Wiki ya Sheria yazinduliwa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na Idara ya Mahakama nchini ili kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Sheria, wiki ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza jijini humo baada ya serikali kuhamishia Makao Makuu yake.

Amesema kuwa serikali inafuatilia kwa karibu na kuzitatua changamoto zote zinazoikabili Idara ya Mahakama nchini, lengo likiwa ni kuhakikisha Wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma za kisheria.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Wiki ya Sheria ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini, hivyo ni vema ikatumika vizuri ili kufanikisha lengo la Idara ya Mahakama nchini la kumpatia haki kila mwananchi bila ubaguzi.

Ametoa wito kwa wataalamu wa masuala ya sheria nchini kutenga muda wao wa kuwasaidia Wananchi  kufahamu masuala ya kisheria kwa kuwa wengi wao wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo, jambo linalochangia baadhi yao kukosa ama kupoteza haki zao. 

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma   amesema kuwa kwa kipindi cha wiki nzima, maonesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika jijini Dodoma  na kwenye Mahakama zote kuanzia ngazi ya wilaya.

Amesema kuwa kupitia maonesho hayo, wananchi wengi watapata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali na kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.

Kila mwaka, Idara ya Mahakama nchini imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Sheria ambayo pamoja na mambo mengine hutoa fursa kwa Wananchi kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.

IGP afanya mabadiliko

0

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amefanya mabadiliko ya Makamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza na mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.

Taarifa iliyotolewa  jijini Dar es salaam kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini inaonyesha kuwa Makamanda walioguswa na mabadiliko hayo ni Mussa Taibu anayekwenda kuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.

Naye Muliro Jumanne aliyekua Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni  anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza  na aliyekua Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, -Jonathan Shana amehamishiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kitengo cha Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Nchini, mabadiliko hayo ni ya kawaida ya kiutendaji kwa Jeshi la Polisi.

Pellegrini amuelezea Klopp

0

Kocha wa West Ham United, – Manuel Pellegrini amesema kuwa kocha wa Liverpool, – Jurgen Klopp amezoea kushinda kwa mabao ya Offside, kauli aliyoitoa baada ya timu yake kutoka sare ya bao moja kwa moja na vinara hao wa Ligi Kuu ya England.

Sadio Mane alianza kuiandikia Liverpool bao la kuongoza katika dakika ya 22,  bao ambalo Pellegrini amesema kuwa James Milner alikuwa katika eneo la kuotea kabla ya kutoa pasi ya kufunga kwa Mane lakini mwamuzi msaidizi hakunyanyua kibendera, kabla ya Michail Antonio kuisawazishia West Ham katika dakika ya 28 akitumia vyema makosa ya safu ya ulinzi ya Liverpool.

Baada ya mchezo huo Pellegrini akakumbushia tukio la miaka Sita iliyopita ambapo Klopp akiwa kocha wa Borussia Dortmund waliinyuka Malaga iliyokuwa ikinolewa na Pellegrini mabao  matatu kwa mawili kwenye mchezo wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Barani Ulaya ambapo mabao mawili ya Dortmund katika dakika za mwisho yalikuwa ya Offside.

Pellegrini amesema kuwa kwenye mchezo huo wachezaji wanne wa Dortmund walikuwa katika eneo la kuotea umbali wa mita saba peke yao, lakini mwamuzi akakubali goli kitendo kilichojirudia kwenye mchezo wa siku ya Jumatatu dhidi ya Liverpool,  hivyo kocha Jorgen Klopp amezoa kushinda kwa mabao ya Offside.

Kwa upande wake Klopp amesema kuwa maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo Kevi Friend kwa kiasi kikubwa yameharibiwa na waamuzi wasaidizi, kwani hata yeye alisikia kuwa bao lao la kuongoza lilikuwa Offside lakini mwamuzi wa pembeni hakuashiria chochote zaidi ya kulikubali.

Kwa matokeo hayo,  Liverpool wanaendelea kusalia kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakifikisha alama 62 ikiwa ni alama Tatu tofauti na Manchester City walio na alama 59 katika nafasi ya pili na nafasi ya Tatu wapo Tottenham Hotspur wenye alama 57.

