Zama mpya tuzo za Ballon D’or

0
1967

Nyota wa mabingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita  Real Madrid wametawala kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya mchezaji bora duniani inayotolewa na jarida la mchezo wa mpira wa miguu nchini Ufaransa, –  Ballon D’or zitakazotolewa Disemba tatu mwaka huu jijini Paris.

Miamba hiyo ya soka barani Ulaya imeingiza wachezaji nane kwenye orodha hiyo wakiongozwa na Gareth Bale, Karim Benzema, Isco Marcelo, Thibaut Courtois, Sergio Ramos, Raphael Varane na mchezaji bora wa mwaka wa FIFA, – Luka Modric.

Awali, tuzo za Ballon d’Or zilikuwa zikijulikana kama FIFA Ballon d’Or,  lakini tangu Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) lijiengue kwenye tuzo hizo mwaka 2016 na kuanza kutoa za kwake kwa kujitegemea, jarida la Ballon d’Or nalo likaendelea na utoaji wa tuzo hizo kivyake.

Wachezaji wengine waliongia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hiyo kongwe ni pamoja na mshambuliaji wa England na klabu ya Tottenham Hot Spurs, – Harry Kane, winga wa Chelsea, –  Eden Hazard na Mshambuliaji wa Liverpool, – Mohamed Salah.

Wengine ni mshambuliaji wa Manchester City, – Sergio Aguero, mlinda mlago wa Liverpool, – Alisson Becker pamoja na washambuliaji wa timu hiyo  Sadio Mane na Roberto Firmino.

Manchester United imeingiza mchezaji mmoja tu kwenye orodha hiyo ambaye ni kiungo Paul Pogba pamoja na Wafaransa wenzake N’golo Kante anayekipiga kwenye klabu ya Chelsea na kipa wa Tottenham, –  Hugo Lloris.

Nyota Cristiano Ronaldo wa Ureno na Klabu ya Juventus aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Real Madrid atakuwa akitetea tuzo aliyotwaa mwaka 2017 pamoja na Lionel Messi, Antoine Griezmann, Kylian Mbape na Neymar.

Orodha hiyo inahitimishwa na Edinson Cavani, Diego Godin, Kevin De Bruyne, Mario Mandzukic, Jan Oblak, Luiz Suarez na Ivan Rakitic.