Yanga yaelezea ushindi wake dhidi ya Mbao

0
836

Kocha wa timu ya Yanga,- Mwinyi Zahera amesema kuwa walijipanga tangu mapema kuvunja mwiko wa kufungwa na Mbao FC kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na  ndio maana wakapata ushindi wa mabao mawili kwa moja katika mchezo uliochezwa Jumatano Februari 20 mwaka huu.

Kocha huyo Mkongomani  amesema kuwa aliwaambia wachezaji wake mapema kutokuwa na mawazo ya kufungwa na Mbao FC na waende kupambana na walifanya hivyo na kuibuka na ushindi huo.

Katika mchezo huo Mbao walitangulia kufunga goli kupitia kwa mshambuliaji wake Mkongwe Ndaki Robert mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa Heriether Makambo.

Katika matokeo mengine ya michezo ya ligi kuu iliyochezwa siku hiyo ya Jumatano Februari 20 mwaka huu, moto wa Maafande wa Jeshi la Magereza nchini (Tanzania Prisons) katika kujinasua na janga la kushuka daraja,  umezidi kukoka baada ya kuinyoosha Mbeya City kwa bao Moja kwa Bila katika mchezo uliounguruma kwenye dimba la Sokoine.

Kwingineko nyota ya Mtibwa Sugar inazidi kufifia na sasa wamegeuka kuwa pombe ya ngomani, baada ya kukung’utwa bao Moja kwa Bila na KMC,  bao ambalo ni la  pekee kwa wakusanya mapato hao wa Manispaa ya Kinondoni na limefungwa na Sadala Lipangile.

Chama la Wana Stand United wakiwa nyumbani kwenye dimba la Kambarage mjini Shinyanga,  wameibuka na ushindi wa mabao Matatu kwa Mawili dhidi ya Wanapaluhengo kutoka Ngome ya Chifu Mkwawa Lipuli FC,  wakati Singida United wakikiona cha moto toka kwa Wanakuchele Ndanda FC katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Nangwanda Sijaona na kula mweleka wa mabao Mawili kwa bila.