Ethiopia na Somalia kuwakabili Al Shabaab

0

Ethiopia  na Somalia  zimekubaliana kuunganisha nguvu ili kupambana na wanamgambo wa Al Shabaab wa nchini Somalia ambao wameendelea kuhatarisha usalama wa nchi hizo na nchi nyingine jirani.

Mataifa hayo yamefikia makubaliano hayo baada ya wanamgambo hao kufanya shambulio katika kambi moja ya kijeshi nchini Somalia na kusababisha vifo vya askari kadhaa, kabla ya kushambuliwa na vikosi vya Marekani.

Wanamgambo hao wa Al Shabaab,  wiki iliyopita walifanya mashambulio nchini Kenya na kusababisha vifo vya watu 21 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Habari zaidi kutoka nchini Kenya zinasema kuwa watuhumiwa watano katika shambulio hilo ambalo ni la kigaidi  wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya kuhusika na ugaidi.

Raia wa Kenya wameendelea kuwa na wasiwasi baada ya kubainika kuwa magaidi wanne kati ya watano waliohusika na shambulio hilo lililotokea mjini Nairobi ni raia wa nchi hiyo.

Tshisekedi aendelea kutambuliwa

0

Nchi mbalimbali za Afrika pamoja na Jumuiya za Kimataifa zimeendelea kumtambua Felix Tshisekedi kuwa ndiye rais ajaye wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada ya mahakama ya katiba ya Jamhuri hiyo  kuidhinisha ushindi wake.

Mahakama hiyo ya katiba imefikia uamuzi huo na kutupilia mbali madai ya mpinzani mkuu wa Tshisekedi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba 30 mwaka 2018  Martin Fayulu,  aliyesema kuwa ndiye mshindi.

Miongoni mwa nchi za Afrika zilizotangaza kumtambua Tshisekedi ni Kenya na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambao kwa pamoja wamempongeza Tshisekedi kwa ushindi huo  na kutoa wito wa kufanyika kwa  makabidhiano ya amani ya madaraka.

Disemba 30 mwaka 2018, Fayulu aliwasilisha ombi katika mahakama hiyo ya katiba akidai kuwa kulikua na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu wakati wa uchaguzi huo na kwamba Tshisekedi amefanya makubaliano ya kugawana mamlaka na Rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila, madai yaliyokanushwa na Rais huyo mteule.

Fayulu ambaye alishika nafasi ya pili katika matokeo ya uchaguzi huo wa rais,  ameendelea kupinga matokeo hayo na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kutomtambua Tshisekedi na ameitisha maandamano ya nchi nzima kwa lengo la kupinga matokeo hayo.

Rais huyo mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwenye umri wa miaka 55, ataapishwa Jumanne Januari 22 mwaka huu ili kushika rasmi wadhifa huo wa urais.

CAG atinga bungeni

0

Mdhibiti  na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  Profesa Mussa Assad tayari amewasili katika ofisi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko  jijini Dodoma ili kuhojiwa na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.

Profesa Assad ameitikia wito wa Spika wa Bunge Job Ndugai  aliyemtaka afike mbele ya kamati hiyo kufuatia kauli yake aliyoitoa kwa Bunge kuwa ni dhaifu.

Katika ofisi hizo za Bunge jijini Dodoma, Profesa Assad amepokelewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge ya  Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge, – Emmanuel Mwakasaka.

Mourinho atetea kufanya vibaya akiwa na Manchester United

0

Aliyekuwa kocha wa Manchester United ya England – jose Mourinho ametetea mwenendo mbovu  wa timu hiyo ilipokuwa nanye ambao ulipelekea kufukuzwa kazi kwenye timu hiyo mwezi Desemba mwaka jana.

Mourinho amesema watu hawajui kinachotokea nyuma ya pazia ndiyo maana wanakosoa kirahisi matokeo ya kinachofanyika nyuma ya pazia.

Kocha huyo Mreno anasema mambo hayakuwa shwari ndani ya Manchester United ndiyo mana alivurunda kwenye msimu wake wa mwisho hali iliyosababishwa na kutoungwa mkono na bodi ya klabu hiyo.

Anasema kuna maamuzi alikuwa anataka yachukuliwe ili timu ikae sawa lakini bodi haikuonyesha ushirikiano jambao lililopelekea mpasuko kwenye timu na kuifanya ikose matokeo mazuri.

Kati ya mambo ambayo Mourinho amewahi kuyalalamikia hadharani alipokuwa akiwanoa Mashetani Wekundu ni pamoja na uongozi kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji aliokuwa anawataka huku yeye pia akilalamikiwa kwa kutokuelewana na wachezaji wake wakiongozwa na Paul Pogba.

Hata hivyo Mourinho ameongeza kuwa hafikirii kustaafu kufundisha kabumbu kwani umri wake bado mdogo na siku si nyingi atarejea kufundisha kandanda kwenye timu kubwa.

Waaandishi wamelaani kifo cha mwandishi nchini Ghana

0

Chama Waandishi wa Habari nchini Ghana kimelaani tukio la mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi nchini humo – Ahmed Hussein-Suale aliyeuawa kwa kupigwa risasi mara tatu siku ya Januari 16.

Tukio hilo linafuatia ripoti kadhaa za kiuchunguzi alizozifanya Hussein-Suale akiwa chini ya kampuni ya Tiger Eye Private Investigations ambapo alihusika katika kufichua vitendo vya rushwa kwenye soka la Ghana na ripoti hizo zilisababisha aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Ghana – Kwesi Nyantakyi kufungiwa maisha kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu.

