UNHCR yaiomba radhi Tanzania

0

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), – Filippo Grandi Ikulu jijini Dar es salaam na kumhakikishia kuwa serikali itaendeleza ushirikiano na shirika hilo katika kutekeleza jukumu la kuhudumia wakimbizi.

Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kutoka nchi mbalimbali baada ya kutokea machafuko katika nchi hizo, na imekuwa ikiwapa hifadhi na kuwaruhusu watumie rasilimali za Watanzania licha ya wakati mwingine kutopata misaada kutoka Jumuiya ya Kimataifa.

Nchi yetu kwa sasa ina wakimbizi 350,000 waliopo katika maeneo mbalimbali wakiwemo Elfu 40 wa kutoka nchini Burundi, tunawapa hifadhi na wanatumia huduma za kijamii na miundombinu ya Watanzania katika maeneo wanayoishi, nimefurahi Grandi anasema tutaendelea kushirikiana na kwamba sasa wapo tayari kusaidia gharama za kuhudumia wakimbizi pamoja na jamii katika maeneo wanayoishi wakimbizi, maana tangu miaka kumi iliyopita UNHCR imekuwa ikiahidi kutoa fedha za kusaidia wakimbizi lakini haitekelezi ahadi zake”, amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo Rais Magufuli amesema kuwa pamoja na dhamira njema ya kuwapa hifadhi wakimbizi na kuwapa uraia baadhi yao, serikali inaendelea kuwahimiza kurejea makwao wakimbizi ambao katika nchi zao machafuko yamekwisha ili wakaungane na familia, ndugu, jamaa na kujenga nchi zao.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu huyo wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, -Filippo Grandi amemshukuru Rais Magufuli na serikali yake kwa kuendelea kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi kutoka nchi zenye matatizo mbalimbali na kuongeza kuwa UNHCR inatambua mchango mkubwa ambao kwa miaka mingi Tanzania inautoa kuwapa hifadhi na kuwahudumia wakimbizi kutoka kwenye nchi zinazoizunguka ambazo zimekuwa na machafuko ya mara kwa mara.

Grandi ameahidi kuwa UNHCR itahakikisha inatekeleza ahadi zake za kusaidia jukumu la kuwapa hifadhi wakimbizi, kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kubwa ya kuhudumia wakimbizi hao kwa kuvipatia teknolojia na vitendea kazi pamoja na kusaidia jamii katika maeneo yanayokaliwa na wakimbizi.

Aidha, Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR ameomba radhi kufuatia serikali ya Tanzania kukamata makontena yaliyoingizwa nchini yakiwa na nguo zinazofanana na sare za jeshi,  hali iliyolazimu nguo hizo kuchomwa moto na kubainisha kuwa jambo hilo halitajirudia.

“Ilitokea kampuni moja ya Japan ilitoa msaada wa nguo kwa ajili ya wafanyakazi wetu, nguo zile kwa bahati mbaya zilikuwa zinafanana kama sare za jeshi na tulizipokea ili tuzisambaze kwenye maeneo ambayo tunawahudumia wakimbizi, hili ni kosa hatukupaswa kufanya hivyo na hatujawahi kufanya hivyo, lakini wakati mwingine vitu hivi vinatokea, namuomba radhi Rais na namuahidi kuwa haitatokea tena”, amesema Grandi.

Rais Magufuli amempongeza Grandi kwa uungwana wake wa kuomba radhi kwa kitendo cha kuingiza nguo zinazofanana na sare za jeshi na amesema anaamini UNHCR haitarudia kufanya hivyo.

Mauaji Njombe, taarifa yatolewa Bungeni

0

Serikali imetoa taarifa rasmi Bungeni jijini Dodoma kuhusu matukio ya mauaji na utekaji nyara watoto mkoani Njombe ambapo hadi hivi sasa watoto  kadhaa wameuawa.

Akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, -Kangi Lugola amesema  kuwa tayari serikali imetuma makachero maalumu mkoani Njombe kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa matukio hayo.

