Wasanii wakosa mikopo kwa kutokuwa na elimu ya uwekezaji

0
423

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema imetoa asilimia 11.6 tu ya mikopo yote iliyoombwa na wasanii mbalimbali kati ya Julai 2022 hadi Aprili 2023 kutokana na waombaji kutokuwa na elimu ya uwekezaji.

Hayo yameelezwa na Waziri Pindi Chana bungeni jijini Dodoma ambapo ametaja sababu nyingine kuwa ni waombaji kutorasimisha miradi yao, kutokuwa na uelewa wa uandishi wa miradi, kutokuwa na kumbukumbu za mapato na matumizi, kutokuwa na elimu ya fedha, usimamizi mbovu wa miradi na kutokuwa na uhakika wa masoko ya kazi walizoziombea mitaji.

Katika kipindi hicho, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ulipokea maombi ya mikopo yenye thamani ya shilingi Milioni 9.2 kutoka kwa waombaji 219. Hadi Aprili, 2023 mfuko ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi Milioni 1.07.

Kupitia mkopo huo, mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Studio 21zilizowezeshwa ikiwemo kununua vifaa vya kisasa vitakavyoweza kuzalisha kazi zenye ubora unaotakiwa na kumewaondolea wasanii usumbufu na gharama za kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta sehemu za kuzalisha kazi zao.

Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewasilisha bajeti ya shilingi Bilioni 35.4 ili kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.