Warriors wapoteza kwa Dallas Mavericks

0
1081

Golden State Warriors wameendelea kuwa na msimu mbaya zaidi katika historia ya timu hiyo kwenye Ligi ya Kulipwa ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani (NBA) baada ya alfajiri ya kuamkia leo kunyukwa alama 142 kwa 94 na Dallas Mavericks.

Luka Doncic amefunga alama 35 na kucheza Rebounds yani mipira iliyorudi Kumi, huku Tim Hardway Jr akifunga alama nyingine Ishirini na kulizamisha kabisa jahazi la Warriors lililokuwa likiongozwa na Erick Paschall aliyefunga alama 22 na kucheza Rebounds Saba.

Kwingineko Fred Vanvleet amewaongoza Mabingwa Watetezi Toronto Raptors kupata ushindi wa alama 113 kwa 97 dhidi ya Orlando Magic akiifungia alama 24 na Terence Davis akifunga nyingine 19.

Katika matokeo mengine Cleveland Cavaliers wamepoteza kwa alama 124 kwa 100 mbele ya Miami Heat wakati Brooklyn Nets wakiinyuka Charlote Hornets alama 101 kwa 91 na Milwaukee Bucks wakiitandika Atlanta Hawks alama 135 kwa 127.