Timu ya Soka ya Biashara United ya Mkoani Mara imemtambulisha rasmi, Vivier Bahati raia wa Burundi kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo kwa kipindi cha miezi sita.
Kocha huyo ametambulishwa hii leo Januari 18, 2022 katika makao makuu ya timu hiyo yaliyopo Kata ya Mukendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Katibu wa Biashara United, Khaji Mtete amesema kuwa, timu hiyo ilifanya mchakato wa kutafuta kocha mpya baada ya kocha aliyekuwepo Patrick Odhiambo raia wa Kenya kuondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Mtete amesema kuwa, kocha Vivier mwenye leseni B ya CUF atahudumu kwa kipindi cha miezi sita ambapo timu ikiridhishwa itaingia naye kandarasi ya kipindi kingine kuinoa timu hiyo.
Kwa upande wake Kocha Vivier Bahati amesema kuwa, amefurahi kupata nafasi ya kuinoa timu hiyo ambapo amesema hali ya timu hiyo si nzuri licha ya kucheza mpira mzuri lakini ameahidi kupambana kuhakikisha timu inakuwa na matokeo mazuri.
“Tunaomba ushirikiano kwa wana Mara wote wanaoipenda timu, ninaamini Mungu atatufungulia mlango kutokana na nguvu na juhudi zetu kwa pamoja zitaiweka Biashara United kuwa sehemu nzuri,” amesema.