African Media Group mambo poa

0

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais John Magufuli amefanya ziara fupi ya kutemblea ofisi za kampuni ya African Media Group inayomiliki vituo vinne vya Televisheni na viwili vya Redio.

Akizungumza na Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa kampuni hiyo jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 42 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, Rais Magufuli amewapongeza wafanyakazi hao kwa utendaji kazi wao mzuri na kuwataka kufanya kazi kibiashara.

Rais Magufuli ameahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili kampuni hiyo ikiwemo ile ya uchakavu wa vifaa na majengo na kuahidi kununua vifaa vipya ili kuviwezesha vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kampuni hiyo ya African Media Group kuonekana nchi nzima.

Kuhusu ubovu na ufinyu wa jengo linalotumika hivi sasa, Rais Magufuli ameiagiza Menejimenti ya kampuni  hiyo pamoja na wafanyakazi kushirikiana ili kutafuta jengo katika sehemu watakayohitaji ili liweze kuandaliwa kama ofisi.

Akiwa katika ofisi hizo Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Milioni Mia mbili kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Camera ambazo zitasaidia kurahisisha utendaji kazi katika vituo mbalimbali vya televisheni vilivyo chini ya kampuni hiyo ya African Media Group, kampuni inayomilikiwa na CCM.

Ligi Kuu Soka Tanzania Bara kuendelea

0

Mzunguko wa 25 wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara unaendelea kuanzia katikati hadi mwishoni mwa juma hili,  kwa kuchezwa michezo kadhaa kati ya siku ya Jumatano na Jumamosi.

Singida United wakiwa kwenye dimba lao la nyumbani,  watawaalika vinara wa ligi hiyo Yanga kwenye mchezo utakaopigwa siku ya Jumatano Februari Sita.

Siku hiyo hiyo ya Jumatano itashuhudiwa michezo mingine miwili, ambapo JKT Tanzania watawaalika Biashara United ya Mara kwenye dimba la Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo,  huku matajiri Azam FC wakiwakaribisha Alliance FC kwenye uwanja wa Azam Complex.

Alhamisi Februari Saba,  itachezwa michezo miwili ambapo Coastal Union watapepetana na wazee wa kupapasa – Ruvu Shooting Stars huku bingwa mtetezi Simba ikimenyana na Mwadui FC kwenye dimba la Taifa jijini Dar es salaam.

Siku ya Ijumaa kutakuwa na mchezo mmoja sawa na Jumamosi ambapo Mtibwa Sugar watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Manungu mkoani Morogoro kukipiga na African Lyon huku JKT Tanzania wakiwa ni wenyeji wa Yanga kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Baba Mtakatifu Francis ziarani Uarabuni

0

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis yupo katika falme za Kiarabu kwa ziara ya kiserikali na kidini.

Hiyo ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani katika nchi za kiarabu na ameweza kuendesha misa mjini Abu Dhabi.

Kabla ya kwenda katika falme hizo za Kiarabu,  kiongozi huyo alielezea kusikitishwa na mauaji na kisiasa yanavyoendelea nchini Yemen na kutaka Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua ili kuwasaidia wananchi wanaoathiriwa na mapigano nchini humo.

Miongoni mwa mambo ambayo Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani Baba Mtakatifu Francis anatarajiwa kusisitiza katika mazungumzo na wenyeji wake kwenye Falme za Kiarabu ni kuimarisha umoja na amani miongoni mwa wakazi wa dunia.

Ajali ya ndege yaua Watano

0

Ndege ndogo ya abiria imeanguka katika makazi ya watu kwenye jimbo la California nchini Marekani na kusababisha vifo vya watu watano akiwemo rubani wa ndege hiyo.

Watu walioshuhudia ajali hiyo wamesema kuwa kabla ndege hiyo haijaanguka iligawanyika vipande na baadae kushika moto.

Wamesema kuwa walisikia kishindo kabla ya kuanguka kwa ndege hiyo na kisha mlipuko uliosababisha nyumba moja yenye ghorofa mbili kushika moto.

Watu wengine wawili wamejeruhiwa katika ajali hiyo ambayo imeanguka dakika chache baada ya kuruka kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Yorba Linda.

Mamlaka zinazohusika katika jimbo hilo la California zinaendelea na uchunguzi kujua sababu za kuanguka kwa ndege hiyo ndogo ya abiria.