Serikali imesema itawachukulia hatua za kisheria, wale wote watakaobainika kuhusika na upotevu wa mapato katika uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru jijini Dar es salaam wakati wa mechi za mpira wa miguu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amesema kuwa, pamoja na kuongezeka kwa mapato katika mechi ya Yanga na Simba iliyochezwa hivi karibuni katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kufikia shilingi milioni 545.4, bado serikali imebaini mianya ya upotevu wa mapato katika uwanja huo.
“Serikali inawaonya wale wote waliokuwa wanashiriki katika kuvujisha na kufanikisha upotevu wa mapato wakati wa mechi katika uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru, na kwamba haitasita kuchukua hatua kali dhidi yao pale watakaobainika”, amesema Dkt Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt Abbasi, serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu uvujishaji na upotevu wa mapato katika viwanja hivyo ili kuziba mianya yote, na tayari baadhi ya njia zinazotumika zimebainika.
Amesema kwa upande wa watendaji watakaobainika kujihusisha na uvujishaji na upotevu wa mapato, nao watachukuliwa hatua kali bila kujali nafasi zao na maeneo wanayosimamia.