Idadi ya watu waliokufa baada ya kuvunjika
kwa kingo za bwawa moja la maji lililopo kwenye mgodi mkubwa wa chuma wa Vale
nchini Brazil imeongezeka na kufikia 58.
Watu wengine zaidi ya mia tatu,
wengi wao wakiwa wafanyakazi wa mgodi huo uliopo kwenye jimbo la Minas
Gerais Kusini Mashariki mwa Brazil
hawajulikani walipo.
Mpaka sasa vikosi vya uokoaji
nchini Brazil ambavyo vimekua vikitumia helikopta 13, vimeshindwa kuwapata watu ambao awali
walidhaniwa kuwa wako hai.
Kwa mujibu wa idara ya Zimamoto
nchini Brazil, takribani watu elfu 24 wamehamishwa
kutoka kwenye nyumba zao zilizopo katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo la Minas Gerais
kufuatia kuwepo kwa wasiwasi wa kutokea kwa madhara zaidi.
Serikali imefuta kodi ya pango ya
ardhi kwa taasisi na madhehebu ya dini nchini kuanzia mwaka wa fedha wa
2018/2019.
Hatua hiyo imetangazwa jijini Mbeya na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, – William Lukuvi wakati wa ibada ya kuwaweka Wakfu viongozi wa Jumuiya
Kuu ya Kanisa la Kibaptisti Tanzania (BCT).
Akitangaza hatua hiyo, Waziri Lukuvi
amesema kuwa Rais John Magufuli ameiagiza wizara hiyo kutoyatoza
kodi madhehebu ya dini kwa sehemu ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kufanyia
ibada.
“Rais ameagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu wa fedha, madhehebu ya dini yasilipe kodi ya ardhi kwa
maeneo ambayo huduma za maombi na ibada zinatolewa, hata hivyo msamaha huu
hauhusu maeneo ambayo kuna miradi ya kuingiza fedha ambayo tunajua madhehebu
mengi yameanzisha,” amesema Waziri Lukuvi.
Amefafanua kuwa tayari agizo hilo limetolewa kwa Makamishna wa ardhi wa kanda
na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa majiji, manispaa na halmashauri zote nchini.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi ametoa nafasi
ya kukutana na viongozi wa dini ambao wana migogoro ya ardhi kwenye maeneo
ambayo wanatoa huduma.
“Najua kuna migogoro mingi kwenye maeneo ambayo mnatoa huduma, hivyo nawakaribisha ofisini kwangu Dodoma na
kama migogoro itakuwa mikubwa nitafika mpaka eneo la mgogoro,” amesema Waziri
Lukuvi.
Awali, Askofu wa kanisa la Baptisti nchini, Arnold Manase alimweleza Waziri
Lukuvi kuwa kanisa hilo ni moja ya
madhehebu yanayoongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi.
“Kwa kuwa Waziri mwenye dhamana upo, naomba nafasi nije ofisini kwako
nikueleze migogoro iliyopo ndani ya kanisa langu ili uangalie namna ya kuitatua
maana migogoro imekithiri mpaka kufikia hatua ya kujenga makundi miongoni mwa
waumini,” amesema Askofu Manase.
Vikosi vya uokoaji nchini Brazil vinaendelea kuwatafuta watu walionusurika kufuatia kuvunjika kwa kingo za bwawa moja la maji lililopo kwenye mgodi mkubwa wa chuma wa Vale.
Takribani watu 200 hawajulikani walipo kufuatia tukio hilo lililotokea kwenye jimbo la Minas Gerais.
Habari kutoka nchini Brazil zinasema kuwa maji yaliyochanganyika na tope yamewafunika ardhini mamia ya wafanyakazi wa mgodi huo wa chuma.
Gavana wa jimbo la Minas Gerais, – Romeu Zema amesema kuwa, kuna wasiwasi huenda wafanyakazi wengi wa mgodi huo wa chuma wa Vale wamekufa katika tukio hilo na kwamba mpaka sasa ni watu Tisa tu ndio waliothibitika kufa.
Barabara nyingi za kuingia na kutoka katika mgodi huo mkubwa wa chuma zimeharibiwa na maji yaliyotoka kwa kasi kwenye bwawa hilo, na kufanya kazi ya uokoaji kuwa ngumu.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter,
Rais Jair Bolsonaro wa Brazil amelitaja tukio hilo kama janga la kitaifa na kuongeza kuwa serikali yake inafanya kila linalowezekana ili kuwaokoa watu walionusurika.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania -TBC, Tido Mhando ameachiwa huru baada ya kukutwa hana hatia dhidi ya kesi iliyokuwa ikimkabili ya matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha hasara ya zaidi ya Shilingi Miloni Mia Nane.
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Wilbard Mashauri amesema hakuna ushahidi unaoonyesha mikataba hiyo kusainiwa na Mwanasheria Mkuu wa mwanasheria mkuu wizara husika wala mjumbe yeyote wa Bodi ya TBC.
Hakimu Mashauri amesema mikataba ya serikali ni lazima ihusishe ofisi ya mwanasheria mkuu na taasisi zinazohusika na kwa kesi ya TBC mikataba hiyo haikukidhi vigezo vya kuwa mikataba na hakuna ushahidi unaonyesha mwendelezo wa kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya Channel Two Jijini London
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa .
