Taa za sola pamoja na jenereta ruksa

0

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ameagiza wavuvi wanaotumia taa za sola pamoja na jenereta kwa ajili ya shughuli za uvuvi wasikamatwe mpaka hapo utakapoandaliwa utaratibu mwingine.

Waziri Mpina ametoa agizo hilo Bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Amesema kuwa Julai Mosi mwaka huu, serikali itatoa maelekezo zaidi kuhusu matumizi ya vifaa hivyo na kwamba haikusudii kuzuia matumizi ya taa hizo za sola pamoja na jenereta kwa Wavuvi kwenye maeneo mbalimbali nchini.  

Naye Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile ameliambia Bunge kuwa serikali ina mpango wa kuweka huduma ya kipimo cha  CT SCAN katika hospitali za mikoa mbalimbali nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, – January  Makamba naye amepata nafasi ya kujibu swali bungeni Ijumaa Februari Mosi na kuwataka Wakazi wa Zanzibar kuandika anwani sahihi pindi wanapoomba na kupata ajira katika taasisi za Muungano, lengo likiwa ni kufahamu uwiano wa watendaji katika taasisi hizo kwenye pande zote za Muungano.

Newcastle yavunja rekodi ya usajili

0

Timu ya Newcastle United ya nchini England imevunja rekodi yake ya usajili kwa kumsajili kiungo mchezeshaji Mparaguay Miguel Almiron kutoka timu ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), -Atlanta United kwa kitita cha Paundi Milioni 20.

Usajili huo umevunja rekodi ya usajili wa Michael Owen ambapo timu hiyo ya ST James Park ilitumia kiasi cha Paundi Milioni 16 mwaka 2005.

Almiron mwenye umri wa miaka 24 alifunga magoli 13 msimu uliopita na kuisaidia Atlanta United kutwaa ubingwa wa Marekani.

Kiungo huyo Mchezeshaji ameshawahi kucheza kwenye timu za Cerro Porteno ya nyumbani kwao Paraguay na Lanus ya Argentina.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha usajili huo, Almiron amesema kuwa amefurahi kujiunga na Newcastle United, klabu yenye historia kubwa.

Newcastle United pia imemsajili mlinzi Antonio Barreca kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu kutoka timu ya Monaco ya nchini Ufaransa.

Barafu yaikosesha ushindi Liverpool

0

Kocha wa timu ya Liverpool ya nchini England, -Jurgen Klopp amesema kuwa kudondoka kwa barafu kwenye uwanja wa Anfield kulisababisha timu yake kukosa ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Leicester City.

Kocha huyo Mjerumani amesema kuwa mchezo  huo haukwenda vizuri kama walivyokuwa wanataka na kwamba endapo wangeshinda wangeongeza pengo la pointi na kuwa  Saba dhidi Manchester City.

Kabla ya mchezo huo kati ya Liverpool  na Leicester City, wahudumu wa uwanja huo wa Anfield walilazimika kutoa parafu iliyodondoka, kitu ambacho kocha Klopp amesema kuwa kilikuwa ni kikwazo kwao.

Wakati wa kipindi cha mapumziko, wahudumu walirudi tena kutoa barafu zilizodondoka kwenye uwanja huo, lakini barafu zingine hazikutoka hasa zile zilizodondoka wakati mchezo ukiendelea.

Mke wa Mufti azikwa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaongoza mamia ya waombolezaji kwenye mazishi ya mke wa Mufti wa Tanzania Abubakar Zubeiry, – Mama Shafi, mazishi yaliofanyika wilayani Korogwe mkoani Tanga.


Akitoa salamu wakati wa mazishi hayo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, serikali itaendelea kuwaunga mkono viongozi wote wa dini katika kipindi chote kiwe cha raha ama shida.


Kabla ya Waziri Mkuu kutoa salamu hizo, dua ilisomwa na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu.
Mke wa Mufti wa Tanzania alifariki dunia Januari 30 mwaka huu wilayani Korogwe.

Makamu wa Rais ateta na Mabalozi

0

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi kutoka nchi Tatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.


Mabalozi hao ni pamoja na Gaber Mohamed Abulwafa ambaye ni Balozi mpya wa Misri nchini na alifika kwa Makamu wa Rais kwa lengo la kujitambulisha na pia kuzungumzia mambo mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.


Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Balozi huyo mpya wa Misri nchini amemueleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha sekta za Elimu, Afya na Miundombinu.


Kwa upande wake Makamu wa Rais amemuhakikishia Gaber ushirikiano mzuri katika kazi zake akiwa nchini, na kumueleza kuwa kwa miaka mingi uhusiano kati ya Misri na Tanzania umezidi kuimarika na kuwa na manufaa.


Balozi mwingine aliyekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais ni Francisca Pedros ambaye ni Balozi mpya wa Hispania nchini, ambapo Makamu wa Rais amempongeza kwa kuwa Balozi wa kwanza mwanamke kuteuliwa kuitumikia nchi yake hapa nchini.


Naye Yonas Yosef Sanbe ni Balozi mpya wa Ethiopia nchini na katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, anafarijika kuona uhusiano wa Ethiopia na Tanzania unaendelea kuimarika.


Makamu wa Rais pamoja na mambo mengine, amempongeza Balozi huyo mpya wa Ethiopia nchini kwa kuwa wa kwanza kuwa na makazi yake Tanzania.

NMB kukuza sekta ya maziwa

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Profesa Elisante Ole Gabriel, ameitaka Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa.

Profesa Ole Gabriel ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa kikao na maafisa kutoka idara ya kilimo ya Benki ya NMB waliofika ofisini kwake kwa lengo la kumwelezea mikakati ya benki hiyo ambayo imekuwa ikifanya tafiti ili kuwekeza katika sekta hiyo ya maziwa.

“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ni kwamba, kwa wastani angalau mtu MMOJA anatakiwa walau atumie lita Mia Mbili za maziwa kwa mwaka, lakini kwa bahati mbaya kwa Watanzania wastani ni lita 47 tu, bado tuna kazi kubwa sana,” amesema Profesa Ole Gabriel.

Amesema kuwa Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia dawati la sekta binafsi, ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa yanatumika ipasavyo.

Katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Ole Gabriel ameongeza kuwa wakati umefika kwa Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji, hasa wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo, – Carol Nyagaro amesema kuwa kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali, imeilazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja wapya kupitia sekta mbalimbali.

“Kutokana na kasi ya Mheshimiwa Rais John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo,” amesema Ngayaro.

Amesisitiza kuwa Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo, inafikiria pia kuwekeza katika sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi karibuni.