Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, – Abdulmajid
Nsekela amesema kuwa kwa muda mrefu
imekua ni vigumu kuwakopesha wachimbaji wa madini nchini kutokana na wachimbaji
hao kutokuwa na makazi ya kudumu.
Nsekela ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam, wakati
wa mkutano wa wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya
madini, mkutano uliokuwa na lengo ya kujadili changamoto mbalimbali
zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini na namna ya kuzitatua changamoto
hizo.
Amesema kuwa hatua ya wachimbaji hao wa madini
kutokuwa na makazi ya kudumu, inawawia vigumu watendaji wa benki hiyo ya CRDB kuwafuatilia
ili kuwapatia mikopo.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya CRDB,
– Abdulmajid Nsekela amesema kuwa pamoja
na ugumu huo, bado ipo nafasi ya kuzungumza
na wachimbaji hao wa madini kwa lengo la kuona
namna ya kuweza kuwapatia mikopo kuanzia hivi sasa.
Timu tatu za mpira wa miguu kutoka nchini Morocco zimepangwa kwenye kundi
moja katika hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Barani Afrika katika droo
iliyofanyika Januari 21 mwaka huu.
Katika kundi A, bingwa mtetezi wa michuano hiyo Raja Casablanca
wamepangwa na timu ya Renaissance Berkane na Hassania Agadir, wakiwa pamoja na timu ya As Otoho Oyo ya Congo
Brazzaville.
Kundi B zipo timu mbili za Tunisia,
ambazo ni bingwa wa kihistoria wa
michuano hiyo CS Sfaxien na bingwa mara mbili wa kombe hilo la Shirikisho
Barani Afrika, -Etoile Du Sahel.
Timu nyingine mbili zinazounda kundi hilo ni Salitas ya Burkina Faso na Enugu Rangers kutoka nchini Nigeria.
Nalo kundi C, timu ya Nkana FC ya Zambia
itacheza na Zesco United pamoja na timu za Al Hilal ya Sudan na miamba ya
Asante Kotoko ya nchini Ghana.
Kundi la D linaundwa na timu za
Zamalek ya Misri, Hussein Dey ya Algeria, Petro Atletico ya Angola na Gor Mahia
kutoka nchini Kenya.
Hatua ya makundi ya michuano hiyo itaanza
mwezi Februari mwaka huu ambapo michezo
mitatu itapigwa ndani ya kipindi cha mwezi huu huku michezo ya marudiano
ikichezwa mwezi Machi.
Wadau wa sekta ya madini nchini wameishauri
serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo
wa madini kwa kuondoa kodi mbalimbali ambazo zimekua zikiwaumiza ikiwa ni
pamoja na Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT).
Wadau hao
wametoa ushauri huo jijini Dar es salaam
wakati wa mkutano wa wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa
sekta ya madini, mkutano uliokuwa na lengo ya kujadili changamoto mbalimbali
zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini na namna ya kuzitatua.
Wamesema kuwa kuwepo kwa kodi na tozo nyingi zinazotozwa
na taasisi mbalimbali kunasababisha vitendo vya utoroshwaji wa madini.
Naye mmoja wa wadau hao Mutalemwa Titus amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu wameshindwa kuuza madini yao kutokana na wizara ya Madini kuwakatalia kuyeyusha madini hayo aina ya Tin, hivyo kumuomba Rais Magufuli kuingilia kati suala hilo.
Muinjilisti Solomoni Mihayo ni Mdau wa madini kutoka mkoani Geita, yeye ametaja njia mbalimbali zinazoweza kutumiwa na watu wasio waaminifu kusafirisha madini nje ya nchi ikiwa ni pamoja na madini yenye thamani kubwa kufungwa kwenye matairi ya akiba ya magari na kuwekwa kwenye vioo vya kuongozea magari.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, – Paul Makonda ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali za kuiletea nchi maendeleo na kuifanya iweze kujitegemea.
Makonda ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es salaam ametumia mkutano huo kuwaomba Watanzania wote kuendelea kuwa wazalendo hasa katika kuitetea nchi yao mahali popote walipo na wale wenye nia ya kuitangaza nchi vibaya kuacha kufanya hivyo.
Amempongeza Rais John Magufuli na serikali yake kwa kazi nzuri ya kuliletea Taifa maendeleo ikiwemo ile ya kuboresha miundombinu ya aina mbalimbali.