Amesema hospitali hiyo itakayosaidia serikali kuboresha huduma za afya kwa kuongeza idadi ya madaktari bingwa Mkoani Shinyanga na kuweza kukabiliana na tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga mkoani humo.
Hata hivyo Waziri Ummy ameeleza kuwa halmashauri ya manispaa ndiyo itakayokuwa na jukumu la kusimmamia miundombinu ya hospitali hiyo mara itakapokmalika.
Aliyewahi kuwa Naibu Waziri kwenye wizara
mbalimbali nchini, -Shamim Khan ametunukiwa tuzo ya juu ya heshima (Pravasi
Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, -Ram Nath Kovind.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari
na wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kuwa, tuzo hiyo imetolewa
wakati wa mkutano wa 15 wa Diaspora wa India
uliofanyika kwenye mji wa Varanasi uliopo katika jimbo la Uttar
Pradesh nchini India Januari 23 mwaka
huu.
Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana
na mchango wake mkubwa kwa jamii hususani katika masuala ya akina mama, pamoja
na kudumisha amani na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini
Tanzania.
Akizungumza wakati akimtunuku tuzo hiyo,
Rais Kovind wa India amesema kuwa Shamim
Khan pia amefanya kazi kubwa katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya
Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na serikali ya
Tanzania, hali iliyosaidia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya
nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Shamim Khan amemshukuru
Rais Kovind kwa kumtunuku tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwake.
Pia ameipongeza serikali ya India kwa
kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina yake na
Tanzania na amemuomba Rais Kovind
kuendelea kusaidia juhudi za serikali iliyo chini ya Rais John Magufuli katika
kuwaletea maendeleo watanzania.
Tuzo hiyo ya juu ya heshima hutolewa na Rais wa
India kwa raia wenye asili ya nchi hiyo ambao wamekua wakitoa mchango mkubwa
katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India.
Watu mbalimbali wakiwemo wasanii wameendelea kutuma
salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wa Mwanamuziki maarufu wa nchini
Zimbabwe na Afrika, – Oliver Mtukudzi kufuatia kifo cha mwanamuziki huyo.
Baadhi ya wasanii hao ni wale wanaounda kundi la Sauti Sol la nchini Kenya na Daniel Mhlanga.
Mtukudzi amefarika dunia Januari 23 mwaka huu katika hospitali moja mjini Harare akiwa na umri wa miaka 66.
Habari zaidi kutoka mjini Harare
zinasema kuwa Mtukudzi
amekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo kwa takribani mwezi mmoja.
Katika siku za hivi karibuni, msanii huyo alilazimika
kufuata baadhi ya ziara zake za muziki katika nchi mbalimbali duniani, kutokana na kuugua.
Muziki wa mwanamuziki huyo wa Zimbabwe, -Oliver Mtukudzi
unafahamika kuwa ni wa miondoko ya Afro-Jazz na umevuka mipaka na kupata
mashabiki wengi kote duniani.
Mtukudzi amekuwa katika taaluma ya muziki kwa zaidi ya
miongo mine na kufanikiwa kutoa albamu 67.
Albamu ya mwisho ya
Mtukudzi imeangazia hali ya kisiasa ilivyo hivi sasa nchini Zimbabwe na matatizo mengine
ya kijamii.
Jumla ya watahiniwa 322, 965 ambao
ni sawa na asiliamia 78.38 ya watahiniwa 426,988 waliofanya mtihani wa kidato
cha nne mwaka 2018 wamefaulu mitihani yao.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA) Dakta Charles Msonde amesema kuwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi
kimeongezeka kutoka asilimia 77.09 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 78.38 mwaka
2018.
Dkt Msonde amezitaja shule kumi
zilizofanya vizuri ambazo zina idadi ya watahiniwa zaidi ya arobaini kuwa ni St
Francis Girls ya mkoani Mbeya, Kemebos ya mkoani Kagera, Marian Boys ya mkoani
Pwani, Ahmes ya mkoani Pwani, Canossa ya mkoani Dar es salaam, Maua Seminary ya Kilimanjaro, Precious Blood ya mkoani
Kilimanjaro, Marian Girls ya mkoani Pwani,
Bright Future Girls ya mkoani Dar es salaam na Bethel Sabs Girls ya
mkoani Iringa.
Shule zilizofanya vibaya katika
mtihani huo ni Pwani Mchangani ya Kaskazini Unguja, Ukutini ya Kusini Pemba,
Kwediboma ya mkoani Tanga, Rwemondo ya mkoani Kagera, Namatula ya mkaoni Lindi,
Kijini ya Kaskazini Unguja, Komkalakala ya mkoani Tanga, Kwizu ya mkoani
Kilimanjaro, Seuta ya mkoani Tanga na
Masjid Qubah Muslim ya mkoani Dar es salaam.
Dkt Msonde ameongeza kuwa hali ya
ufanyikaji wa mtihani huo wa kidato cha nne nchini mwaka 2018 ni nzuri kwa kuwa
ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu na kwa kuzingatia kanuni za
mitihani.
Hata hivyo amesema kuwa shule ya
sekondari ya Tumaini Lutheran Seminary
iliyopo wilayani Malinyi mkoani Morogoro
imefutiwa matokeo ya watahiniwa wote, pamoja na kufungwa kwa kituo hicho kutokana na
kufanya udanganyifu.