Timu ya Yanga imetupwa nje ya michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja na timu ya Malindi, katika mchezo wa Kundi Be uliochezwa Januari 7 katika uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Bao la Yanga lilifungwa na mshambuliaji wake Matheo Anthony, huku yale ya Malindi yakipachikwa wavuni na Abdulsamad Kassim na Juma Hamad.
Kwa matokeo hayo, Malindi inafikisha alama saba baada ya kucheza michezo mitatu, ikishinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja ,huku Yanga ikibaki na alama zake tatu baada ya kucheza michezo mitatu, ikishinda mchezo mmoja na kupoteza michezo miwili.
Malindi inaungana na Azam fc iliyoshinda mabao mawili kwa moja mchezo wake dhidi ya Kvz na kufuzu hatua ya nusu fainali kutoka kundi Be, wakiungana na Simba kutoka kundi Aa, huku ikisubiriwa timu moja kutoka kundi Aa, kukamilisha idadi ya timu nne katika hatua hiyo ya nusu fainali.
Michuano hiyo ya 13 ya Kombe la Mapinduzi inaendelea kwa kuchezwa michezo mingine miwili ambapo Kmkm watacheza na chipukizi saa kumi na robo alasiri huku simba wakishuka dimbani saa mbili na robo usiku dhidi ya Mlandege.