Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema kuwa beki wa Taifa Stars, Erasto Nyoni amerejea nchini kuendelea na matibabu baada ya wataalamu kushauri hivyo.
Taarifa ya TFF imekuja baada ya baadhi ya mashabiki kuhoji sababu za nguli huyo kurejea nchini na kukiacha kikosi cha Taifa Stars nchini Cameroon ambako kinashiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
“Mchezaji Erasto Nyoni amepewa ruhusa ya kuondoka kwenye kambi ya Taifa Stars, amerudi nyumbani kuendelea na matibabu baada ya kushauriwa na jopo la madaktari wa timu,” imeeleza tarifa ya TFF.
Hata hivyo tarifa hiyo haikueleza kuwa beki huyo kisiki anasumbuliwa na tatizo gani.
Nyoni ni mchezaji pekee aliyebaki kwenye kikosi cha Taifa Stars ambaye alikuwemo katika kikosi kilichoshiriki CHAN 2009 nchini Ivory Coast.