Yanga yatinga Mkoani Kigoma tayari kukabiliana na Simba

0
162

Timu ya Yanga imewasili alfajiri ya leo tarehe 22 Julai, mkoani Kigoma ikitokea Dar es salaam tayari kwa mtanange wa Fainali ya FA dhidi ya watani wao wa jadi SIMBA SC.

Wakizungumza na TBC viongozi na wachezaji wa Yanga wamesema wamejipanga kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo na wanatarajia matokeo mazuri kwa kuibuka na ushindi na kuwa mabingwa wa michuano ya FA.

“Kikosi cha wachezaji na timu ya ufundi takribani arobaini kimewasili salama, na sisi tumekuja kwa utulivu lengo ni kutumia nguvu ileile, kasi ileile, uwezo uleule kuhakikisha dakika tisini tunatoka na ushindi,”- amesema Antonio Nugaz.

Kwa upande wake mchezaji nafasi ya kiungo wa Yanga Zawadi Mauya amesema wachezaji wapo vizuri kuleta matokeo ya ushindi.

Kwa mara ya kwanza Magharibi mwa Tanzania mkoani Kigoma kunafanyika fainali ya kombe la shirikisho inayokutanisha watani wa jadi Simba na Yanga mwishoni mwa wiki hii siku ya jumapili.