Ufunguzi wa mkutano huo wa wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini pia umehudhuriwa na Rais John Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi mbalimbali wa serikali, siasa pamoja na wale wa kidini.
Baraza la Mawaziri limeridhia utozwaji wa
kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme
unaouzwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa Shirika la Umeme la
Zanzibar (ZECO) na kufuta malimbikizo ya deni la kodi ya VAT lililofikia
shilingi Bilioni 22.9 kwa TANESCO kwenye umeme uliouzwa ZECO.
Baraza la Mawaziri limefanya uamuzi huo
Ikulu Jijini Dar es salaam, katika kikao kilichoongozwa na Rais John Magufuli
na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali
Mohamed Shein, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Mawaziri.
Akizungumza baada ya kikao hicho
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri Rais John Magufuli amesema kuwa baada ya
kufanya uamuzi huo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango atawasilisha
marekebisho madogo ya sheria ya VAT sura ya 148 kupitia sheria ya fedha ya
mwaka 2019 ili umeme unaouzwa Zanzibar utozwe VAT kwa kiwango cha asilimia
sifuri.
“Kwa hiyo madeni yatakayokuwa yanadaiwa
kwa Zanzibar ni yale madeni ya kulipia umeme, umeme wametumia kiasi fulani
wanalipa kama wanavyolipa wa maeneo mengine kwa mfano wanavyolipa Dar es salaam,
suala la kutoza VAT sasa halipo na katika hilo kwa sababu kulikuwa na deni
ambalo lilikuwa limefika shilingi Bilioni 22.9, sisi Baraza la Mawaziri
tutapeleka mapendekezo Bungeni kwamba lisamehewe kwa sababu lipo ndani ya
bajeti ya mwaka huu wa 2018/2019, kwa hivyo litapunguza mapato yatakayotakiwa
kukusanywa na serikali”, amesema Rais
Magufuli.
Kwa upande wake Dkt Shein amesema kuwa pamoja
na kuridhia utozaji wa VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri, Baraza la Mawaziri
pia limekubaliana kuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ataitisha vikao vya
kuzungumzia masuala ya Muungano kila mara kunapokuwa na hoja ya masuala ya
Muungano ili kujadili na kutoa uamuzi.
“Tungependa sana mambo haya yafanyike
vizuri kwa sababu pande mbili za Muungano zinatuhusu sote, hili ni muhimu kwa
sababu mambo yakikusanyika mengi wananchi wanahisi hatusaidii jitihada zao, kwa
hivyo tumeridhia kuwa masuala ya Muungano ambayo yapo chini ya Makamu wa Rais,
wakae pamoja wayajadili ili yapate uamuzi wa pande zote mbili” amesema Dkt
Shein.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemuapisha Anjella Kairuki kuwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji.
Kairuki ameapishwa kabla ya kuanza kwa
kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, kufuatia mabadiliko madogo yaliyofanywa na
Rais Magufuli Januari Nane mwaka huu ambapo Kairuki aliyekuwa Waziri wa Madini
aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji.
Mchezaji wa zamani wa klabu ya Everton ya
England, – Steven Pienar anatarajiwa kuendesha programu maalumu za michezo kwa
timu za vijana za mpira wa miguu nchini.
Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa
SportPesa Tanzania, – Tarimba Abbas amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es
salaam kuwa Pienar atakuwepo nchini wakati wa michuano ya kombe la SportPesa
ambapo ataitumia fursa hiyo kuendesha programu hizo ikiwemo kufanya mazoezi na
timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Akizungumzia mashindano hayo ya kombe la
SportPesa ya mwaka huu, Tarimba amesema kuwa ili kuendana na ushindani
unaoonyeshwa na timu kutoka nchini Kenya, wameamua kuendesha mashindano hayo
katikati ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuzipa nafasi timu za Tanzania
kuonyesha ushindani.
Nao viongozi wa Mashirikisho ya nchi
zinazotoa timu shiriki kwenye mashindano hayo wamezitaka timu zao kuonyesha
ushindani.
Mashindano hayo ya kombe la SportPesa
yanaanza kutimu vumbi Jumanne Januari 21 ambapo timu Nane kutoka Tanzania na
Kenya zitachuana.