Vita ya maneno baina ya Zidane na PSG yaendelea

0
1193

Kocha wa Klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania, – Zinedine Zidane amesema kuwa, hatotengua kauli yake iliyomtia katika vita ya maneno na Klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, aliposema nyota wa klabu hiyo Kylian Mbappe ana ndoto za kuichezea Real Madrid.

Hivi karibuni Zidane maarufu kama Zizzou alitamka wazi kuwa Mfaransa mwenzake Kylian Mbappe ana ndoto ya siku moja kuichezea Real Madrid, kauli ambayo viongozi wa PSG wakiongozwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Michezo Leonardo Araujo hawajaipenda.

Baada ya kauli hiyo ya Zidane, Leonardo amemtaka Zidane aache kumchanganya Mbappe, lakini Zidane mwenyewe ameshikilia msimamo wake ambapo amesema kuwa yote aliyosema ni mambo ambayo Mbappe ameshayatamka mwenyewe kwamba ni ndoto yake siku moja kuvaa jezi nyeupe za Real Madrid.

Zidane ameongeza kuwa, alichokisema kinabaki kama kilivyo na atarudia kila siku na kwamba anaweza kusema chochote anachotaka ilimradi hakivunji misingi ya maadili ya taaluma yake.