Waziri Mkuu akutana na Rais wa CAF

0
2220

Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) Ahmad Ahmad ameelezea kuridhishwa na maandalizi ya michuano ya Afrika ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Michuano hiyo ya mpira wa miguu kwa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 inatarajiwa kufanyika mwaka 2019 nchini Tanzania.

Akizungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam, Ahmad ameihakikishia serikali kuwa hakuna mabadiliyo yoyote ya ratiba yatakayofanyika kuhusu wenyeji wa michuano hiyo na kwamba CAF itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha michuano hiyo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mechi zote za michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika jijini Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi kushiriki katika mashindano makubwa kama hayo kwa kuwa yanasaidia kwenye ukuzaji wa vipaji kwa vijana ambao wengi wao ni wanafunzi.

Rais huyo wa CAF Ahmad Ahmad yupo nchini kwa ajili ya kuongoza mkutano maalum wa mabadiliko ya katiba ya Baraza la Vyama vya Soka katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam unahudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wanachama wote 12 wa CECAFA.