Klabu ya soka ya Yanga, imewataka mashabiki wake kuhakikisha wanaingia uwanjani kwa wingi hasa ikizingatia wao ndo wenyeji wa mchezo ujao dhidi ya watani wao wa Jadi Simba Sc, mchezo ambao utapigwa Jumamosi Aprili 30,2022 katika dimba la Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Msemaji wa Klabu ya Yanga Haji Manara amesema mashabiki wa Yanga wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kwenye michezo kadhaa kwenye ligi hivyo amewataka kuendelea kujitokeza kushuhudia timu hiyo ikifanya vizuri kwenye ligi ya NBC ambapo Yanga inaongoza kwa tofauti ya alama 13.
“Tunakusudia kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba SC sisi kama wenyeji tuwe na Mashabiki wengi zaidi uwanjani na kutakuwa na Promotions nyingi kuelekea mchezo huu na Mashabiki wetu watafaidika sana na promotions hizo”. Amesema Haji Manara.
“Tutakuwa na Punguzo la bei Maalum ambapo Mshabiki wa Yanga utajipatia jezi ya msimu huu na tiketi ya Mzunguko kwa Shillingi 25,000 tu na pia tutakuwa na Punguzo Maalum kwa Jezi za Msimu uliopita na tiketi ya Mzunguko kwa shilingi 15,000 tu” ameongeza Manara
Mchezo wa mkondo wa pili wa mahasimu hao wa Dar es salaam unatarajiwa kupigwa Jumamosi wiki hii katika Dimba la Benjamin Mkapa ambapo katika mchezo wa mkondo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.