Timu nne zagawana alama Ligi Kuu Tanzania Bara

0
363

Timu nne zilizoshuka dimbani leo katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara zimemaliza michezo yao kwa kutoka sare ya goli 1-1.

Mchezo wa kwanza uliopigwa saa nane mchana katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi umezikutanisha timu za Namungo FC dhidi ya KMC FC. Watoto wa jiji la Dar es Salaam (KMC) ndio waliokuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa na Charles Ilanfya dakika ya 30 , na wakulima wa Korosho (Namungo) wakasawazisha dakika ya 43 kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Shiza Kichuya.

Kwa matokeo hayo Namungo imepanda hadi nafasi ya tano ikiwa na alama tano baada ya michezo minne, huku KMC ikipanda hadi nafasi ya 14 kutoka 16, ikiwa na alama 2 baada ya michezo minne.

Mchezo wa pili umezikutanisha Geita Gold FC dhidi ya Mbeya City FC ambapo Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata goli dakika ya 45 kupitia kwa Juma Luzio. Geita Gold ilisawazisha dakika 12 baadaye kupitia kwa George Mpole.

Kwa matokeo hayo, Mbeya City imepanda na kufikia na kufikia nafasi ya sita ikiwa na alama sita baada ya michezo minne. Geita Gold imepanda kutokana nafasi ya 15 hadi nafasi ya 13 ikiwa na alama mbili baada ya kucheza michezo minne.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Polisi Tanzania. Mchezo huo utarushwa mbashara kupitia TBC FM kuanzia saa 10:00 jioni.