Ajali yaua wanne Kigoma

0

Watu wanne wamekufa na wengine  43 wamejeruhiwa  baada ya basi mali ya kampuni ya  Fikoshi Investment  lililokua likisafiri kutoka mkoani Mwanza kuelekea mkoani Kigoma kuacha  njia na kupinduka katika eneo la Mnarani wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Kamanda wa polisi wa  mkoa wa Kigoma, – Martin Ottieno amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyohusisha basi lenye namba za usajili  T 400 AUV.

Kamanda Ottieno amesema kuwa miili ya watu hao wanne waliokufa kwenye ajali hiyo,  imehifadhiwa katika kituo cha afya cha Uvinza na majeruhi wote katika ajali hiyo wamelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma, – Maweni kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kufuatia ajali hiyo, Kamanda  Ottieno ameendelea kutoa wito kwa madereva wa vyombo  vya moto mkoani Kigoma,  kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka matukio ya ajali yanayoweza kuepukika.

Viongozi wa dini washauriwa kuhimiza mafundisho yenye maadili

0

Askofu Mkuu wa Kanisa la full Gospel Bible Fellowship, – Zachary Kakobe ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuhimiza mafundisho yenye maadili kwa  waumini wao, mafundisho ambayo pamoja na mambo mengine yatasaidia kuondoa vitendo vya rushwa.

Askofu Kakobe ametoa kauli hiyo katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachotangazwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakati akielezea mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya Taifa.

Aidha Askofu Kakobe ametoa wito kwa Wanasiasa nchini kuheshimu mamlaka iliyopo madarakani na kutoa ushirikiano kwa Rais John Magufuli ili kudumisha amani na utulivu nchini.

Pia amezishauri taasisi za dini  nchini kuwa mfano kwa jamii katika kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule.

Mwanamuziki Mtukudzi afariki dunia

0

Mwanamuziki maarufu nchini Zimbabwe, Oliver Mtukudzi amefariki dunia katika Hospitali moja mjini Harare alikokuwa akipatiwa matibabu kwa takriban mwezi mmoja.

Katika uhai wake Mtukudzi amefanya ziara kwenye nchi mbalimbali duniani na kujizolea mashabiki wengi ambapo na kutoa albamu zaidi ya 60.

Amekuwa katika muziki kwa zaidi ya miaka 40 na kukuza vipaji vya wanamuziki nchini Zimbabwe.

Halikadhalika Mtukudzi ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Balozi wa heshima wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto – UNICEF.

Mtukudzi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66.

Viongozi wa dini wamuomba Rais kuingilia kati michezo ya kubahatisha

0

Kiongozi wa dhehebu la Mabohora nchini Zainul Adam Jee amemuomba Rais Dkt John Magufuli kutolea tamko michezo ya kubahatisha maarufu kama betting ambayo amesema inadhoofisha nguvu kazi ya taifa na hasa vijana.

Akizungumza katika mkutano wa Rais Dkt Magufuli na viongozi wa dini Adam Jee michezo hiyo ambayo inashika kasi nchini inasababisha vijana wengi ambao ndio kazi ya taifa kuwa wavivu.

“Vijana wengi wameacha kufanya kazi na badala yake wanatumia muda wao mwingi kucheza michezo ya kubahatisha ambayo haina maana sana kwao.”alisema Adam Jee

Ameongeza kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa watu wataacha kufanyakazi kwa bidii kama unavyoagiza na kuona kama michezo hiyo ndio chanzo cha kuwapatia kipato.

Serena aondolewa katika mashindano ya wazi ya Australia

0

Katika michuano ya wazi ya tenesi ya Australia inayoendelea  mjini Melbourne mchezaji Serena Williams  amefungwa na Karolina Pliskova kwa seti mbili kwa moja ya   6-4, 4-6, 7-5 .

Naye bingwa wa michuano ya wazi wa Marekani, Naomi Osaka  kutoka Japan  kwa sasa amefanikiwa kuingia hatua ya  nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kumfunga Elina Svitolina kwa seti mbili kwa bila ya  6-4 6-1.

Michezo ya Robo fainali inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mchezo wa tenesi duniani itwakutanisha Raonic dhidi ya  Pouille Novack Djokovic dhidi ya  Nishikori.

Rais Dkt John Magufuli akutana na viongozi wa dini

0

Rais Dkt John Magufuli  anakutana na viongozi  wa madhehebu mbali mbali  ya dini hapa nchini Ikulu  Jijini Dar es salaam ambapo amewashukuru kwa kuendelea kuliombea Taifa.

Rais Dkt Magufuli amesema  ana imani kuwa maombi ya viongozi hao wa dini yamewezesha Tanzania kubakia katika amani na upendo.

Rais Magufuli amesema ameamua kukutana na viongozi wa dini mwanzoni mwa mwaka ili kwa pamoja washauriane katika maswala mbalimbali kwa mustakabali mpana wa maendeleo ya taifa.

“Najua naweza kupata mawazo na ushuri mzuri wa kufanyia kazi kwa kipindi hiki cha uongozi wangu”alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ateta na Wadau wa madini

0

Rais John Magufuli amesema kuwa  yupo tayari kupeleka hati ya dharura katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya kodi mbalimbali wanazotozwa wafanyabiashara wa madini,  endapo wafanyabiashara hao watatoa mapendekezo yatakayosaidia kuongeza makusanyo katika sekta hiyo.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, mkutano uliokuwa na lengo ya kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji hao na namna ya kuzitatua.

Ametoa kauli hiyo baada ya wafanyabiashara hao wa madini kulalamika kuwa kumekuwa na kodi nyingi katika biashara ya madini,  jambo linalosababisha baadhi yao kukwepa kodi.

Awali wakati wa mkutano huo, Rais Magufuli alitoa nafasi kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano huo  kutaja changamoto zinazowakabili ambapo alitumia takribani saa sita kusikiliza changamoto hizo.

Wakitaja changamoto zao, baadhi ya Wadau hao wa sekta ya madini nchini  wameishauri serikali  kuondoa kodi mbalimbali ambazo zimekua zikiwaumiza wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mkutano huo unaoshirikisha wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini, utaendelea Jumatano Januari 23 mwaka huu  ambapo yanatarajiwa kufanyika majadiliano mbalimbali yenye lengo la kuboresha sekta ya madini nchini.

Makamanda watatu wa polisi wahamishiwa Makao Makuu

0

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini  Simon Sirro, amefanya mabadiliko ya Makamanda wa polisi kwa mikoa mitatu hapa nchini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Uhusiano cha Jeshi la polisi nchini Makao Makuu imesema kuwa, Makamanda walioguswa na mabadiliko hayo ni wa mikoa ya kipolisi ya Ilala,- Salum Hamdun, Temeke,  Emmanuel Lukula na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, -Ramadhani Ng’anzi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makamanda hao wote  watatu wamehamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola dhidi yao.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Makamanda wapya wa polisi wa mikoa hiyo watateuliwa hivi karibuni.