Waziri Bashungwa asisitiza Uhuru wa vyombo vya habari uendane na wajibu

Vituo vya Utangazaji

0
2302

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uhuru wa vyombo vya habari akisisitiza uhuru huo kuenda sambamba na wajibu.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo wakati akizindua kituo cha matangazo mjini Kahama mkoani Shinyanga kilichopewa jina la Gold Fm ikiwa na kauli mbiu ya Sauti ya dhahabu.

Akizungumza katika mahojiano maalum mara baada ya uzinduzi wa kituo hicho Waziri Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inathamini na kuamini katika uhuru wa vyombo vya habari kupaza sauti za watanzania ili kuyafikia matamanio yao.

Innocent Bashungwa-Waziri wa habari, utamaduni,sanaa na michezo

Waziri Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita kwa kuthamini uhuru wa vyombo vya habari inakusudia kuondoa asilimia 50 ya ada za tozo mbalimbali za leseni kwenye marekebisho ya kanuni za maudhui ya mtandaoni na maudhui ya utangazaji katika redio na televisheni

Wamiliki wa mitandao ya kijamii kama YouTube ambayo maudhui yake siyo ya kihabari wataruhusiwa kupakia video zao mitandaoni bure, kama sehemu ya kuwawezesha kujitangaza na kujiingizia kipato zaidi” ameongeza Waziri Bashungwa

Akizungumzia uwekezaji huo waziri Bashungwa amesema ana furaha kuona uwekezaji wa namna hii unaenda sehemu husika, na endapo watahitaji kuanzisha kituo cha televisheni waanze mapema na wakihitaji msaada waseme maana hiyo ndiyo kazi ya Serikali.