Rais
John Magufuli amewaapisha Majaji wa Mahakama ya Rufani na wengine wa Mahakama
Kuu aliowateua hivi karibuni na kusema kuwa kazi ya kusimamia haki ina
changamoto kubwa, hivyo majaji hao wanatakiwa wamtangulize Mwenyezi Mungu
katika kutekeleza majukumu yao.
Wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Ikulu
Jijini Dar es salaam, Rais Magufuli pia ameshauri Majaji hao wapya kuzingatia
sheria pamoja na katiba ya nchi katika utendaji kazi wao wa kila siku hasa katika kuwahudumia Watanzania ambao wengi wao wamekua walikosa haki yao ya
kisheria.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ataendelea
kuteua Majaji wengi zaidi kadri bajeti
itakavyoruhusu kwa kuwa bado mahitaji ya Majaji hao ni makubwa.
Kwa upande wa Wakuu wapya wa wilaya za Tarime
mkoani Mara na Mwanga mkoani Kilimanjaro ambao nao amewateua hivi karibuni
pamoja na Wakuu wengine wa wilaya nchini, Rais
Magufuli amewaagiza kutotumia madaraka yao vibaya na kuacha tabia ya kuwaweka watu ndani pasipo kuzingatia utaratibu
kama inavyofanywa hivi sasa na baadhi yao.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alipata
fursa ya kuzungumza wakati wa hafla hiyo, ambapo Majaji Sita wa Mahakama ya Rufani na
wengine Kumi na Watano wa Mahakama Kuu
wameapishwa, huku wakuu wa wilaya mawili na Wakurugenzi Kumi wa halmashauri za
wilaya wamepatiwa maelekezo ya kikazi na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi
wa umma.
Akizungumza na watendaji hao, Makamu wa
Rais ameelezea furaha yake kutokana na ongezeko la Majaji wanawake na kuwataka
kufanya kazi huku wakiyatazama kwa ukaribu makundi mbalimbali ambayo yamekua
yakilalamika kukosa haki.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma ametoa wito kwa majaji hao wapya kufanya kazi kwa kujituma na kwa haraka ili
kuweza kushughulikia mashauri mengi zaidi.
Ameelezea matumaini yake kuwa Majaji hao wapya
watatenda haki na kutoruhusu malalamiko ya aina yoyote.
Majaji wa Mahakama ya Rufani walioapishwa
katika hafla hiyo ni Sahel Barke, Jaji Mary Levira, Jaji Rehema Sameji, Jaji Winnie Korosso, Jaji Ignus Kitusi na Jaji
Lugano Mwandambo.
Majaji walioapishwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu ni pamoja na Cyprian Mkeha, Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji Mwinshehe
Kulita, Jaji Ntemi Kilikamajenga, Jaji Zepherine Galeba na Jaji Juliana Masabo.
Majaji wengine walioapishwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu ni Mustapha Ismail, Jaji
Upendo Madeha, Jaji Willbard
Mashauri, Jaji Yohane Masara, Jaji Lilian Mongella, Jaji Fahamu Mtulya, Jaji John Kahyoza, Jaji Athumani Kirati na Jaji Susan Mkapa.
Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya
walioteuliwa ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi ni pamoja na Isaya Mbenje
anayekwenda halmashauri ya Pangani, Dkt
Fatuma Mganga halmashauri ya Bahi,
Regina Bieda, -Tunduma, Jonas Mallosa halmashauri ya Ulanga, Ally Juma Ally
anayekwenda Njombe na Misana Kwangura halmashauri ya Nkasi.
Wengine ni Diodes Rutema halmashauri ya
Kibondo, Netho Ndilito halmashauri ya Mufindi, Elizabeth Gumbo halmashauri ya
Itilima na Stephen Ndaki anayekwenda halmashauri ya Kishapu.
Wakuu wapya wa wilaya ni Charles Kabeho
aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Tarime mkoani Mara na Thomas Apson ambaye
anakua mkuu wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.