Yanga Yalazimishwa Sare

0
1347

Wawakilishi wa Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika YANGA imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Zesco United ya Zambia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Matokeo ya sare nyumbani yanamaanisha kwamba Yanga inatakiwa kwenda kufanya ilichokifanya kwenye Raundi ya kwanza kushinda ugenini baada ya sare kama hiyo nyumbani na Towsnhip Rollers ya Botswana mwezi uliopita.

Goli la Yanga limefungwa kwa mkwaju wa penati kutoka kwa mchezaji Sibomana dakika ya 26 huku bao la kusawazisha la Zesco United likifungwa na Thabani Kamusoko katika 4 za nyongeza baada ya 90 za mchezo huo.

Timu hizo zitarudiana Septemba 27, mwaka huu mjini Ndola na mshindi wa jumla ataingia hatua ya makundi, wakati atakayefungwa ataangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.