Amesema  kuwa mpaka sasa watu Ishirini na Tisa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Waziri Lugola ameliambia Bunge kuwa, serikali inasikitishwa na matukio hayo ya mauaji na itahakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ya Nchi, – Kangi Lugola pia  ametoa  wito kwa wakazi wa mkoa wa Njombe na Watanzania wote,  kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola ili kukomesha vitendo hivyo vya mauaji ya watoto mkoani Njombe.

UNICEF yapata wasiwasi kuhusu watoto Iraq

0

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kuwa lina wasiwasi na usalama wa watoto wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Iraq, katika kipindi hiki ambapo nchi hiyo inaelekea katika msimu wa baridi kali.

Katika taarifa yake UNICEF imesema kuwa ina wasiwasi kuwa watoto wengi wanaweza kufa kwa baridi kali, kwani kambi hizo za wakimbizi haziwezi kuhimili hali hiyo ya baridi, ikizingatiwa kuwa katika siku za hivi karibuni Iraq ilikumbwa na mafuriko makubwa.

Mafuriko hayo yaliwaathiri wakimbizi wanaoishi kwenye kambi mbalimbali za wakimbizi nchini humo, ambao wamekuwa wakiishi kwenye mahema ya muda  ambayo hayawezi kuhimili mvua na baridi kali na watoto wakiwa katika hatari kubwa zaidi.

Guido alishutumu Jeshi

0

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela ambaye amejitangaza kuwa Rais wa serikali ya mpito ya nchi hiyo Juan Guido, amelishitumu jeshi la nchi hiyo  kwa kuendelea kumuunga mkono Rais Nicolas Maduro.

Guido amelishutumu jeshi la Venezuela kwa kuzuia misaada ya kibinadamu kwenye mipaka ya nchi hiyo ili isiweze kuingia nchini humo, ikiwemo ile ya dawa kwa ajili ya  kutibu binadamu.

Amesema kuwa anashangaa kuona jeshi la Venezuela bado linamuunga mkono Maduro, licha ya kutotambuliwa na Mataifa ya Magharibi ikiwemo Marekani.

Kiongozi huyo wa upinzani nchini Venezuela, – Juan Guido amesema kuwa nchi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa za binadamu na wagonjwa wengi wanazihitaji katika hospitali mbalimbali, lakini jeshi linaweka vizuizi katika maeneo ya mipaka.

Watendaji wa sekta ya sheria watakiwa kutenda haki

0

Rais John Magufuli amewataka Watendaji wa sekta ya sheria nchini kuendelea kufanyakazi kwa uaminifu na haki licha ya changamoto mbalimbali zilizopo.

Rais Magufuli ametoa wito huo jijini Dar es salaam wakati wa kilele cha maadhimisho siku ya sheria nchini, maadhimisho yanayoashiria kuanza kwa shughuli za Kimahakama kwa mwaka huu.

Amesema kuwa kuna baadhi ya Watendaji wa sekta ya sheria nchini si waaminifu na wamekua hawatendi haki wakati wa kutoa maamuzi mbalimbali na hivyo kuwakoseha Watanzania haki yao ya kupata huduma za kisheria.

Amewataka Watendaji hao kuepuka upendeleo wakati wa kutoa maamuzi na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika shughuli zao za kila siku.

Kuhusu upungufu wa Watendaji wa sekta ya sheria nchini, Rais Magufuli amesema kuwa tatizo hilo ni kwa sekta zote, hivyo iwekwe mikakati ya kutumia waliopo hadi hapo bajeti itakaporuhusu.

Ameipongeza idara ya Mahakama nchini kwa mafanikio mbalimbali hasa katika kupunguza mrundikano wa kesi na kuongeza mapato baada ya kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato hayo.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa Idara ya Mahakama imeendelea kupunguza mrundikano wa kesi katika mahakama mbalimbali nchini.

Profesa Juma amesema kuwa mrundikano huo wa kesi umepungua zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambapo kesi zimepungua kutoka 999 mwaka 2016 hadi kufikia 729 mwaka 2018.

