Pellegrini kuisaidia Man City

0

Kocha wa timu ya West Ham United, -Manuel Pellegrini amesema anataka kuifunga Liverpool ili kuisaidia timu yake ya zamani ya Manchester City kwenye harakati za kuusaka ubingwa wa Ligi Kuu ya  England.

Februari Tatu mwaka huu, Manchester City iliifunga Arsenal na hivyo kupunguza pengo la alama kufikia mbili  dhidi ya Liverpool huku Liverpool wakiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi West Ham United.

Pellegrini raia wa Chile alishinda ubingwa wa England mwaka 2014 akiwa kocha wa Manchester City na amesema kuwa kama wakishinda itakua ndio furaha yake.

West Ham United ipo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England na katika mchezo wake wa hivi karibuni itamkosa mlinzi wake Winston Reid ambaye anauguza jeraha la goti kwa muda wa mwaka mmoja.

Mabaki ya ndege iliyombeba Emiliano yaonekana

0

Mabaki ya ndege iliyopotea ambayo ilimbeba mchezaji wa timu ya Cardiff City, -Emiliano Sala yameonekana kwenye Pwani ya Uingereza.

Ndege hiyo iliyokuwa ikitoka nchini Ufaransa kwenda nchini Uingereza ilipotea Januari 21 mwaka huu  ikiwa na watu wawili ndani, ambao ni mchezaji huyo Emiliano na David Ibbotson ambaye ni rubani.

Kiongozi wa kikosi kilichokua kikiitafuta ndege hiyo David Mearns amesema kuwa,  baada ya kuonekana kwa mabaki ya ndege hiyo, kazi inayofanyika hivi sasa ni kuendelea kuchunguza chanzo cha tukio la kupotea kwa ndege hiyo.

Emiliano alijiunga na Cardiff City kwa ada ya uhamisho ambayo ni rekodi kwa timu hiyo na wakati ndege hiyo inapotea alikuwa akitoka nchini Ufaransa kwenda nchini Uingereza kujiunga na timu hiyo baada ya kukamilisha uhamisho wake.

Mkutano wa wakuu wa EAC waendelea Arusha

0

Mkutano wa Ishirini wa kawaida wa Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea na kikao chake cha ndani  jijini Arusha.

Miongoni mwa Marais wanaoshiriki katika mkutano huo ni Dkt John Magufuli wa Tanzania, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda.

Habari kutoka jijini Arusha zinasema kuwa nchi za Burundi na Sudan Kusini zimetuma wawakilishi katika mkutano huo.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt Ally Kivejinja amesema  kuwa kikao hicho kitajadili agenda mbalimbali zenye maslahi kwa nchi wanachama ikiwemo kuimarisha ushirikiano na usalama.

PAC yawasilisha taarifa yake

0

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imewasilisha bungeni taarifa ya shughuli za kamati kwa mwaka 2018, taarifa  inayoonyesha mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchambuzi wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uhakiki wa mfuko mkuu wa serikali.

Akiwasilisha taarifa hiyo Mwenyekiti wa PAC, -Naghenjwa Kaboyoka amesema kuwa sababu ya tofauti ya Shilingi Trilioni Moja Nukta Tano katika ripoti ya mwaka ya CAG kwa mwaka 2016/2017 imetokana na kusanyo la Shilingi Trilioni 25.3 na fedha zilizotolewa na hazina Shilingi Trilioni 23.8 kama ilivyoripotiwa na CAG katika ripoti ya hesabu za serikali kuu iliyoishia Juni 30 mwaka 2017.

Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali pia imebainisha uwepo wa uwekezaji usiokuwa na tija uliofanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika ununuzi ya ardhi.

Mwenyekiti huyo wa PAC Naghenjwa Kaboyoka ameishauri serikali kuzifanyia kazi  kwa wakati hoja za ukaguzi zinazotolewa na CAG.

Kyela kudhibiti utoroshaji wa kokoa

0

Halmashauri  ya  wilaya  ya Kyela  mkoani  Mbeya  imesema kuwa   itaendelea  kudhibiti  utoroshaji  wa  kokoa katika halmashauri hiyo ili  kuongeza mapato.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti  wa  halmashauri  ya wilaya ya Kyela Dkt Hunter Mwakifuna mara  baada  kumalizika kwa kikao  cha  Baraza  la  Madiwani  la halmashauri hiyo kilichokua kikijadili mapendekezo ya bajeti  kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 .

Dkt Mwakifuna amesema kuwa tangu utoroshwaji huo wa kokoa kwenda nje ya wilaya hiyo Kyela kuanza kudhibitiwa mwaka 2017, mapato ya halmashauri hiyo yameongezeka kwa asilimia 90 hadi kufikia hivi sasa.

Kufuatia utoroshaji huo wa kokoa wilayani Kyela, Dkt Mwakifuna ametoa wito kwa wakulima wa zao hilo wilayani humo kuuza kokoa yao katika vyama vya ushirika, hatua ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia kuongeza mapato ya halmashauri ya wilaya hiyo.

Trump kukutana na Xi Jinping

0

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa atakutana na Rais  Xi Jinping wa China hivi karibuni kwa lengo la kutia saini makubaliano ya kina ya kibiashra kati ya nchi hizo.

Trump ametoa kauli hiyo jijini Washington baada ya mazungumzo yake na Makamu wa Waziri Mkuu wa China, –  Liu He, mazungumzo yaliyohusu masuala ya kibiashara baina ya mataifa hayo mawili.

Amesema kuwa ana imani kuwa mataifa hayo mawili yenye nguvu zaidi za kiuchumi duniani yatafikia makubaliano ya kibiashara ambayo ameyaita kuwa ni makubwa zaidi kuwahi kufikiwa.