Turan ahukumiwa kwenda jela miaka Mitatu

0
847

Kiungo wa klabu ya FC Barcelona ya nchini Hispania , – Arda Turan amehukumiwa kwenda jela miaka Mitatu, kwa kosa la kufyatua risasi katika hospitali moja nchini Uturuki.

Turan ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo kwenye klabu ya Istanbul Basaksehir, mwaka 2018 akiwa katika klabu moja ya usiku aligombana na Berkay Sahin ambaye ni Mwanamuziki mashuhuri nchini Uturuki, ugomvi uliosababisha nyota huyo wa muziki kuvunjika pua na
kupelekwa hospitali kwa ajili ya upasuaji.

Kwa mujibu wa mke wa Sahin, ugomvi huo haukuishia katika klabu hiyo ya usiku, bali Turan alifunga safari mpaka hospitalini na akafyatua risasi sakafuni wakati nyota huyo akiwa kwenye harakati za kupelekwa
wodini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa pua iliyovunjika wakati wa ugomvi huo.

Mwanandinga huyo amehukumiwa kwa kosa la kufyatua risasi na kusababisha taharuki ikiwa ni kinyume na sheria ya umiliki wa silaha, lakini pia kwa kusababisha majeraha makubwa kwa Mwanamuziki huyo wa Uturuki.

Mahakama nchini Uturuki imemuhukumu Turan kwenda jela miaka mitatu, lakini hata hivyo hatotumikia adhabu hiyo gerezani hadi hapo atakapopatikana na makosa mengine katika kipindi kisichopungua miaka Mitano ijayo.

Klabu ya Istanbul Basaksehir imemtoza Turan faini ya Lira Milioni 2.5 za Uturuki ambazo ni sawa na Paundi Laki Tatu na Nusu kutokana na tukio hilo na yeye mwenyewe Turan ameomba radhi kufuatia kitendo hicho.