Jaji Mkuu ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni nakala za hukumu za kesi zimeendelea kupatikana kwa wakati na kusisitiza wahusika kuendelea kutoa kwa wakati nakala hizo na bila malipo.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma, ifikapo mwezi Juni mwaka huu zaidi ya majengo Hamsini ya mahakama yatakua yamejengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli mbiu ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu ni Kutoa haki kwa wakati, wajibu wa mahakama na wadau.

Huduma ya mahakama inayotembea yazinduliwa

0

Rais John Magufuli amezindua huduma ya mahakama inayotembea, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini.

Mahakama hiyo inayotembea itaanza kutoa huduma kwenye mahakama za mwanzo katika mikoa ya Dar es salaam na Mwanza.

Huduma hiyo ya mahakama inayotembea inatolewa kufuatia changamoto ya kutokuwepo kwa huduma za kutosha za mahakama katika maeneo hayo na hivyo kuwanyima wananchi haki ya kupata huduma za kisheria.

Gari litakalotoa huduma hizo za mahakama inayotembea limegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 470.

Kauli mbiu ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu ni Tutoe haki kwa kwa wakati.

‘Nabii’ hatiani kwa kudai anatibu Ukimwi

0

Mahakama nchini Zimbabwe imemtia hatiani mchungaji mmoja kwa makosa ya kughushi na imemtoza faini ya Dola 700 za Kimarekani kwa kudanganya kwamba ana dawa ya mitishamba inayoponya Ukimwi.

Awali Nabii huyo Walter Magaya alikiri kosa la kukiuka sheria ya udhibiti wa dawa kwa kuuza dawa ambayo haijathibitishwa na mamlaka zinazohusika.

Alikamatwa na polisi mwezi Novemba mwaka 2018 ambapo pia alipatikana na kidhibiti cha dawa alichokuwa akidai kwamba inatibu watu wenye virusi vinavyosababisha Ukimwi na Ukimwi.

Magaya mwenye umri wa miaka 35, mwezi Oktoba mwaka 2018 alisema kuwa dawa yake inayoitwa Aguma ina nguvu za kimiujiza za kutokomeza virusi vinavyosababisha Ukimwi ndani ya siku 14 na kwamba dawa hiyo haina madhara yoyote kwa watumiaji.

Ndipo polisi nchini Zimbabwe walipovamia ofisini kwake na kumfanyia upekuzi, kwa tuhuma za uhalifu.

Kabla ya kupekuliwa alijaribu kuharibu baadhi ya vidhibiti kwa kuvitumbukiza chooni na kuchoma moto baadhi ya maboksi yenye dawa hizo, ambapo hata hivyo polisi walizipata zikiwa zimeungua nusu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, hadi mwaka 2016 watu milioni 1.3 walikuwa wakiishi na virusi vinavyosababisha Ukimwi nchini Zimbabwe.

Guterres azungumzia mgogoro wa Venezuela

0

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa  umoja huo hautajihusisha na jitihada zozote zenye lengo la kumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Venezuela.

Amewaambia Waandishi wa habari jijini New York nchini Marekani kuwa hatua hiyo si kwa nia mbaya, bali ni kuepuka kuonyesha upendeleo kati ya pande zinazovutana katika mgogoro huo.

Hata hivyo Guterres amesema kuwa Umoja wa Mataifa unaufuatilia mgogoro huo wa kisiasa nchini Venezuela kwa karibu kwa kuwa unaleta wasiwasi mkubwa.

Mataifa ya Mexico na Uruguay ambayo hayajatangaza kumtambua  Juan Guaido kama Rais wa mpito wa Venezuela yalikuwa na matarajio kwamba Guterres atashiriki katika mazungumzo yanayofanyika hii leo ambayo yana lengo la kunusuru hali ilivyo sasa nchini Venezuela.

Pamoja na mambo mengine, Wajumbe wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo walitarajiwa kuhamasisha kufanyika kwa majadiliano baina ya Guaido aliyejitangaza Rais wa Mpito wa Venezuela na Rais  wa sasa wa nchi hiyo Nicolas Maduro ili kuiondoa nchi hiyo kwenye mgogoro huo wa kisiasa.