Serikali imelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha vilabu vinakuwa na Wataalamu wenye uwezo wa kutoa tiba za michezo kwa wachezaji ili kulinda afya za Wachezaji wawapo michezoni.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza Bungeni jijini Dodoma, wakati wakijibu swali la Mbunge wa Temeke,- Abdallah Mtolea aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha kuwa kila klabu hapa nchini inakuwa na Madaktari wa michezo kwa ajili ya kuwahudumia Wachezaji.
Naibu Waziri Shonza amesema kuwa, TFF inapaswa kuhakikisha kila klabu inakuwa na Wataalamu wa afya za michezo waliothibitishwa.
Kuhusu suala la kuwawekea Bima Wachezaji, Naibu Waziri huyo wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa, serikali imefanikiwa kuwawekea bima Wachezaji pamoja na kuwapima afya zao hasa panapokuwa na mashindano makubwa.
Naibu Waziri Shonza pia ameishauri TFF kutafuta baiskeli za miguu mitatu (Bajaji) ili ziweze kutumika kama gari za kubeba wagonjwa kwenye viwanja mbalimbali vya michezo badala ya kutegemea magari ya kubeba wagonjwa ambayo kwa baadhi ya maeneo ni vigumu kupatikana.