ya ubora wa bidhaa yao.

Akiongea kwa niaba ya wawekezaji mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika maziwa cha Asas, Fuad Abri amesema bado idara ya mifugo haijawashirikisha vema sekta binafsi na kujua maoni yao juu ya nini kifanyike ili kuinua sekta hiyo.

Kwa upande wake  Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewataka maafisa ugani kwenda kwa wafugaji na kutoa elimu ya uzalishaji maziwa wenye tija pamoja na  kuhamasisha wananchi kuhusu  unywaji wa maziwa.

Simba yawafuata As Club Vita

0

Msafara wa wachezaji 20 wa timu ya Simba ukiambatana na benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi umeondoka nchini asubuhiI Januari 17 kuelekea jijini  Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kuwakabili As Club Vita katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mchezo huo wa pili wa kundi De utachezwa jumamosi ya wiki hii January 19 majira ya saa moja jioni mjini Kinshasha na Kikosi cha SIMBA imesafiri bila ya nahodha wake John Bocco aliyemajeruhi ambapo nafasi yake imechukuliwa na Adam Salamba.

Katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo, Simba ambao ndio vinara wa kundi, walianza vyema kwa kupata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Js Saoura ya Algeria katika mchezo uliochezwa Januari 12   katika uwanja wa Taifa jijini Dare es salaam.

Simba wanaongoza kundi lao la De wakiwa na alama tatu sawa na Al Ahly ya Misri, lakini Simba wana uwiano mzuri wa mabao ya kufunga ambapo wao wana mabao matatu huku Ahly wakiwa na mabao mawili.

Mchezo mwingine wa kundi hilo utachezwa kesho Ijumaa ambapo bingwa wa kihistoria wa michuano hiyo Al Ahly wanasafiri hadi nchini Algeria kumenyana na Js Saoura wanaoburuza mkia kwenye kundi lao.

Familia zatakiwa kuheshimu haki za watumishi wa ndani

0

Jamii imetakiwa kuwathamini na kuheshimu haki na mikataba ya watumishi wa ndani ili kumaliza mitafaruku inayotokea mara kwa mara ikiwemo unyanyasaji wanaofanyiwa watoto katika familia.

Ushauri huo umetolewa na Mwandishi wa kitabu cha Thamani ya Dada wa kazi za nyumbani, Astelia Bulugu na Mwalimu wa masuala ya malezi Wilbroad Prosper katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC One kwamba familia zinapaswa kuwaheshimu  wafanyakazi wa ndani kwani ni watu muhimu.

Aidha wadau hao wa masuala ya malezi wamesema wafanyakazi wa ndani ni kiungo muhimu katika familia hivyo wanatakiwa kupewa elimu mara kwa mara juu ya malezi, haki na wajibu wao.

Kukosekana kwa maelewano mazuri kati ya wazazi na watumishi wao wa ndani kumepelekea kutokea kwa matukio mbalimbali ya unyanyasaji unaofanywa na pande zote mbili huku baadhi ya matukio hayo yamepelekea vifo.

Gbagbo azuiwa na Icc kuondoka nchini Uholanzi

0

Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai Icc, iliyoko huko The Hague, Uholanzi  imemzuia rais wa zamani wa Ivory Coast,Laurent Gbagbo, kuondoka nchini humo licha ya kuachiwa huru.

ICC imemzuia Gbagbo kuondoka Uholanzi, akiwa anajiandaa kurejea nchini mwake, baada ya waendesha mashtaka katika mahakama hiyo kukata rufaa dhidi ya kesi inayomkabili ya kuhusika na makosa ya uhalifu wa kivita nchini mwake.

Gbagbo anatuhumiwa kutenda kosa hilo miaka minane iliyopita, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Ivory Coast uliompatia ushindi mpinzani wake mkuu Alsane Outtarra, na yeye kukataa kuondoka madarakani.

Askari waliokuwa wakimuunga mkono mwanasiasa huyo walipita nyumba kwa nyumba kuwasaka wapinzani wake na kuwaua pamoja na raia wa kigeni, hali iliyosababisha watu wapatao elfu tatu kupoteza maisha nchini Ivory Coast.

Wafuasi wa Gbagbo walionekana kushangilia, baada ya Icc kutangaza kuwa imemwachia huru mwanasiasa huyo, baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.

Hata hivyo baadhi ya watu ambao ndugu za walikufa wakati wa mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory coast walionekana kukosa amani.