Young Africans SC (Yanga) inatarajia kutambulisha mshambuliaji mpya iliyemsajili karibuni ikiwe ni mkakati wa kuendelea kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu mpya wa 2023/24.
Akizungumza kupitia kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji amesema walianza utambulisho wa mabeki, sasa wako eneo la katikati, na kabla ya Jumamosi watamtambulisha mshambuliaji mpya ambaye tayari wamemsajili.
Akijibu swali kama endapo usajili wa mshambuliaji huyo unamaanisha kuwa Fiston Mayele hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao, amesema klabu hiyo inajiimarisha kwa kuwa na kikosi kipana kutokana na wingi wa mashindano yaliyopo.
“Kumbuka una CAF Champions League, una ligi [Kuu ya NBC] una Azam Confederation Cup, una Mapinduzi Cup, kuna uwezekano kukawa na CECAFA vile vile, kuna karibia mashindano matano, unahitaji squad kubwa,” amesema Arafat.
Amesisitiza kuwa hakuna haja ya mashabiki wa timu hiyo kuwa na hofu kwani wachezaji wote wanaowataka wapo, na kwamba kutokuonekana kwa Mayele kwenye picha za wachezaji wakiwa mazoezini ni kutokana na klabu hiyo kuwa ndio inaamua umma uone nini.