Rais wa Chama cha Wanahabari nchini Ghana – Roland Affail Monney amesema Hussein-Suale alikuwa shujaa wa taifa hilo aliyetumia kalamu yake kuua uovu na sio kuua watu kwa risasi kama alivyouawa yeye hivyo tukio hilo limeijeruhi tasnia ya habari nchini Ghana.

Muda mchache baada ya kuonyeshwa kwa makala walizotengeneza wakina Hussein-Suale, Mbunge Kennedy Agyapong alisambaza picha za Hussein-Suale kupitia vyombo vya habari akitaka mwandishi huyo wa habari aadhibiwe vikali kwa kuwachafua watu mashuhuri nchini humo.

Hata hivyo mbunge huyo amekana kuhusika kwa namna yoyote na mauaji hayo akisema shutma zinazoelekezwa kwake si za kweli.

Mourinho ateetea kufanya vibaya akiwa na Manchester United

Aliyekuwa kocha wa Manchester United ya England – jose Mourinho ametetea mwenendo mbovu  wa timu hiyo ilipokuwa nanye ambao ulipelekea kufukuzwa kazi kwenye timu hiyo mwezi Desemba mwaka jana.

Mourinho amesema watu hawajui kinachotokea nyuma ya pazia ndiyo maana wanakosoa kirahisi matokeo ya kinachofanyika nyuma ya pazia.

Kocha huyo Mreno anasema mambo hayakuwa shwari ndani ya Manchester United ndiyo mana alivurunda kwenye msimu wake wa mwisho hali iliyosababishwa na kutoungwa mkono na bodi ya klabu hiyo.

Anasema kuna maamuzi alikuwa anataka yachukuliwe ili timu ikae sawa lakini bodi haikuonyesha ushirikiano jambao lililopelekea mpasuko kwenye timu na kuifanya ikose matokeo mazuri.

Kati ya mambo ambayo Mourinho amewahi kuyalalamikia hadharani alipokuwa akiwanoa Mashetani Wekundu ni pamoja na uongozi kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji aliokuwa anawataka huku yeye pia akilalamikiwa kwa kutokuelewana na wachezaji wake wakiongozwa na Paul Pogba.

Hata hivyo Mourinho ameongeza kuwa hafikirii kustaafu kufundisha kabumbu kwani umri wake bado mdogo na siku si nyingi atarejea kufundisha kandanda kwenye timu kubwa.

Mlipuko wa bomu waua watu 21 nchini Colombia

0

Watu 21 wamekufa na wengine 68 wamejeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu lilitegwa ndani ya gari nje ya chuo cha polisi nchini Colombia.

Polisi nchini humo wamesema bomu hilo lilitegwa katika gari hilo lililengwa kwa polisi waliopo katika chuo hicho cha polisi kilichopo mjini Bogota lakini raia wengi waliopo nje ndio waliouwawa pamoja na washambuliaji.

Serikali ya nchi hiyo imetangaza siku tatu za maombolezo  huku waziri wa ulinzi wa nchi hiyo akisema tukio hilo ni la kigaidi.

Ulinzi mkali umeimarishwa katika maeneo hayo ya chuo ambapo pia rais wa nchi hiyo Ivan Duque ameamrisha kuimarisha mipaka yote ya Colombia , ndani na nje ya mji.

Umoja wa Afrika wataka kusitishwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi Congo

0

Umoja wa Afrika AU umeomba kusitishwa kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais ambayo yanaendelea kuibua maswali mengi nje na ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais wa Umoja huo Paul kagame amekutana na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (Icglr) katika mkutano wa faragha ulodumu takriban saa tano.

Katika taarifa yao ya mwisho ya mkutano huo wameomba mamlaka nchini Drc kusitisha mpango wa kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais baada ya kubaini kuna mashaka makubwa katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais na ule wa wabunge na magavana wa mikoa yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (Ceni).

Viongozi hao wamesema wanatarajia kutuma  ujumbe wa ngazi ya juu mjini Kinshasa kukutana na mamlaka husika.

Ujumbe huo utaundwa na rais wa sasa Umoja wa Afrika Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, na viongozi wengine ambao walihudhuria mkutano huo.

Mahakama ya Katiba inatarajia kutangaza baadae leo matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais wa Desemba 30, 2019.

Rais Magufuli ataka taasisi za umma kuunganishwa mfumo wa elektroniki

0

Rais Dkt. John Magufuli ameagiza Taasisi za Umma kuunganishwa kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki ili kuiwezesha serikali kufahamu kiwango cha mapato kutoka kwenye taasisi hizo na kutumika kwa maendeleo ya taifa.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jijini Dar Es Salaam wakati akizindua mfumo mpya wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) ambapo amesema tangu mfumo huo uanze serikali imekusanya shilingi Bilioni 93.6.

Pia Rais Magufuli amewapongeza watumishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania –TCRA kwa kuchapa kazi bila woga kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele.

Halikadhalika Rais Magufuli ameongeza mkataba wa miaka mitano wa utumishi kwa Mkurugunzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba amesema kukamilika kwa mradi huo, kutachochea ukusanyaji wa mapato kupitia miamala ya fedha kwa njia ya mawasiliano.